Wednesday, November 10, 2010

Uongozi wa juu Zanzibar wakamilika

SAFU ya uongozi wa juu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar imekamilika baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, kuteua makamu wake wawili, Maalim Seif Shariff Hamad na Balozi Seif Ali Iddi.

Kwa mujibu wa marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kutakuwa na makamu wa rais wawili; wa kwanza akitoka chama kilichoshika nafasi ya pili na wa pili akitoka chama kilichotoa rais.

“Kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu 39 (1),(2) na (3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, leo amemteua Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais,” ilieleza taarifa ya Ikulu Zanzibar jana na kuongeza:

“Wakati huo huo kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu 39(1),(2) na (6) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein amemteua Balozi Seif Ali Iddi kuwa Makamu wa Pili wa Rais.”

Taarifa hiyo ya Ikulu ilisema uteuzi huo ulianza jana na wawili hao walitarajiwa kuapishwa jana hiyo hiyo.

Kwa mujibu wa kifungu cha 39 (1), (2) na (3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ndani ya siku saba baada ya kushika madaraka, Rais atateua Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais.

Kwa mujibu wa Ibara ya 3 ya kifungu hicho, Makamu wa Kwanza wa Rais atatakiwa awe na sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na chama kilichoshika nafasi ya pili katika matokeo ya uchaguzi wa rais.

Ibara hiyo pia inaeleza kuwa iwapo chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa rais kimepata chini ya asilimia tano ya kura zote za uchaguzi huo; au endapo rais atakuwa hana mpinzani katika uchaguzi, basi nafasi ya makamu wa kwanza itakwenda kwa chama chochote cha upinzani kilichoshika nafasi ya pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.

Ibara ya nne inaeleza kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais hatakuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi; Ibara ya 5, inaeleza kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais atakuwa mshauri wa Rais katika kutekeleza kazi zake na atafanya zote atakazopangiwa na Rais.

Kwa mujibu wa Ibara ya 6 ya kifungu hicho cha 39, Makamu wa Pili wa Rais atateuliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka chama anachotoka Rais; na
Ibara ya 7, inaeleza kuwa Makamu wa Pili wa Rais atakuwa ndiye Mshauri Mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake na pia atakuwa kiongozi wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Baraza la Wawakilishi.

Balozi Iddi ni mwanasiasa mwenye kufuata siasa za mrengo wa wastani na amekuwa na uzoefu wa muda mrefu katika siasa, aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali; Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar na kabla ya uchaguzi, alikuwa Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Hamad ambaye ni maarufu kama Maalim Seif, aliwahi kuwa Waziri wa Elimu, Waziri Kiongozi wa SMZ na kwa sasa ni Katibu Mkuu wa CUF.

Alikuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huu na alishika nafasi ya
pili nyuma ya Dk. Shein.

Kulingana na Katiba ya sasa ya Zanzibar, CUF iliyoshika nafasi ya pili katika uchaguzi huo ilipaswa kupendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, wakati CCM ikitakiwa kutaja jina la Makamu wa Pili wa Rais.

Chini ya makubaliano hayo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, nafasi za mawaziri zitagawanywa sawa, miongoni mwa vyama hivyo, vikuu vya kisiasa Zanzibar.

Wakati huo huo, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho amechaguliwa tena kwa kura nyingi kuendelea na wadhifa huo ikiwa ni Baraza la Kwanza la Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kificho alipita kwa kura 45 kutoka kwa wawakilishi 78 waliopiga kura, dhidi ya mshindani wake Abbasi Juma Mhunzi wa CUF ambaye alipata kura 32.

Katika uchaguzi huo, kura moja iliharibika ambapo mshindi alitangazwa kwa kupata kura nyingi.

Hii ni mara ya nne kwa Kificho ambaye ni kada maarufu wa CCM, kushika wadhifa huo na alikuwa mwanachama pekee kupitia chama hicho aliyekuwa akiwania nafasi hiyo.

Baada ya kula kiapo cha utii, Spika Kificho aliwaapisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwamo wanane walioteuliwa na Rais Dk. Ali Mohammed Shein juzi.

No comments: