Tuesday, November 30, 2010

Kikwete awaonya Mawaziri

WAKATI Rais Jakaya Kikwete akiwa katika ngwe yake ya mwisho ya uongozi wa nchi ameonesha kuwa mkali kwa mawaziri wake wapya aliowateua hivi karibuni.

Kikwete amewaeleza wazi kuwa safari hii hana simile wala subira kwa Waziri atakayeboronga katika utekelezaji wa majukumu yake.

Rais Kikwete ametoa msimamo wake wakati anawapa majukumu mapya mawaziri hao na akagusia nyanja mbali mbali zikiwemo uwajibikaji, kufuata kanuni, sheria na pia kupambana na rushwa huku akisisitiza kuwa vita dhidi ya rushwa ni suala la kikatiba na kuwataka kuhakikisha kuwa Mpango wa Pili wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa (NACSAP-11) unatekelezwa.

Akizungumza na Mawaziri na Naibu Mawaziri Ikulu Dar es Salaam jana, Rais Kikwete aliwaeleza mawaziri kuwa katika kipindi hiki cha pili cha uongozi wake hakutakuwa na muda wa kupoteza.

Amesema, hatakuwa tayari kukubali maelezo ya kwa nini utekelezaji wa majukumu ya msingi umeshindikana na amewataka mawaziri kusimamia mapato ya Serikali yasiyotokana na kodi na kudhibiti matumizi ya Serikali.

Pia aliwataka viongozi hao kuzingatia maadili ya uongozi ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria za nchi, kuheshimu sheria katika shughuli na mambo yao binafsi na kutunza siri za Serikali kwa mujibu wa kiapo chao.

Rais Kikwete pia alisisitiza umuhimu wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuwasiliana na wananchi kwa maana ya kueleza mafanikio na mipango ya Serikali katika kushughulikia matatizo ya wananchi.

Rais Kikwete aliwataka mawaziri hao kuvitumia kikamilifu vitengo vya mawasiliano ya Serikali katika wizara zao ambavyo ndivyo vyenye jukumu la kutoa taarifa kuhusu Wizara inavyotelekeza majukumu yake.

“Uzoefu unaonesha kuwa mawaziri wengi ni wazito kufanya mawasiliano na wananchi hata pale ambako Wizara imefanya mambo mengi mazuri. Hivyo, mawaziri muwe mstari wa mbele kuelezea mafanikio ya utendaji wa Serikali katika Wizara zetu,” alielekeza Rais Kikwete na kuongeza:

“Lazima ujengwe utamaduni wa kudumu wa kuwasiliana na wananchi wote ambao ndio waajiri wetu kupitia kura zao. Mawaziri wote tumieni vitengo vyenu vya mawasiliano na vyombo vya habari kwa ustadi ipasavyo”.

Akiwapongeza kuteuliwa kwao, Rais Kikwete alisema: “Mnastahili pongezi hasa ukizingatia ukweli kwamba nyinyi mmebahatika kuteuliwa kutoka kwenye orodha ndefu ya wabunge wengi wenye sifa za kushika nafasi mlizo nazo.

Nimewateua kwa imani kuwa pamoja nanyi, tutatimiza matumaini ya wananchi wa Tanzania waliokichagua Chama Cha Mapinduzi kiendelee kuongoza nchi yetu".

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, wakati akizungumza na wakuu wa idara katika wizara yake baada ya kutoka Ikulu aliwaambia kutokana na msimamo huo wa Rais Kikwete, yeye na naibu wake, hakuna kulala hadi matarajio ya wananchi katika wizara hiyo yatakapopatiwa ufumbuzi.

Dk. Kawambwa aliahidi changamoto ya kwanza kufanyia kazi ni kuhakikisha mikopo inayotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu inaboreshwa, ili kuondoa malalamiko yasiyokwisha kutoka kwa wanafunzi hao.

Akiwa amefuatana na Naibu Waziri wake, Phillip Mlugo, Dk Kawambwa alikiri kuwapo tatizo kubwa la utoaji mikopo, hali iliyofanya wanafunzi karibu wote wa vyuo vikuu kuinyima kura CCM katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu. Licha ya mikopo pia aliahidi kuhakikisha maslahi ya walimu yanaboreshwa ili kuondoa uwezekano wa walimu kugoma.

“Natambua kuwa watoaji na wapokeaji elimu, wote wako kwenye matatizo, hili eneo nitashughulika nalo zaidi.

