Tuesday, November 2, 2010

Shein Rais Zanzibar, Seif ampongeza

HAYAWI hayawi sasa yamekuwa, Zanzibar imempata Rais mpya, Dk. Ali Mohamed Shein, baada ya kumalizika kwa uchaguzi uliofanyika kwa utulivu na amani kubwa.

Mpinzani wake mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, wa Chama Cha Wananchi (CUF) ameyakubali matokeo, na amempongeza Dk. Sein.

Matokeo yaliyompa ushindi Dk. Shein yalitangazwa jana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar huku Maalim Seif, ambaye kwa mujibu wa katiba mpya ya Zanzibar, anakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, akisema ushindi ni wa Wazanzibari wote.

Baada ya kutangazwa kwa Dk. Shein, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, ambaye pia alipata asilimia 50.1 ya kura zote, Maalim Seif aliyekuwa mgombea urais kupitia CUF, alimsifu Rais mteule kwa “uwezo, uzoefu na mahaba yake kwa nchi yake.”

Maalim Seif ambaye alipata asilimia 49.1 ya kura zote alisema: “nina uhakika Dk. Shein ana uwezo, uzoefu na mahaba kwa nchi yake na kwa sababu hiyo, nina uhakika atatoa uongozi wenye busara wa kuunganisha nchi yetu.”

Hata hivyo, Maalim Seif, alimuomba Dk. Shein azungumze na wanachama na mashabiki wa CCM, ili kusiwepo na kubezana na kuonya kuwa hali hiyo ikitokea, inaweza kuchafua hali ya hewa.

Akikubali kuchukua wajibu huo mkubwa wa kitaifa, Dk. Shein alikubali ushauri wa Maalim Seif na kufafanua kuwa, uongozi wake unahitaji Zanzibar yenye heri.

Aliungana na Maalim Seif kuipongeza Zec kwa kuendesha uchaguzi murua na kuwapongeza Wazanzibari wote walioshiriki katika upigaji kura.

Dk. Shein anakuwa rais wa saba Zanzibar baada ya Rais wa Kwanza, Abeid Amaan Karume aliyefuatiwa na Abdul Wakili, Aboud Jumbe, Ali Hassan Mwinyi, Dk. Salmin Amour ambaye alimkabidhi kijiti Rais anayemaliza muda wake, Dk. Amani Abeid Karume.

Awali kabla ya matokeo hayo, matokeo ya Unguja yalionesha Dk. Shein akiongoza katika majimbo 18 na Maalim Seif akiongoza katika majimbo manne.

No comments: