Monday, December 5, 2011

CAG alalamikia fasheni ya ukaguzi maalumu

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ameonya kuwa endapo watendaji wanaosababisha uwepo wa ukaguzi maalumu hawatadhibitiwa mapema, ukaguzi wa hesabu hautakuwa na tija kwa taifa.

Amelalamikia kuelemewa na shughuli za ukaguzi maalumu zinazoongezeka katika ofisi yake kila kukicha.

Utouh alisema hayo juzi Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya mwezi mmoja kwa wakaguzi wapya 100.

Alisema ni lazima Serikali ichukue hatua kukomesha usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo katika ngazi za vijiji, kata na Serikali za Mitaa kwa ujumla, vinginevyo ubadhirifu utaendelea licha ya kulundikana kwa ukaguzi maalumu.

Kwa mujibu wa Utouh, kukithiri kwa usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo serikalini ndio chanzo kikuu cha kuongezeka kwa ukaguzi maalumu unaoilazimisha ofisi yake kuondoka katika utaratibu wa ukaguzi wa kawaida.

Kwa sasa kwa maelezo ya Utouh, ofisi hiyo inalazimnika ‘kubeba mzigo’ wa ukaguzi maalumu usio na uwiano na nguvu kazi ndogo aliyonayo wala tija kwa Taifa.

“Imekuwa ni mtindo wa kawaida sasa hivi kwa kila ofisi kudai ukaguzi maalumu wa miradi yake ya maendeleo, huu sio utaratibu wa kawaida wa kufanya kazi kwa sababu hauna tija kwa taifa.

“Cha msingi wanaosimamia miradi katika vijiji, kata na Serikali za Mitaa wajirekebishe na kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya kuachia mianya ya rushwa na ubadhirifu mwingine, inayosababisha miradi kutokuwa na thamani halisi,” alisema Utouh.

Alisema hata kama ukaguzi maalumu utatekelezwa kwa wingi kiasi gani, wasimamizi wa miradi
wasipomulikwa, kukemewa na kulazimishwa wabadilike na kuweka maslahi ya umma mbele, ukaguzi huo utaendelea kuongezeka huku thamani ya miradi inayokamilika ikiendelea kufanyiwa ubadhirifu na kushuka.

“Ukaguzi maalumu sio ishara nzuri kwa wasimamizi wanaojali kazi yao na kupenda maendeleo, zinamaanisha kuna walakini na kuonesha ishara ya kutotendeka vizuri kwa jambo fulani. “Wasimamizi wa miradi katika vijiji, kata na Serikali za Mitaa wasitengeneze mazingira ya kutoaminiwa kiasi hicho kwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo,” alisema Utouh.

Alisema Serikali imejitahidi kumwongezea vijana wengi wa kazi, lakini hapati ahueni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya ukaguzi maalumu unaoibuka kila kukicha.

“Kwa mtindo huu wa ukaguzi maalumu, hata nikipewa idadi gani ya wakaguzi, mzigo wa kazi
utakuwa ni mzito tu kwa ofisi yangu kwa sababu inakuwa kama fasheni. “Sasa kwa jinsi wafanyakazi wanavyoongezeka ndio ukaguzi maalumu unavyoongezeka, pia kutokana na wasimamizi wa miradi kuongeza kasi ya usimamizi mbovu,” alisema na kuongeza kuwa
kazi haiwezi kuwa na tija kwa staili hiyo.

Katika hatua nyingine, aliwataka wakaguzi wapya kutekeleza majukumu yao hata wakiwa nje ya makao makuu kwa kuwa maeneo hayo yanatambuliwa pia kuwa ni mahali pa kazi.

Aliwataka waondokane na dhana ya kufanya kazi katika makao makuu tu au kwenye miji mikubwa kwa sababu mchango wao unahitajika katika maeneo yote ya nchi.

Mafunzo hayo yalijumuisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Teknohama) katika ukaguzi wa hesabu pamoja na mambo mengine mbalimbali yanayohusu taaluma hiyo.

No comments: