Wednesday, November 24, 2010
TANZIA
Mtandao wa Mashirika yapatayo 50 yanayotetea Usawa wa Kijinsia, Haki za Binadamu, Maendeleo na Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi (FemAct), tunaomboleza kuondokewa na Mpendwa wetu, dada Mary Mwingira, mpiganaji wa muda mrefu wa haki za wanawake na haki za kijamii, aliyefariki siku ya jumapili usiku, tarehe 21 Novemba 2010, baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu. Tunapenda kumuenzi kwa mchango wake katika ukuaji na uimarishwaji wa mashirika ya kijamii hapa Tanzania. Mary Mwingira aliongoza wanawake na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na masuala ya kijinsia hapa Tanzania kushiriki katika Mkutano wa Ulimwengu wa muongo wa Wanawake uliofanyika Nairobi, Kenya, mwaka 1985, wakiunga mkono mashirika mbalimbali kutoka ngazi za kijamii hadi kitaifa na kupata fursa ya wazo mbadala wakati wa Kongamano la mashirika yasiyo ya kiserikali huko Nairobi, pamoja na kubadilishana mawazo na kuunga mkono ujumbe wa kiserikali. Mchakato huu ulipelekea kuanzishwa kwa TANGO, jumuiya mama ya mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania, ambayo Mary Mwingira aliiongoza kwa miaka mingi kama Mkurugenzi Mtendaji. Mary pia alikuwa mwanachama mwanzilishi wa taasisi mbalimbali za wanawake na haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na Taaluma Women and Christian Professionals of Tanzani, na pia alishiriki katika Kongamano la kijamii la Ulimwengu, Nairobi.
Kati ya 1992/1993, Mary Mwingira pamoja na vikundi vya viongozi wengine wa vikundi vya wanawake na jinsia walishiriki katika mchakato wa pamoja katika kutafakari na kupanga mikakati ambayo iliongozwa na waanzilishi wa Mtandao wa jinsia Tanzania katika kuandaa Kongamano la Wanawake la Ulimwengu lililofanyika Beijing, China, mwaka 1995. Kwa kutumia mbinu shirikishi za uraghibishi na uchambuzi wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi, viongozi hawa wanawake wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali walifanya kwa pamoja uchambuzi wa kina wa nafasi ya wanawake hapa Tanzania, mfumo dume na mfumo wa utandawazi kibeberu iliyoendelea kuwakandamiza na kuwanyonya wanawake wakati wa mfululizo wa warsha hizo tatu, na hatimae kupanga kwa pamoja mikakati iliyokuwa inahitajika kwa ajili ya kuendeleza haki za wanawake, usawa wa kijinsia na mabadiliko ya kijamii. Mawazo haya baadaye yaliwasilishwa na viongozi wa TGNP kwa niaba ya Kikundi cha Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Tanzania katika Mkutano wa Maandalizi wa nchi za Kanda ya Afrika ya Mashariki Uliofanyika Uganda mwaka 1993, na kuchapishwa kama Hali Halisi ya Kijinsia Tanzania( Gender Profile of Tanzania), mwaka huo.
Mapema mwaka 1993, viongozi hawa hawa wa mashirika ya wanaharakati wa masuala ya wanawake na jinsia walidai wawezeshaji wa warsha waunde shirika jipya la kudumu na kufanya uchambuzi wa ukombozi wa wanawake kimapindu kwa kutumia mbinu shirikishi. Ni kutokana na mchakato huu TGNP iliweza kuzaliwa, ambapo iliandikishwa rasmi mwishoni mwa mwaka 1993, kwa mchango mkubwa wa Mary Mwingira, kwa upande wa ushauri na kutambulisha wafadhili. Muda mfupi baadaye, wengi kati ya viongozi hao hao wa Jumuiya zisizokuwa za kiserikali za wanawake na haki za kijinsia walianzisha FemAct, kwa ajili ya kuimarisha vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi na haki za binadamu katika ukuaji wa nguzu za pamoja. TANGO ni mwanzilishi wa FemAct na Mary Mwingira alibakia kuwa mshiriki imara katika mapambano mengi yaliyofanywa nchini Tanzania katika kukuza haki za wanawake na za kijamii kwa wote waliokandamizwa, walionyonywa na waliowekwa pembezoni.
FemAct inatuma salamu zake za rambiambi kwa familia ya Mary Mwingira, ndugu, jamaa na marafiki wote. Katika kipindi hiki cha maombolezo, tumkumbuke kwa uwezo wake wa kusimama imara katika mapambano ya kutetea haki, demokrasia na usawa wa kijamii katika ngazi zote.
Tunaiombea roho ya marehemu dada yetu, ilale mahali pema peponi, Amen.
Imetolewa na
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kwa niaba ya FemAct.
Na kusaininwa na
……………………………
Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment