MGOMBEA wa uspika wa Bunge, Andrew Chenge, amemshambulia Spika anayemaliza muda wake, Samuel Sitta kuwa ni mtu hatari aliyemwaga sumu kubwa kwa wananchi dhidi ya viongozi wa serikali katika miaka mitano ya uongozi wake bungeni.
Sumu hiyo kwa mujibu wa mgombea huyo, imesababisha majeraha kwa taifa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi na pia imezaa majeruhi wengi akiwamo yeye binafsi.
“Mimi kama walivyo wengine wengi, ni miongoni mwa majeruhi wa uongozi wa namna hiyo (wa Sitta). Kama Bunge, hatuna budi kukabiliana nalo kwa nguvu kubwa,” alisema Chenge katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari aliouitisha Dar es Salaam jana.
Moja ya majeraha hayo kwa CCM kwa mujibu wa Chenge, ni matokeo ya uchaguzi uliomalizika wiki iliyopita.
“Matokeo yake (ya uongozi wa Sitta), ni wananchi ambao siku zote wamekuwa na imani kubwa na viongozi wao, wamelishwa sumu mbaya na hilo limechochea chuki, hasira na kutoaminiana miongoni mwa jamii.”
Chenge, aliyejiita mwarobaini wa majeraha hayo na kuweka wazi kuwa Sitta ‘anatakiwa kuondolewa kwa nguvu kubwa’, mbali na kumshutumu Spika huyo ambaye ameshatangaza nia ya kutetea kiti hicho, pia alielezea uzoefu wake katika uongozi aliosema unatosha kumpa sifa ya kuwa Spika.
“Nimechukua fomu ya kugombea kiti cha uspika nikiamini kwamba, ninao uwezo wa kutibu majeraha makubwa yaliyoliumiza Bunge na Taifa, wananchi na chama changu (CCM),” alisema.
Kwa mujibu wa Chenge, majeraha hayo yamesababishwa na “kiongozi aliye tayari kujitafutia na kujitwalia umaarufu au ushujaa wake binafsi kwa njia ya kuwahujumu, kuwaumiza na kuwachafua wengine kwa kutengeneza tuhuma na kashfa za kila aina.
“Bunge limekuwa na changamoto kubwa katika miaka mitano iliyopita. Viongozi ambao wajibu wetu wa msingi ni kuonesha njia, badala yake tumekuwa vinara wa uzushi, uongo, fitina na majungu,” alisema Chenge.
Tiba ya uongozi wa aina hiyo kwa mujibu wa mgombea huyo, ni kuchagua kiongozi bora wa Bunge na njia bora ni kupata kiongozi mbadala mwenye uwezo na nia njema.
Sitta alipotafutwa kwa njia ya simu, ilipokelewa na mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mlinzi wake na kusema kuwa anafahamu kinachotafutwa ni kuhusu Chenge lakini Sitta hatajiingiza katika malumbano hayo.
“Mzee hatuwezi kumruhusu ajibu, tumemzuia asijibu, hawezi kuingia katika malumbano,” alisema mlinzi huyo na kuendelea, “watu wanaona, subirini wakati wa kampeni.”
Chenge alisema Sitta aliendesha mijadala kwa kuwafanya wabunge wa chama tawala na wa Kambi ya Upinzani upande mmoja na serikali upande mwingine.
“Mimi nikiwa spika siwezi kuruhusu kitu kama hicho.” Alifafanua kwamba demokrasia ya kibunge, inataka wabunge wa chama tawala na serikali wawe upande mmoja na kambi ya upinzani upande mwingine na kusisitiza kuwa, pamoja na kuwa majeruhi wa uongozi wa Sitta, hatalipiza kisasi katika uongozi wake.
Kwa mujibu wa Chenge, wabunge wa chama tawala wanaruhusiwa kuzungumza lolote kuhusu utendaji wa serikali katika kamati yao ya chama na wakiingia bungeni, wanapaswa kuikosoa Serikali kwa lengo la kuboresha utendaji wake kwa staha.
Kuhusu kambi ya upinzani, alisema yenyewe ndiyo inayopaswa kuikosoa serikali ikibidi iiondoe madarakani kwa kuwa hilo ndilo lengo lao kuu.
Mbali na kuwageuza wabunge wa chama tawala na kambi ya upinzani dhidi ya serikali, Chenge alisema pia Sitta hakutekeleza wajibu wake kama mwamuzi (referee) kwa kuzingatia sheria na kanuni, badala yake aligeuka shabiki na aligeuza Bunge sehemu ya kutoa maoni yake binafsi.
Alipoulizwa kama ametumwa kugombea uspika, Chenge alihoji mbona alipokwenda kugombea ubunge Bariadi Mashariki, hakuna mtu aliyehoji nani aliyemtuma?
Alisisitiza kuwa uzoefu wake kama Mwanasheria Mkuu wakati wa uongozi wa awamu ya pili na ya tatu ndio kilichomsukuma.
Waandishi walipotaka awataje majeruhi wengine na kuhoji kama ni mkakati wake na wa majeruhi hao wa kuingia katika siasa za kusaka uongozi kwa mwaka 2015, Chenge alisema kila mtu aliyekuwa akifuatilia mambo ya Bunge, anafahamu majeraha na majeruhi wengine. Hata hivyo hakutaka kufafanua kuhusu kampeni za 2015.
Alipoulizwa kama aliwahi kufanya jitihada zozote kunusuru hali hiyo akiwa kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya chama hicho, alisema chama chake kimefanya kazi kubwa katika hilo, ikiwemo kuundwa kwa Kamati ya Mzee Mwinyi.
No comments:
Post a Comment