Monday, November 15, 2010

Makinda: Sitabadilika, nitakufa mwadilifu

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda ambaye ushindi wake umekuwa gumzo na hasa baada ya kuenguliwa kwa mtangulizi wake, Samuel Sitta aliyekuwa amejitokeza kutetea kiti hicho, amesema kamwe watu wasitegemee kama atabadilika na kuacha uadilifu wake.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali za awamu mbalimbali, amesema yeye ni mwadilifu wa kuzaliwa na hakuazima wala kukopa kwa mtu, hivyo ana uhakika atakufa na uadilifu wake.

Spika huyo aliyechaguliwa wiki iliyopita, alitoa maelezo hayo wakati alipowahutubia wabunge na wakazi wa mji wa Dodoma katika sherehe za kupongezwa zilizoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dodoma pamoja na wabunge wanawake.

“Uadilifu siazimi wala sikopi kwa mtu, nimezaliwa hivyo na nitakufa nao, baba yangu alikuwa mwadilifu na mwanasiasa na akafa vivyo hivyo,” alisema Makinda (61).

Alisema katika kupata nafasi hiyo, hajatumia hata senti moja wala kutoa kitu, bali ameupata
kutokana na kupigiwa kampeni na watu ambao hawajui, ila kwa utashi wao wenyewe kutokana na kuwa na imani naye.

“Hakuna aliyeniweka katika kiti hiki na nitafanya kazi bila upendeleo na naamini nitasaidiwa na Mungu na hata siku ya kupitishwa asubuhi nilikwenda kanisani kuomba Mungu anipe malaika wa kunisaidia,” alisema.

Tangu amepitishwa na kuchaguliwa kwa kishindo na wabunge, Makinda amekuwa akivumishiwa maneno mengi, ikiwemo kuwa alisaidiwa kupata uteuzi na kushinda kiti hicho na kundi hasimu na aliyekuwa Spika Sitta, jambo ambalo mwanamama huyo amelikanusha tangu aliposhinda kiti hicho.

Spika huyo wa kwanza mwanamke nchini tangu kupata Uhuru, aliweka wazi kuwa nafasi hiyo anaiweza na haendi kujifunza, bali kwenda kufanya vizuri zaidi na

kuzingatia ushauri wa wananchi katika kuliendesha Bunge ambalo litakuwa moja bila kujali itikadi ya vyama vya siasa. Aliahidi

kulifanya Bunge hilo kuwa moja na imara na wawakilishi wawe wa kweli kuwawakilisha wananchi na si mtu binafsi, huku akisema Bunge la sasa lipo wazi hivyo si rahisi mtu kulibadilisha zaidi ya kuwashauri wabunge kufahamu sheria na kanuni.

Alirejea kauli yake kuwa kama Sitta angepitishwa na Kamati Kuu ya CCM kutetea kiti chake, angeondoa jina lake na kuongeza “ingewezekanaje mimi na Sitta wote tuondoke kwenye Bunge, isingekuwa sahihi, kweli tuache watu kutoka nje?

Ndiyo maana mimi pia nilichukua fomu…maneno ya mitaani nayachukulia ni ya watu waliofilisika, mimi sina tatizo na Siita, ni kaka yangu tumefanya kazi pamoja.”

Naye Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake, Mizengo Pinda alisema Makinda ana uwezo na anashaurika vizuri na kushauri wenzake vizuri, hivyo ana imani atawasaidia Watanzania.

Katika sherehe hizo, wanawake walimpa Makinda zawadi ya picha yenye mchoro wa mama aliyebeba mzigo wa kuni na mtoto mgongoni pamoja na seti ya mkufu wa dhahabu yenye lulu.

No comments: