Thursday, November 4, 2010

Ucheleweshaji wa matokeo wasikitisha waangalizi EU

Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) wameuelezea Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita kuwa, ulifanyika kwa amani na mpangilio mzuri kwa asilimia 95.

Hata hivyo, waangalizi hao, wameeleza kuwa ucheleweshaji wa kutangaza matokeo ya uchaguzi kuwa ni jambo linalosikitisha kwa sababu linasababisha mashaka na shauku miongoni mwa wapiga kura na wagombea na kwamba pia wana mashaka na uwazi katika zoezi zima la kukokotoa matokeo ya uchaguzi.

Taarifa ya awali iliyotolewa na Kiongozi wa waangalizi hao, David Martin, jana, pia ilikosoa utaratibu wa kuzuia mgombea binafsi kuwa unakiuka kanuni za kimataifa kwa sababu sharti hilo linawanyima watu haki na fursa ya kusimama kugombea, hasa wale ambao wangependa kushiriki katika uchaguzi kama wagombea binafsi.

Alisema kuwa sharti la kumtarajia mtu kuwa mwanachama wa chama cha siasa na kuwa hanabudi apendekezwe na chama husika ili kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu linawawekea mipaka ridhaa ya wapiga kura na kwamba linaweza kuwalazimisha kumchagua mgombea ambaye hawakumtaka kutokana na mgombea waliyemtaka kutokuwepo katika orodha ya wagombea walioidhinishwa.

Martin, alisema Ujumbe Maalum wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) iliukadiria mchakato mzima wa uchaguzi huo kuwa ulikuwa mzuri na wa kuridhisha kwa asilimia 95 katika vituo vyote vya kupigia kura walivyotembelea upande wa Tanzania Bara na ubande wa Visiwani Zanzibar.

Alisema kwa ujumla, taratibu muhimu katika vituo vya kupigia kura zilitumiwa kwa ulinganifu katika kila kituo cha kupigia kura nchini kote, licha ya kuwepo dosari kadhaa kama vile upoteaji wa baadhi ya vifaa vya kupigia kura, ikiwa ni pamoja na karatasi za kupigia kura, fomu za wapiga kura na orodha za wapiga kura.

Aliongeza kusema kuwa, tathmini iliyofanywa na waangalizi hao kuhusu utendaji wa wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya chini, ilidhihirisha kwa ujumla utendaji wao una ufanisi, wenye mpangilio mzuri na kuwa upo tayari kwa muda wote.

“Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa ujumla iliendesha chaguzi kwa namna ya kitaalam zaidi na kwenda na wakati katika maandalizi yote ya uchaguzi,” alisema.Kwa upande wa Tanzania Bara, Martini, alisema Chama cha Mapinduzi (CCM) kilinufaishwa kwa kuwa chama tawala na kuonekana kuwa na msingi imara zaidi wa kifedha ambao ulikiwezesha kufanya kampeni zenye mwonekano mkubwa zaidi ikilinganishwa na vyama vingine.

Alisema chama hicho tawala pia kilinufaishwa na muundo wa utawala wa vyombo vya serikali.

Alisema kuwa, ujumbe wa EU EOM utaendelea kubaki nchini kufuatilia kwa karibu zoezi zima la kukokotoa matokeo ya uchaguzi, utangazaji wa matokeo na kufuatilia matokeo yote yatakayojitokeza baada ya uchaguzi na kwamba watatoa taarifa ya kina ya mwisho baada ya miezi miwili au mitatu baada ya mchakato mzima wa uchaguzi kukamilika.


CHANZO: NIPASHE

No comments: