MGOMBEA wa uspika wa Bunge la Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anne Makinda (61), amesema, akichaguliwa, Bunge litakuwa imara na lenye kasi kuliko lililopita.
Makinda amewaeleza waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa, ana uzoefu wa kuliongoza Bunge na ameiva kushika madaraka hayo.
Ametoa kauli hizo baada ya kushinda katika kura za wabunge wa CCM waliopendekezwa kugombea nafasi hiyo.
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM jana ilimteua Makinda, Anna Abdallah na Kate Kamba kuwania kuteuliwa kugombea uspika kwa tiketi ya CCM.
Mbunge huyo wa Njombe Kusini ameshinda kwa kupata kura 211, Kate kamba alipata kura 15, na Anna Abdallah alipata kura 14.
Makinda atachuana na mgombea wa Chadema anayewania uspika wa Bunge, Mabere Marando.
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amesema, chama hicho kinaamini kuwa, mgombea wake atashinda.
Makinda amesema, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Bunge la Tanzania hadi kuwa Naibu Spika.
Amesema, wakati akiwa Naibu Spika wa Bunge alipata uzoefu wa kuliongoza Bunge kwa kutembelea mabunge mbalimbali duniani na kuona uendeshaji wake.
Makinda amesema, kambi ya upinzani isitegemee kuwa kutakuwa na mteremko katika utoaji wa maamuzi, yatatolewa kwa kufuata taratibu na kanuni za Bunge.
Amesema, wabunge wote wanapaswa kazifahamu kanuni za Bunge ili wasije kulalamika unapotolewa uamuzi kwa kufuata kanuni hizo.
Makinda amesema, wabunge hao wakizifahamu kanuni hizo mapema wataweza kuwa makini wanapochangia mijadala na pia kama kuna kanuni ambayo haifai kwa wakati huu basi wawaze kuibadili mapema.
No comments:
Post a Comment