-Asambaratisha vigogo CCM
-CCM wapigwa butwaa, watafakari kilichowasibu
WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiendelea kutangaza matokeo ya urais, wimbi la mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk, Willibrod Slaa, limeteka nchi na sasa anasema anasubiri matokeo ya jumla aweze kutoa tamko zito.
Matokeo ya kushitusha yamekuwa yakitangazwa nchi nzima ambako baadhi ya majimbo ambayo yamekuwa, mengine kwa miaka mingi, mikononi mwa Chama cha Mapinduzi (CCM), yakiangukia mikononi mwa CHADEMA.
Katika mahojiano maalumu na Raia Mwema jana Jumanne, Dk. Slaa alisema pamoja na kuwapo kwa mapungufu mengi kabla na baada ya upigaji kura, anasubiri matokeo na taarifa kutoka kwa watu wake kabla ya kutoa tamko.
“Kimsingi tunasubiri taarifa za kutosha kuweza kutoa tamko na pia tunaendeela kufuatilia matokeo yanayotolewa na NEC na tunalinganisha na yale ya mawakala wetu nchi nzima tuweze kujua, maana kuna maeneo tunasikia wanatangaza matokeo wakati mchakato katika eneo husika haujakamikika,” alisema.
Alitoa mfano wa Jimbo la Kiteto ambako alisema kulikuwa na mvua iliyosababisha kuchelewa kwa masanduku kufika eneo la kujumlishia matokeo, na kwamba tayari NEC ilikuwa imetangaza matokeo Dar es Salaam kabla hata ya masanduku kufika kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo.
“Pia kuna ucheleweshaji wa ajabu wa kutoa matokeo katika maeneo ambayo tunaungwa mkono na ni maeneo yale ambayo hayakuwa na matatizo ya usafiri yakiwamo yale ya miji mikuu,” alisema Dk. Slaa.
Mbali ya ucheleweshwaji wa matokeo, Dk. Slaa alizungumzia pia kufutwa kwa matokeo katika baadhi ya majimbo na kata na akahoji haki za wapiga kura katika maeneo hayo zitalindwa vipi.
“Kuna majimbo matatu na kata zaidi ya 10 zimefutiwa matokeo, sasa wapiga kura hao watapataje haki zao, lakini pia kulikuwa na matumizi makubwa ya dola kabla ya uchaguzi na siku ya uchaguzi, mfano kule Mbeya, mara baada ya mkutano wangu wa mwisho, Polisi walipiga mabomu hadi usiku wa kuamkia siku ya kupiga kura na hiyo imewatisha wapiga kura wengi,” alisema.
Tayari NEC imekwisha kutangaza matokeo katika baadhi ya majimbo, ambako mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amekuwa akiongoza huku katika baadhi ya maeneo akigawana kura ama kuzidiwa na mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Dk. Slaa.
Hata hivyo, kumekuwa na wimbi kubwa la kukataliwa CCM na kwa maana hiyo mgombea wa CCM Rais Jakaya Kikwete katika maeneo mengi nyeti, yakiwamo maeneo wanamoishi viongozi na watendaji wa serikali na vyombo vya dola, katika miji mikubwa ikiwamo Dar es Salam, Mwanza, Arusha na Mbeya.
Katika maeneo hayo yakiwamo yale ya Jimbo la Kawe na Kinondoni, Rais Kikwete amejikuta akigawana ama kuzidiwa kura na Dk. Slaa, katika maeneo nyeti yakiwamo Oysterbay, Kijitonyama na Mbezi, hali inayoashiria kuwa siku zijazo kwa CCM na wagombea wake ni mbaya.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya chama tawala, chama hicho kimepoteza kura nyingi katika maeneo nyeti ya kisiasa ya Kanda ya Ziwa, Dar es Salaam, Arusha, Iringa, Mbeya na Kilimanjaro, maeneo ambayo tokea kuanza kwa siasa za vyama vingi yamekuwa ngome kuu ya chama tawala.
Maeneo mengine ambayo CCM kimepata kura chache ni Kigoma na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Rukwa, hali ambayo imeelezwa kuwa ni ishara ya CCM kuanza kukataliwa na wananchi wengi wakiwamo wanachama wake.
Wachunguzi wanasema kukataliwa huku kwa CCM ni ajenda ya mageuzi inayosukumwa na ma,kundi ya vijana waliochoshwa na utamaduni wa ufisadi unaowanyima wengi, wengi wao wanaotoka vyuoni, fursa za kukabili vyema hatima ya maisha yao ya sasa na baadaye.
Wachambuzi hao wanasema kwamba inawezekana kwamba Rais Kikwete na CCM wameshindwa kusoma alama za nyakati kwamba wapiga kura walikuwa wanakerwa na kuendelea kuwakumbatia mafisadi na kwamba inawezekana pia kwamba ahadi lukuki mzinazomwaga hazikupeleka ujumbe kwamba zinatekelezeka.
Mgombea aliyefuatia baada ya Kikwete na Slaa, ni Profesa Lipumba, ambaye amepata kura nyingi katika Visiwani, akigawana kura na Kikwete Unguja na mikoa ya Tanga, Lindi na Mtwara.
Chanzo: www.raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment