RAIS Jakaya Kikwete amemuapisha Mizengo Pinda (62) kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.
Rais Kikwete juzi alimteua Pinda kuwa Waziri Mkuu, Bunge likamthibitisha kwa kupiga kura.
Hii ni mara pili kwa Pinda kuapishwa kushika madaraka hayo, kwa mara ya kwanza aliapishwa Februari mwaka 2008 kuchukua nafasi ya Edward Lowassa.
Pinda ameapa kuwa mwaminifu kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wake wote.
Mbunge huyo wa Katavi, pia ameapa kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwanasiasa huyo ameapa kuwa, atamshauri kwa hekima Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na hatatoa siri za Baraza la Mawaziri.
Katika kiapo hicho katika viwanja vya Ikulu Ndogo ya Chamwino, Dodoma, Pinda ameapa kuutetea na kuulinda umoja wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Viongozi wote wakuu wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar wamehudhuria sherehe za kumuapisha Pinda akiwemo Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Wengine waliohudhuria ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Seif Ali Idd.
Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, mawaziri wakuu wastaafu, John Malecela, Frederick Sumaye, na Edward Lowassa pia walikuwepo wakati Pinda anaapishwa.
Viongozi wengine wakuu waliohudhuria sherehe hizo ni Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, Naibu Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, na Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange.
Makatibu wakuu wa Wizara, wakuu wa mikoa, watendaj wakuu wa taasisi za umma na binafsi, mabalozi wa nchi mbalimbali, na viongozi wa vyama vya siasa pia walikuwepo kwenye sherehe hizo.
No comments:
Post a Comment