Friday, November 19, 2010

Kikwete ataka mawaziri wabanwe

RAIS Jakaya Kikwete amewataka wabunge wawabane mawaziri katika Serikali yake lakini wawasahihishe wakiteleza.

Rais Kikwete pia amewaeleza wabunge kuwa, wasiwe wachoyo wa kuwasifu mawaziri wakifanya vizuri.

Kikwete ameyasema hayo mjini Dodoma wakati akihutubia Bunge la 10 na kulifungua rasmi.

Amewaeleza wabunge kuwa hivi karibuni atateua mawaziri makini, waadilifu na wachapakazi hodari.

Kwa mujibu wa Kikwete, atakaowateua wataiongoza nchi yetu kwa umahiri mkubwa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mipango ya Serikali.

Kikwete amesema, atateua watu watakaoondoa urasimu katika katika Serikali, watakuwa karibu na wananchi, na watashirikiana vizuri na wabunge bila kujali vyama vya siasa wanapotoka.

Rais Kikwete amewaomba wabunge wampe ushirikiano Waziri Mkuu kama walivyofanya katika Awamu ya Kwanza ya Serikali yake.

Kwa mujibu wa Kikwete, Serikali atakayoiunda itakuwa na vipaumbele 13 ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye umoja na usalama, na kwamba, Muungano uendelee kudumu na kuimarika.

Ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kuendeleza juhudi za kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa kuharakisha mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda.

Wabunge wameelezwa kuwa, kipaumbele kingine cha serikali itakayoundwa kitakuwa ni kuongeza jitihada za kuwawezesha kiuchumi wananchi wa makundi yote ili washiriki na kunufaika na uchumi unaokua.

Alisema, Serikali itaendelea kujenga na kuimarisha sekta binafsi nchini na kutengeneza mazingira mazuri ya ushirikiano na sekta ya umma sanjari na kuimarisha uwezo wa serikali kupanga mipango ya maendeleo na kusimamia utekelezaji wake bila kuingilia shughuli za sekta binafsi.

Rais Kikwete amelieleza Bunge kuwa, Serikali itatumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu na kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafiri kwa nchi za Afrika Mashariki na kati.

Bunge limeelezwa kuwa, Serikali pia itaongeza jitihada za kuhakikisha kuwa taifa letu linanufaika zaidi na maliasili zake zilizo juu na chini ya ardhi hivyo itahakikisha kwamba, kunakuwa na sera za uvunaji na matumizi ya rasilimali hizo.

Alisema, Serikali itaboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa pamoja na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma.

Kikwete alisema, miaka mitano iliyopita ilikuwa migumu sana kwa kazi ya kujenga uchumi na kupunguza umasikini nchini kwa kuwa uchumi ulipata misukosuko mikubwa ukiwemo ukame uliokausha mazao mashambani.

“Hivi sasa uchumi wetu umekuwa tulivu tena, kasi ya ukuaji ni nzuri, mfumuko wa bei umeshuka sana kutoka wastani wa asilimia 12.1 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 4.2 hivi sasa” alisema.

No comments: