TAASISI ya Utafiti wa Masuala ya Kijamii na Kiuchumi (ESRF), imepongeza ushindi wa Rais Jakaya Kikwete na kuishauri serikali yake kutilia mkazo suala zima la utawala bora kwa kuwa ni eneo ambalo linalalamikiwa zaidi na wananchi.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Bohela Lunogelo alisema wananchi kwa sasa wanahitaji kuona mabadiliko katika mfumo wa utawala bora zaidi, ili kuona kama maisha bora kwa kila Mtanzania yanapatikana.
Akitoa mfano, Dk Lunogelo alisema wananchi wanahitaji kupatiwa huduma bora zinazowajali wateja wanaohitaji huduma hizo, ili kuondoa malalamiko.
Alisema kama hakuna utawala bora ina maana mteja hawezi kuridhika na huduma inayotolewa na hivyo kuishia kulalamika.
Kwa mujibu wa Dk. Lunogelo, kwa sasa utafiti unaonesha kuwa wananchi wanahitaji zaidi majengo ya shule, zahanati na miundombinu kwa kuwa serikali ilifanya vizuri maeneo hayo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Alisema kwa sasa wanahitaji serikali ijayo iwekeze zaidi nguvu zake kwenye utawala bora na usimamizi wa maliasili za serikali.
"Kama hakuna utawala bora, ni dhahiri kuwa kutakuwepo na ucheleweshwaji wa maendeleo kwa wananchi.
Mmahospitalini wananchi wanahitaji huduma bora na dawa ziwepo, na pia kwenye mashule walimu wawepo wa kutosha na walipwe mishahara kwa wakati na wapatiwe makazi bora, haya yanaangukia kwenye utawala bora," alisema
Alisema wananchi pia wanahitaji kufahamu mapato yatokanayo na rasilimali za serikali kama vile madini na mazao ya ardhi na misitu ili watambue yanasaidia vipi kuboresha huduma za kijamii nchini kwa kuwa ni maeneo ambayo yanazusha malalamiko kwa wananchi.
"Wananchi kwa sasa wamebadilika, siyo kama ilivyokuwa zamani, wakiona kuna dalili za rushwa au usimamizi mbovu wa rasimali za serikali wanahoji kwa nini hali hiyo inatokea, utawala bora usiishe maofisini tu bali ufanyike kwa vitendo na utiliwe mkazo,"alisema.
Dk Lunogelo serikali ijyao pia inapaswa kuhakikisha inaboresha mfumo mzima wa kuchagua vijana wanaojiunga na kozi mbalimbali vyuo vikuu kwa kuwa malalamiko yamekuwapo kuwa
ukosefu wa utawala bora umechangia kwa wao kukosa nafasi.
No comments:
Post a Comment