Thursday, November 4, 2010

Uspika: Makinda sasa amvaa Sitta

Kinyang'anyiro cha kiti wa Spika wa Bunge la Tanzania kimeanza kwa kishindo na safari hii Naibu Spika wa Bunge aliyemaliza muda wake, Anne Makinda, ameamua kupambana na aliyekuwa bosi wake, Spika anayemaliza muda, Samuel Sitta.

Jana Makinda aliithibitishia NIPASHE kwa njia ya simu kuwa amechukua fomu za kuomba ridhaa ya chama chake, CCM, kuwania kiti hicho.

Hata hivyo alisema kuchukua fomu si hoja, bali kurudisha.

Ingawa Makinda alichukua fomu hizo mapema ofisi ndogo makao makuu CCM Lumumba, hakutaka taarifa zake zitangazwe wazi.

Sitta alichukua fomu hiyo jana saa 8:45 mchana.

Alikabidhiwa fomu hizo na Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi CCM, Mattson Chizi, ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, alizijaza na kuzikabidhi ilipotimu saa 9:45 alasiri.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi fomu hiyo, Sitta alisema, ikiwa atapata nafasi kwa mara nyingine mipango aliyonayo ni kuliimarisha Bunge ili liendelee kukubalika kuwa ni chombo makini na hasa kinachotetea makundi maalum kama wangonge vijijini, vijana na wafanyakazi wa kawaida.

“Hii inatokana na falsafa ya CCM, mawazo ya hayati baba wa Taifa, Julius Nyerere, ili yawepo maendeleo lazima tuende pamoja tusiwe na makundi kwani ukiishi kwenye makundi ni kuwatelekeza Watanzania,” alisema.

Akizungumzia kuhusu makundi ya wanaharakati wanaotaka kumng'oa kwenye nafasi hiyo, Sitta alisema makundi ni sehemu ya siasa na kwamba mtu hawezi kuwa mwanasiasa halafu akakosa makundi.

“Mimi ni jasiri najiamini, tabia ya kuwa mnafiki katika masuala ya kisiasa sina, najua watu watatumia fedha nyingi, lakini umma unanikubali, jimboni kwangu vilisimamishwa vyama vya upinzani saba, lakini nimeweza kushinda kwa kishindo,” alisema na kuongeza kuwa:

“Katika kinyang'anyiro hicho hakuna chama cha upinzani kilichopata kura kwa asilimia zaidi ya mbili, najua vyama hivi kama Jahazi Asilia, DP, hawa wamepewa fedha na watu kuja kusumbua tu, lakini nashukuru wananchi wamenikubali na wamenipachika jina la 'chuma cha pua' yaani ukikiingiza kwenye moto kinakuwa imara zaidi.”

Aidha akizungumzia kuhusu uhuru wa wabunge bungeni, Sitta alisema wanahaki kuzungumza mambo ya wananchi, lakini suala wanalotakiwa kufuata ni katiba inavyosema.

Alisema endapo atapata ridhaa hiyo kwa mara nyingine hatamzuia mbunge wa chama chochote kuongea kwa sababu ni haki yao.

Kuhusu madai yaliyozagaa kuwa alikuwa haitendei haki CCM, Sitta alisema hizo ni tuhuma za adui zake ambao wapo wa aina mbili.

“Wapo wanaopata shida katika mambo ya uwazi yanapotolewa, mtu kuwa ndani ya CCM haimaanishi usijulikane mambo unayoyafanya lazima kipato chako kijulikane,” alisema.

Alisema CCM hakisimamii maovu na kwamba watasalimika pindi wanapoyabaini maovu na kuyachukuia hatua.

“Sidhani kama wananchi wanataka Bunge liwe la kuficha uovu, lakini wale wenye nia nzuri sidhani kama wanakasirika uwazi unapokuwepo,” alisema.

Akielezea kuhusu upinzani ulivyochukua majimbo mengi ya udiwani na ubunge, Sitta alisema itabidi CCM wakae watafakari na kutathmini.

Alisema kwa upande wa Urais imeonyesha wananchi bado wanaimani na Rais Jakaya Kikwete.

"Ngazi za kata na majimbo wananchi wameona wabadilishe viongozi na sehemu zinazoshtua zilizochukuliwa na upinzani ni zile za mijini ambazo ni Dar es Salaam, Mwanza, Iringa, Arusha na Mbeya,"alisema na kuongeza,

"CCM tunatakiwa kutafakari hili kwani wananchi wanawaheshimu viongozi walio wazi, wanaofahamu kiongozi huyu utajiri wake ni wa aina gani," alisema.

Aidha, alisema endapo atapata nafasi ya kuwa Spika wa Bunge la Kumi, atatetea sana sheria zitakazolenga uwazi zaidi ili wasitukanwe wote.

"Nina uzoefu wa kutosha na Bunge na nitakabiliana nalo kuliko kama baadhi ya watu wanavyojaribu kutaka kuniondoa katika hili,"alisema.

Sitta alisema kuwa Spika haimaanishi mpinzani asipewe haki, kila Mbunge hutakiwa kupewa haki yake bila kuangalia ni wa chama tawala au upinzani.

"Ninauzoefu wa Mbunge la Tisa, wapo watu wanaojua kujenga hoja, wanaelimu na wanasifa nzuri hii ni kwa pande zote, naweza kusema wanauwiano mzuri," alisema.

Awali, kabla ya kuchukua fomu, Sitta akizungumza na wanaandishi wa habari kuhusu uchaguzi wa mwaka huu, utaratibu ulioanzishwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi wa kuingiza taarifa kwenye kumpyuta ndio mshindi atangawe ulikuwa na urasimu.

"Huu ulikuwa ni urasimu, sisi tulikuwa na mawakala wetu ambao walitusaidia kuhesabu kura, sasa unakuta mtu anajijua ni mshindi lakini kutokana na urasimu huu anajikuta anakaa siku tatu ndipo atangazwe," alisema na kuongeza,

" Inawezekana hivi unawafundisha maofisa Utumishi wa Wilaya siku tatu mafunzo ya Excel ili aelewe na aweze kujumlisha matokeo kwa wakati," alihoji.

Naye, Makinda akizungumza na gazeti hili jana jioni alisema kuwa, anatarajia kurudisha fomu kesho na kwamba hoja sio kuichukua bali ni kuisoma na kuijaza kisha kuirudisha.

Aidha, alipoulizwa kama anauwezo wa kupambana na kumng'oa Sitta, Makinda alisema huwa hapendi kutumia neno kumng'oa na kwamba hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu bado hajarudisha fomu.

"Mwandishi kesho uje pale CCM Makao Makuu, mara baada ya kurudisha fomu ndipo uniulize maswali kwa sasa siwezi kuongea chochote," alisema.

Awali akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhiwa fomu ya Sitta, Chizi alisema hadi kufikia jana alasiri jumla ya watu wawili walikuwa wamechukua fomu.

Alimtaja mwingine aliyechukua fomu kuwa ni Salim Kungulilo ambaye ni Mwalimu na mtafiti wa sayansi na kwamba taarifa alizonazo ni kwamba Mbunge wa zamani wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge anatarajia kufika hapo baadaye kuchukua fomu.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Chenge alisema kuwa, hana mpango wa kugombea nafasi hiyo kwa mwaka huu labada mwaka 2015.

Aidha alisema kwa wakati akizungumza na mwandishi alikuwa jimboni kwa wapiga kura wake.

CHANZO: NIPASHE

No comments: