Monday, November 22, 2010

‘Panga’ lawasubiri manaibu waziri

IWAPO Rais Jakaya Kikwete atatekeleza matakwa ya wananchi ya kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, kuna uwezekano kuwa nafasi zitakazopunguzwa ni za manaibu waziri.

Baraza lililomaliza muda wake lina manaibu waziri 21 huku Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Wizara ya Fedha zikiwa na manaibu waziri wawili kila moja huku wizara zingine 17 kati ya 26 zilizoundwa katika Baraza hilo zikiwa na naibu waziri mmoja.

Wizara saba hazina manaibu waziri, lakini wachambuzi wa mambo ya siasa wamedokeza kuwa kuna uwezekano Rais Kikwete akaendelea kupunguza idadi ya manaibu waziri ili kutoa fursa ya mawaziri kufanya kazi kwa karibu na makatibu wakuu wa wizara.

Kwa mfumo wa wizara, kila wizara ina Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu.

Wizara pia zina wakurugenzi wa idara mbalimbali ambao wanamsaidia Katibu Mkuu hali
iliyoelezwa kuwa inatoa fursa kwa waziri kumudu majukumu ya kazi hata pasipo kuwepo na naibu wake.

Waziri anayeteuliwa na Rais kazi yake kubwa ni kusimamia sera za Serikali iliyoko madarakani na kuhakikisha kuwa Ilani ya chama kilichoko madarakani itatekelezwa na wizara husika.

Makatibu wakuu ndio watendaji ambao mara zote wamekuwa wanasimamia maelekezo na sera za Serikali na kuhakikisha kuwa malengo yaliwekwa na wizara husika kwa kila mwaka yanafikiwa.

Ni kutokana na hali hiyo wachambuzi wanaamini kuwa Rais Kikwete atapunguza manaibu waziri katika baadhi ya wizara. Wizara ambazo kwa sasa hazina manaibu waziri ni Ardhi, Katiba na Sheria, Utawala Bora, Muungano, Utumishi, Sera na Uratibu na Bunge pamoja na Mazingira.

Wizara inayoweza kutokuwa na manaibu waziri ni Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambayo waziri wake mara nyingi shughuli zake zinafanywa na Mkuu wa Majeshi anayeshirikiana na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa.

Wizara ya Jinsia, Wanawake na Watoto nayo inaweza isipewe naibu waziri pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi iliyoundwa na Rais Kikwete ili kuhamasisha ufugaji bora na uboreshaji wa sekta ya uvuvi.

Wizara nyingine ambayo inaweza isiwe na naibu waziri ni Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wizara ya Kazi, Maendeleo ya

Vijana na Ajira. Wachambuzi hao pia wamebainisha kuwa ni ngumu Rais Kikwete kupunguza Baraza la Mawaziri hasa kutokana na vipaumbele vya Serikali yake ambavyo viko 13.

Baraza la sasa lina mawaziri 26 ukiacha Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na Rais mwenyewe hivyo kulifanya Baraza hilo kuwa na watu 30.

Lakini Rais pia anaweza kuunganisha baadhi ya wizara ili kuleta ufanisi zaidi na kuepusha migongano ya kikazi, hali ambayo imefanya baadhi ya mambo yasishughulikiwe kutokana na wizara hizo kutupiana mpira.

Iwapo ataunda Baraza kwa kuzingatia vipaumbele hivyo ina maana kuwa kutakuwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi ili kukuza amani na usalama.

Pia kutakuwa na Wizara ya Muungano ambayo iko katika Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo kama atahitaji kupunguza Baraza, atalazimika kuchanganya na Mazingira ambayo nayo iko katika Ofisi ya Makamu wa Rais ili zishikwe na waziri mmoja badala ya mawaziri wawili kama ilivyokuwa hapo awali.

Katika hotuba yake ya kulizindua Bunge, Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, Rais Kikwete alikiri kuwa zimebaki kero ndogo ndogo za Muungano, hali inayoonesha kuwa kwa kuwa suala hilo pia husimamiwa na kamati maalumu waziri wake lazima aongezewe majukumu ambayo wachambuzi hao wanahisi ni ya mazingira.

Lakini wengine wanasema kama Waziri huyo ataongezewa jukumu la mazingira, atalazimika kuongeza juhudi za kuhifadhi mazingira hasa wakati huu ambapo makali ya athari za mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuiumiza nchi.

Katika Ofisi ya Rais, kunatarajiwa kuwepo na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambavyo ni moja vya vipaumbele vyake.

Ili kutekeleza jukumu la kuimarisha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi jirani na mataifa mengine lazima, Rais ataunda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wizara hiyo ya Afrika Mashariki inaweza isiwe na naibu waziri huku Wizara ya Mambo ya Nje lazima itakuwa na naibu waziri ambaye atatoka sehemu moja ya Muungano kutokana na wizara hiyo kuwa ya Muungano.

Wamesema Wizara ya Maliasili na Utalii nayo lazima itakuwepo, lakini pia licha ya umuhimu wake wadadisi wanadokeza kuwa pia naweza kuwa na naibu waziri.

Lakini pia Rais anaweza kuunganisha Wizara ya sasa ya Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja na mambo ya umwagiliaji akaiondoa kwenye Wizara ya Maji ambayo inaweza kubaki peke yake.

Kwa vile kilimo kinachosisitiziwa kwa sasa ni cha mwagiliaji, kuna uwezekano wizara hiyo ikawa moja.

Lakini kutokana na vipaumbele vya Serikali, matazamio ya kupunguzwa Baraza hilo yatakuwa ni madogo na kama akifanya hivyo, Rais anaweza kuua wizara tatu na kuziacha zingine 23 zikiendelea kuwepo, lakini kwa kiasi kikubwa akipunguza idadi ya manaibu waziri.

Rais Kikwete anatarajiwa kutangaza Baraza lake la Mawaziri siku yoyote wiki hii.

No comments: