Friday, November 4, 2011

Tanzania yakataa misaada ya ushoga

TANZANIA imetoa msimamo kuwa haiko tayari kuhalalisha vitendo vya kishoga kwa vigezo vya kupata misaada ya maendeleo.

Msimamo huo ulitangazwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alipokuwa akijibu tamko la Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.

“Tupo tayari kwa lolote, hatuwezi kuvunja utaifa wetu kwa nchi yoyote tajiri kutoa masharti ya
kipuuzi ili tushibe matumbo yetu, kama wanadhani misaada ndiyo silaha yao wakae na pesa zao,” aling’aka Membe.

Cameron katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) hivi karibuni, alitishia kufuta misaada katika nchi ambazo zinapinga ushoga.

Katika vitisho hivyo, Cameron alisema mataifa ambayo yanapata msaada kutoka Uingereza, lazima yakubaliane na ushoga ambao aliuita sehemu ya utekelezaji wa haki za binadamu.

Lakini Membe aliweka wazi kuwa Tanzania bila kujali vitisho vya Cameron, itaendelea kupinga vitendo hivyo kwa kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya shughuli za Serikali za kulinda utaifa wa nchi.

Sheria za nchi
Waziri Membe alisema Tanzania haihitaji mjadala mrefu kuhusu suala hilo, kwa kuwa sheria ya nchi inatamka wazi kuwa ndoa ni uhusiano unaotambulika kati ya jinsi mbili tofauti.

Alifafanua kuwa Sheria za Makosa ya Jinai zinakataza ndoa za jinsi moja na ni makosa ambayo mtu akitiwa hatiani, adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka 30.

Membe alikumbusha kuwa sheria hizo si zinatumika Tanzania tu, lakini pia zilitungwa na Waingereza wenyewe wakati wakiitawala Tanganyika.

Ulinzi wa utamaduni
“Nchi hii inafuata utamaduni, kanuni na sheria na hatupokei amri au ushauri unaoingilia utamaduni wa nchi yetu kwa visingizio vya misaada,” alisisitiza Membe.

Alisema tamko hilo linahatarisha kuvunja uhusiano kati ya nchi na nchi kwa kuwa wamehusisha misaada ya maendeleo na ushoga.

Ushoga Jumuiya ya Madola
Kwa mujibu wa Membe, suala la ushoga halikuwa ajenda katika mkutano wa Jumuiya ya Madola wiki iliyopita na wala halikuzungumzwa.

Lakini alisema katika vikao vyao vya awali vya mkutano huo, chama tawala cha Uingereza, Conservative, kilichomekea mada hiyo.

Alisema katika kujadili utaratibu wa mkutano huo wa Jumuiya ya Madola, chama hicho alichosema kinashabikia ushoga, kilipenyeza masuala ya haki za binadamu kwa kila mtu kuwa na uhuru wa kufanya anachotaka kwa mafumbo tu.

Hatima ya Jumuiya ya Madola
Membe alisema tamko hilo ni hatari kwa Jumuiya ya Madola, kwani linaweza kuvunjika kutokana na ukweli kuwa suala hilo halikujadiliwa katika vikao rasmi vya jumuiya hiyo vilivyofanyika hivi karibuni.

Alisema Cameron atawajibika iwapo jumuiya hiyo itavunjika kwani kati ya nchi 54 za jumuiya hiyo, nchi 13 pekee ndiyo zinashabikia ushoga wakati 41, ikiwemo Tanzania, hazishabikii.

Jaribio la balozi shoga
Akielezea harakati za mataifa ya kigeni kutaka kuingiza utamaduni huo aliouita wa kipuuzi katika mfumo rasmi wa Serikali, Membe alisema mwanzoni mwa mwaka huu, Serikali
iliimkataa balozi wa nchi kubwa rafiki ambaye alikuwa akijihusisha na ushoga.

Alisema Tanzania ilipokea barua kutoka nchi hiyo ambayo ni rafiki kuwa anakuja balozi ambaye ameoa mwanamume mwenzake.

Baada ya kupokea barua hiyo, Membe alisema alimpelekea Rais Jakaya Kikwete na baada ya Rais kuisoma, alisema: “Toba yarabi” na kutoa agizo la kumkataa balozi huyo.

Shein naye alaani
Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ), Dk Ali Mohamed Shein, akizungumza na wanahabari Ikulu Zanzibar jana, alisema masharti ya ushoga kwa Zanzibar ni kitu kisichowezekana kabisa.

“Zanzibar inafuata maadili ya dini ya kiislamu na mila zake … wakate misaada yao wakitaka na kamwe hatutakwenda kuomba misaada kama masharti ndiyo hayo … najua hata jamii ikiulizwa itajibu hivyo hivyo,” alisema Shein.

Alisema hata kwa Zanzibar kulitaja neno hilo (ubaradhuli) ni mwiko na katika utamaduni wa visiwani halipo kabisa na kwamba kama hiyo ndiyo haki za binadamu basi haitawezekana.

Kuiunga mkono al Shabaab
Katika hatua nyingine, Membe alisema Serikali iko tayari kutoa msaada wowote kwa Kenya katika kulikabili kundi la al Shabaab la Somalia.

Alisema katika mkutano utakaofanyika Novemba 20, Kenya watatoa taarifa ya majeshi yake Somalia na katika mkutano huo wa siri Nairobi, Serikali ya nchi hiyo itaelezea matatizo na kinachohitajika ili kupewa msaada.

Oktoba 28, vikosi vya Kenya vilipambana na wanamgambo wa al-Shabaab ndani ya Somalia kwa mara ya kwanza tangu kuvuka mpaka na kuingia nchini humo.

1 comment:

Anonymous said...

source?????