RAIS Jakaya Kikwete amelizindua Bunge la 10 na kutaja vipaumbele vyake 13 atakavyovizingatia katika miaka mitano ijayo ya Serikali yake, huku akiahidi kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za serikali.
Sambamba na hilo, ameeleza utayari wake kulivalia njuga na kuondoa nyufa za mgawanyiko wa kidini uliotokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.
Rais Kikwete alisema “nitaboresha zaidi ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa pamoja na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma…naahidi tutajipanga zaidi kusukuma kwa nguvu nidhamu na uwajibikaji katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.”
Alitaja kipaumbele kingine ni kuhakikisha kunakuwa na umoja, amani na usalama na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaendelea kudumu na kuimarika na kuahidi kero chache za Muungano zilizosalia ambazo hazijapatiwa ufumbuzi, kupatiwa ufumbuzi ulio muafaka kwa pande zote mbili.
Pia Serikali yake katika miaka mitano ijayo itaendeleza juhudi za kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa kuchukua hatua thabiti za kuharakisha mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
Katika kufanikisha hilo, alisema bajeti ya kilimo itaendelea kuongezwa na kufikia asilimia 10 na kuhimizwa kilimo cha umwagiliaji; kuongeza juhudi za ujenzi wa viwanda vipya na kurahisisha taratibu za utoaji wa leseni za biashara na upatikanaji wa malighafi na ardhi.
Serikali ijayo itawawezesha wananchi kiuchumi na kuboresha mipango ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wanaotaka kujiajiri, kuwatambua na kuwawezesha wajasiriamali wa kati, ili washiriki katika uwekezaji mkubwa wa ndani na nje ya nchi.
Rais Kikwete ameahidi kujenga na kuimarisha sekta binafsi na kutengeneza mazingira mazuri ya ushirikiano na sekta ya umma pamoja na kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati hivyo kutaboreshwa miundombinu ya reli, barabara, viwanja vya ndege na teknohama.
Alitaja kipaumbele kingine ni kuongeza jitihada za kuhakikisha taifa linanufaika na maliasili zake kwa kuhakikisha kunakuwa na sera na sheria za uvunaji na matumizi ya rasilimali hizo zinazonufaisha taifa sawia ambapo sasa Shirika la Taifa la Madini (Stamico) kwa niaba ya serikali litaimarishwa ili kushiriki katika umiliki wa migodi mikubwa na ya kati na hivyo taifa kunufaika.
Vingine ni kukuza ajira hasa kwa vijana na kuongeza kasi ya kujenga majengo ya wafanyabiashara wadogo na kuongeza kuwa yatajengwa Dar es Salaam na Mwanza na baadaye katika miji mingine mikuu ya mikoa.
Alisema wataboresha elimu ya msingi na sekondari ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto na mkazo utakuwa katika masomo ya sayansi; kuboresha huduma za kijamii na uchumi kwa kuongeza fedha katika mifuko ya fedha, kuimarisha benki ya rasilimali na kuanzisha benki ya kilimo.
“Tutaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa bajeti ya elimu ili tufundishe na kuajiri walimu wengi zaidi, tupate vitabu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia na kuongeza matumizi ya teknohama katika utoaji wa mafunzo na kujenga uwezo wa wanafunzi na walimu kiteknolojia ili kwenda sambamba na karne ya utandawazi,” alifafanua Rais Kikwete mbele ya wabunge.
“Tutaendelea kuimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yetu na majirani na mataifa mengine duniani na mashirika ya kimataifa na tutaendelea kutafuta marafiki wapya na kuboresha diplomasia ya uchumi na tutaongeza juhudi za kuhifadhi mazingira.”
Kwa upande wa afya, alisema huduma zitasogezwa zaidi kwa wananchi, kujenga uwezo wa ndani wa kutibu maradhi ili kupunguza watu wanaopelekwa nje kwa matibabu na bajeti ya afya itaendelea kuongezwa.
Kipaumbele cha mwisho ni kulinda mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kukamilisha ahadi za mwaka 2005 ambazo hazijatekelezwa.
Rais Kikwete alisema mambo matatu aliyoyaahidi mwaka 2005 ataendelea kuyapa kipaumbele ambayo ni kuhakikisha nchi na watu wake wanakuwa wamoja na yenye utulivu na amani; kukuza uchumi na kupunguza umasikini na kuhakikisha demokrasia inastawi na serikali inaendeshwa kwa misingi ya utawala bora na kuendeleza mapambano ya rushwa na maovu katika jamii.
