Friday, November 5, 2010

LOWASSA AMJIBU DR. SLAA

TAARIFA RASMI KWA VYOMBO VYA HABARI NOVEMBA 5, 2010

Novemba 3, 2010 mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa aliwatuhumu makada 30 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa walifanya kikao cha kupanga mipango ya kumwibia kura mjini Mwanza. Kati ya makada aliowatuhumu ni pamoja na
mimi.

Napenda kuufahamisha umma kuwa habari hizi si za kweli kwa sababu mwezi wote wa Oktoba, nilikuwa jimboni kwangu nikifanya kampeni za kuwania kiti cha Ubunge katika Jimbo la Monduli. Sikupata kusafiri kwenda Mwanza hata siku moja, na siku aliyoitaja ya Oktoba 19, nilikuwa katika vijiji vya Mfereji na Enguiki nikifanya kampeni siku nzima.

Ukiacha tuhuma hizo, pia upo uvumi uliosambazwa kwamba nilishiriki kikao cha mikakati ya kuchakachua kura, mjini Arusha kumsaidia mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Batilda Burian aweze kushinda kiti hicho. Nasema uvumi huu ni uzushi na si wa kweli.

Kutokana na yote haya, ninakwazika kwamba inaonekana katika nchi yetu umeanza kuingia utamaduni mpya wa kufanya siasa za uongo, uvumi, uzushi na kila aina ya hila kwa nia ya kujipatia ushindi. Kwa uzoefu wa mataifa mengi yaliyotuzunguka, ndani ya Afrika na sehemu nyingine duniani, amani hupotea kutokana usambazaji wa taarifa za uongo.

Mwasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alituachia amani na utulivu ambavyo ni tunu ya taifa hili.

Dalili zinazoonekana, kuna watu wanaelekea kuchoshwa na amani iliyopo.

Wanajiandaa kufanya vurugu, kuliingiza taifa hili katika machafuko, na sijui wanafanya hivyo kwa faida ya nani.

Wito wangu kwa Watanzania, ni kwamba tusiichoke amani. Amani tuliyonayo ndiyo imetutofautisha na mataifa mengi yaliyotuzunguka na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kupigiwa mfano. Tuelekeze nguvu zetu katika shughuli halali za kutuletea kipato zisizoharibu amani yetu.

Tukiiharibu amani tuliyonayo, mwisho wa siku nchi yetu itateketea na sote hatutakuwa salama. Tutakuwa tumekwisha.

Mwisho, namsihi Dk. Slaa ajipe muda wa kuzifahamu vyema siasa za nchi hii. Asidanganywe na mahudhurio ya mikutano ya hadhara akadhani ndizo kura katika masanduku ya kupigia kura. Namsihi ajifunze` zaidi jinsi ya kufanya siasa za kistaarabu bila kueneza uvumi, uongo, chuki na uzushi vyenye kutetelesha amani ya nchi yetu. Mungu ibariki Tanzania.


Edward Lowassa
Mbunge Mteule wa Monduli

2 comments:

Elinora Herman said...

Ni vyema mjue kwamba, lisemwalo lipo, huu si uzushi ninaamini kuwa mtu hawezi kusema kitu tuuuuuuuuu. bali ukweli utabakia kuwa palepale.msijitafutie namna ya kujiosha kwa wananchi. Dr slaa si muongo ni mkeli mbona hamtaki kumpeleka mahakamani.mim ninaamini kingacho ni dhahabu.peoples power

Mbele said...

Ni kweli kuwa Mwalimu Nyerere alitujengea msingi wa amani. Lakini Mwalimu huyo huyo hatimaye alitutahadharisha kuwa CCM ni tishio kwa amani na usalama wa nchi yetu. Soma hapa.