CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesisitiza bado hakiyatambui matokeo yaliyotangazwa na tume ya Taifa ya uchaguzi na kumpa ushindi Rais Jakaya Kikwete ,lakini imefafanua kuwa hatua hiyo haina maana kwamba wabunge wake na madiwani hawatatekeleza wajibu wao.
Chama hicho kimesema kuwa kutokana na mfumo uliopo sasa kuendelea kupendelea chama tawala, tayari kimeanza mchakato wa kudai tume huru ya uchaguzi kupitia Bunge na mabadiliko ya katiba ili uwanja wa kisiasa uweze kutoa fursa sawa kwa wote.
Mwenyekiti wa Chama hicho Bwana Freeman Mbowe amewaambia waandishi wa habari Mjini Dodoma kuwa amesema kuwa ni muhimu sasa kuundwa kwa tume maalumu kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa uchaguzi uliopita ili hatimaye ibainishe kasoro zilizopo na kutoa majibu sahihi kwa nini wananchi wengi hawakujitokeza kupiga kura.
Kwa upande wake aliyekuwa mgombea wa kiti cha Urais kupitia CHADEMA Dokta Willbroad Slaa amesema yupo tayari kutaja majina ya maofisa wa usalama wa Taifa waliohusika katika kuvuruga zoezi la uchaguzi iwapo majina hayo yatahitajika kama ushahidi mahakamani maana kitendo kilichofanywa ni kosa la jinai.
No comments:
Post a Comment