“Leo tulikuwa na mkutano na Rais (Kikwete) ametwambia wazi, kuwa safari hii hana simile wala subira, anachotaka ni watu tufanye kazi. Na sisi tunakuja hapa kwa hadhari kuwa hakuna kulala,” alisema Dk Kawambwa ambaye awali alikuwa Wizara ya Miundombinu.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Cyril Chami, akianza kazi rasmi aliahidi kuandika waraka kwa Baraza la Mawaziri, kuomba Serikali iboreshe viwanda ikiwamo kufufua vilivyokufa kwa kuvichukua na kurudi kwenye miliki yake.

Waziri huyo ambaye amepandishwa kutoka Naibu Waziri katika wizara hiyo, alisema:“Miaka mitatu nyuma, tulifanya ukaguzi wa viwanda vyote na tukajua kwa nini vingine vilifungwa au havijaanza kazi na sasa tunataka vifanye kazi”.

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kupokewa rasmi wizarani hapo na wafanyakazi huku akifuatana na Naibu wake, Lazaro Nyalandu, alisema baadhi ya viwanda vilivyoshindwa kufanya kazi vitawezeshwa ili vifufuke.

“Kuna viwanda vingine tumeona wamiliki wameshindwa kuzalisha bidhaa walizoomba awali na wanataka kubadili aina nyingine, nao tutawasaidia wazalishe wanachoweza baada ya kutetea hoja zao,” alisema.

Kwa upande wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, wakati akizungumza na wafanyakazi wa wizara yake, alisema baada ya miaka miwili, watu watajua upole na ujana wake ukoje, kwani anaamini atakuwa amefanya kazi vizuri na kwenye hilo, hana shaka nalo.

Alisema licha ya kutegemea kuteuliwa katika wizara hiyo nzito, atatekeleza Ilani ya CCM kwa kasi zaidi, huku akiahidi kuhakikisha sheria zote zilizotungwa kusimamia maliasili vikiwamo vitalu na wanyamapori zinasimamiwa ipasavyo.

Alisema anaamini kutokana na kuwekwa sheria za uwazi na shirikishi, mianya ya rushwa na vitendo vyake wizarani hapo vitakwisha.

Kwenye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Waziri Dk Haji Mponda, aliwataka wafanyakazi wa wizara hiyo, kushirikiana kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Dk Mponda alitaja changamoto kubwa kwa wafanyakazi wa sekta hiyo kuwa ni kutoa huduma bora za tiba katika vituo vyote vya afya nchini ili kuinua uchumi wa nchi “Mtanzania wa leo anataka huduma bora za tiba … mtu anapoingia hospitalini au kwenye zahanati anachotaka ni kumwona mganga na kupata huduma bora, hivyo kila mtoa huduma hana budi kuwajibika katika hilo.”

Miongoni mwa mawaziri walioanza kazi kwa cheche ni wa Ujenzi, John Magufuli ambaye juzi aliagiza Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kusimamisha nafasi za kazi za mameneja wa mikoa zilizotangazwa kwenye vyombo vya habari na kuamuru mameneja wote waliosimamishwa kazi warejee kazini.

Wakati huo huo, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mashirika yapatayo 50 yanayotetea usawa wa kijinsia, haki za binadamu na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct), yamepongeza uteuzi wa mawaziri na naibu mawaziri uliofanywa na Rais Kikwete Novemba 24 mwaka huu.

Hata hivyo, taarifa ya FemAct iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, ilielezea kutoridhishwa na idadi ndogo ya mawaziri wanawake na pia ukubwa wa Baraza hilo kwa jumla.

“Idadi ya wanawake walioteuliwa kuwa mawaziri ni ndogo sana. Katika uteuzi huu, jumla ya mawaziri ni 29, kati yao wanaume ni 22 sawa na asilimia 76 na wanawake ni wanane, sawa na asilimia 24.

“Naibu mawaziri ni 21, wanaume ni 18 sawa na asilimia 86 na wanawake ni watatu sawa na asilimia 14. WanaFemAct walitarajia kuwa hiki kilikuwa kipindi mwafaka cha kufikia uwiano wa 50:50 ingawa mikakati iliyowekwa na fursa zilizokuwapo hazikutoa fursa hiyo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

2 comments:

Anonymous said...

I likе the helpful іnfo you prоvide for yοur artіcles.
I will bookmark your weblog and cheсk again right
here frequеntlу. I am fairly ѕurе
I will leаrn lots of new stuff right right here!
Good lucκ foг the following!

My site: Www.Hcg-Injections.com/

Anonymous said...

Hmm it looks like your blog ate my first comment (it was super long) so I guess I'll just sum it up what I submitted and say, I'm thoroughly enjoying your blog.

I as well am an aspiring blog writer but I'm still new to everything. Do you have any helpful hints for beginner blog writers? I'd really
appreciate it.

Feel free to visit my web-site ... travel