RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema Serikali yake ya Awamu ya Saba ambayo ni ya Umoja wa Kitaifa, imejipanga kusimamia na kuhakikisha kuwa suala la amani, maadili, demokrasia na utawala bora linakuwa ajenda kuu ya kitaifa.
Pia amesema katika kuhakikisha kuwa matatizo ya wafanyakazi visiwani hapa yanapatiwa ufumbuzi hasa kimaslahi, Serikali hiyo inatarajia kuunda wizara mpya ya Utumishi wa Umma ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia masuala yote ya wafanyakazi.
Aidha, ametoa shukrani kwa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa maridhiano waliyofikia ambayo yameleta mabadiliko ya kisiasa visiwani na kuvipatia sifa duniani kote.
Akizindua Baraza la Wawakilishi jana mjini hapa, Dk. Shein alisema wakati umefika kwa Serikali hiyo mpya itakayojenga historia ya Zanzibar, kuonesha mfano kwa kusimamia maadili na utawala bora hasa katika kupiga vita rushwa, lakini pia kuwahudumia wananchi kwa misingi ya Katiba na Sheria.
“Maadili ndio itakuwa ajenda yetu ya kitaifa, tunapaswa kama viongozi kuwajibika kwa wananchi waliotuchagua, nawahakikishia kuwa tutapambana na rushwa kwa hali yoyote ile na nitashughulikia kuanzishwa kwa Sheria ya Rushwa, na kwa kuanzia, nitaziba mianya yote ya upoteaji ovyo wa mapato ya Serikali,” alisema Dk. Shein na kushangiliwa.
Alisema tangu mchakato wa uchaguzi uanze na kumalizika, Wazanzibari wameonesha hali ya amani, utulivu na kupendana na hivyo kutoa fursa kwa Serikali hii kutumia nafasi hiyo kama chachu ya kuwaletea maendeleo.
“Jamii imepata matumaini mapya, hali ambayo imetoa fursa sasa ya kuijenga nchi kiuchumi kwa pamoja,” alieleza.
Alisema atahakikisha anawaongoza wananchi wake kwa kufuata misingi ya Katiba ya Zanzibar, bila kujali itikadi zao na kipaumbele kikiwa ni kuwajengea maisha na uchumi bora ambao kwa mujibu wa dira ya Serikali hiyo, hadi mwaka 2015 uchumi utapanda na kufikia asilimia 10.
Aliwataka wananchi kudumisha jitihada za maridhiano kwa kusimamia umoja na mshikamano ili kuiwezesha Serikali itimize ahadi ilizotoa na kuwaletea maendeleo wanayotarajia ambapo pia alisisitiza juu ya umuhimu wa wananchi kushiriki maendeleo ya nchi yao.
Aliwaahidi wananchi hao kuwa Serikali yake itatekeleza kwa vitendo ahadi zote ilizotoa wakati wa kampeni ambazo ni kuimarisha sekta ya kilimo, viwanda, uvuvi na ufugaji, miundombinu kuanzia barabara, bandari na viwanja vya ndege, huduma za kijamii kama vile maji, elimu, afya na umeme na ajira, lengo likiwa ni kuwakwamua wananchi na umasikini.
Aliahidi kwa kushirikiana na Rais Jakaya Kikwete kusimamia na kutatua kero za Muungano ambapo Serikali yake itaanza kwa kuboresha Kamati ya Pamoja ya kutatua kero hizo.
Akitoa shukrani, Mwakilishi wa Kambi ya Upinzani, Abubakar Hamis Bakari, alisisitiza juu ya ushirikiano baina ya Wazanzibari bila kujali itikadi za vyama vyao, na kuahidi kuwa hotuba hiyo ya Rais itatumika kama moja ya zana za ujenzi wa Zanzibar mpya.
“Kuna mwanasiasa mmoja nchini Marekani alisema nyumba iliyogawanyika si imara, tudumishe umoja wetu,” alisema Bakari.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Maalim Seif na Jaji Mkuu Hamid Mahamoud waliokuwa katika msafara wa Rais.
Wageni waalikwa wengine ni Mama Mwanamwema Shein, wake wawili wa Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho, huku mke wake wa tatu akishindwa kufika kutokana na dharura pamoja na mabalozi wadogo waliopo nchini.
No comments:
Post a Comment