Akizungumzia kuhusu nyufa ya mgawanyiko wa kidini alisema; “hatuna budi kuchukua hatua za haraka kuziziba vinginevyo hatuna nchi, hatuna taifa, tutafanana na nchi nyingine tu. Nawahakikishia utayari wangu wa kushirikiana na wanasiasa wenzangu, viongozi wa dini na wa kijamii kulitafutia ufumbuzi suala hili.”
“Si vyema na si busara kuliacha likatoa mizizi na kulimong’onyoa taifa letu, nawaomba wenzangu mkubali tushirikiane tuinusuru nchi yetu,” alieleza Rais Kikwete. Kuhusu magereza, alisema, “tutalivalia njuga na kulipatia ufumbuzi muafaka tatizo kubwa la mlundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani.”
Kwa upande wa kilimo na mifugo, alisema mavuno kwa mazao ya kilimo ya chakula na biashara yameendelea kuongezeka na mwaka huu, kipo chakula cha kutosha nchini.
Akizungumzia elimu, alisema Serikali yake itaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa bajeti ya elimu ili kufundisha na kuajiri walimu wengi zaidi, huku akisisitiza kwamba katika miaka mitano ijayo, “tutaendelea na upanuzi wa fursa za kupata elimu, lakini mkazo mkubwa tutauelekeza katika kuboresha elimu inayotolewa.”
Kuhusu mapato, alisema ukusanyaji mapato ya serikali umeongezeka kutoka wastani wa Sh bilioni 177.1 mwaka 2005 kwa mwezi hadi kufikia Sh bilioni 453 kwa mwezi hivi sasa, huku akiahidi kuongezwa maradufu jitihada za kukusanya mapato na kuimarisha matumizi ya serikali.
“Tutaboresha mfumo wa ukusanyaji mapato ya serikali na kupanua wigo wa walipa kodi. Tutakuwa wakali kuhakikisha mianya inayovujisha mapato inazibwa na pesa za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” alifafanua Rais Kikwete na kuongeza: “Uzembe, wizi na ubadhirifu havitavumiliwa.
Tutaendelea kuzipa uzito unaostahili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na kuchukua hatua zipasazo kasoro zinapobainika. CAG akamate bila kusubiri Bunge.”
Akitoa hotuba ya kuahirisha Bunge, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alimpongeza Rais Kikwete kwa kutoa maelekezo mahsusi ya kutekeleza katika miaka mitano ijayo, akisema msingi wa maelekezo hayo ni Dira ya Maendeleo 2025, Mkukuta na Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Malengo ya Maendeleo ya Milenia.
Alisema kama Waziri Mkuu anamuahidi Rais kuwa yeye pamoja na Baraza la Mawaziri litakaloundwa, kuwa karibu na wabunge, huku akieleza kuwa hotuba ya Rais inayo mambo mazuri kama vile kipaumbele cha umoja wa Watanzania akisema ni jambo lisilopaswa kugeuzwa la kawaida, kwani ni kubwa.
Mengine ni kupambana na umasikini, akisema bado ni changamoto kubwa na ameeleza jinsi Serikali yake itakavyokabiliana nayo katika kilimo, uvuvi na mifugo. “Ulipofafanua nikasema upele umepata mkunaji,” alisema Waziri Mkuu.
Jingine ni suala la ushiriki wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, akisema ni lazima serikali kwa muda wote itoe maelezo ya kina ya hatua kwa hatua ambayo yanafikiwa kwa wananchi ili azma hiyo itimie kwa kunufaisha Watanzania wote.
Bunge limeahirishwa hadi Februari 8, mwakani. Aidha, wabunge mbalimbali waliipongeza hotuba ya Rais Kikwete, huku Mbunge wa Kilosa, Mustafa Mkulo akisema ameweza kuelezea mafanikio yake na ahadi ya Tume ya Mipango kuanza kazi Januari kutaifanya Tanzania kuwa na dira ya kuleta maendeleo.
Naye Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF), amesema hotuba hiyo imekidhi kutokana na kuelezea kuwa demokrasia itaimarika na kutekeleza suala la amani kwa kudhibiti ujambazi na mauaji ya albino.
Mbunge wa Isimani, William Lukuvi (CCM), alisema imetoa mwelekeo mzuri hasa aliposisitiza serikali iondoe urasimu na watu wachape kazi ambapo alifafanua “hapo tutaondoa kero za msingi na kupata mafanikio.”
No comments:
Post a Comment