Thursday, November 17, 2011

Vijana Chadema watoa kauli nzito, kuandamana bila kikomo

BARAZA la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limepinga kitendo cha Bunge na Serikali kushinikiza muswada wa mchakato wa kuundwa kwa Katiba Mpya kusoma kwa mara ya pili bungeni, kwani bado unadosari kubwa.

BAVICHA wametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya utendaji wa taasisi hiyo iliyokuwa ikijadili na kuangalia mchakato wa muswada wa kuelekea kuundwa kwa Katiba Mpya.

Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa BAVICHA, John Heche imeeleza kuwa ili kuonesha kuwa BAVICHA haikubaliano na kitendo cha muswada huo kusomwa kwa mala ya pili bungeni itaungana na wananchi na wanaharakati kupaza sauti zao kuupinga muswada ikiwemo kufanya maandamano ya bila kikomo nchi nzima.

“Muswada uliosomwa bungeni jana ni batili kwa kuwa ulipaswa kusomwa kwa mara ya kwanza ili kutoa fursa pana kwa wananchi kuujadili kwani ule wa awali ulikataliwa na Serikali kuamriwa na wananchi kwenda kuuandaa tena mpya na kuingizwa baadhi ya maoni taliotolewa na wananchi,” alisema Heche.

Heche katika taarifa hiyo ya BAVICHA pia wamepinga kitendo cha wanafunzi 12,000 kunyimwa mikopo na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa visingizio kuwa hawana sifa. Amesema kitendo hicho si cha kiungwana kwani hadi sasa bodi hiyo haina uwezo kubaini mwanafunzi masikini ni yupi na tajiri ni nani.

Katika hatua nyingine BAVICHA imepinga kitendo cha baadhi ya viongozi wa Serikali kuwatimu wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga kwa madai kuwa wanasafisha miji kama ilivyotokea mjini Mbeya hivi karibuni.

“Tunapinga unyanyasaji wa wafanyabiashara ndogondogo nchini na pia tunalaani kitendo cha matumizi ya nguvu kubwa kwa wamachinga wa jiji la Mbeya, BAVICHA inaitaka Serikali kuwatengea maeneo maalumu ya wamachinga kufanya biashara zao ambayo yatakuwa ni rafiki kwa biashara zao,” amesema Heche.

No comments: