Tuesday, November 16, 2010

Dk Shein ateua Baraza la Mawaziri la Kitaifa

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameunda Baraza jipya la Mawaziri lenye sura ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa kuwapa nafasi nyeti
baadhi ya vigogo wa juu wa Chama cha Wananchi (CUF).

Baraza hilo lenye wizara 16, pia limejumuisha baadhi ya manaibu waziri wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete iliyomaliza muda wake na mawaziri wa serikali iliyopita wa Serikali ya Dk.

Amani Abeid Karume, huku aliyekuwa Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha akiachwa.

Baadhi ya vigogo hao wa CUF walioteuliwa katika baraza hilo, yupo aliyekuwa mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Juma Duni Haji
ambaye amepewa Wizara ya Afya.

Wengine wa CUF walioteuliwa katika baraza hilo ni pamoja na mwanamama Mwakilishi machachari wa CUF, Fatma Abdulhabib Fereji, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais.

Wengine kutoka CUF na nafasi zao katika mabano ni Aboubakar Khamis Bakary, ambaye
alikuwa Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi (Waziri wa Katiba na Sheria), Hamad Masoud Hamad aliyekuwa Waziri kivuli wa Miundombinu (Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano).

Pia yumo Abdilahi Jihad Hassan ambaye ni mwakilishi mpya wa Magogoni (Waziri waAhmed Mazrui aliyeteuliwa dakika za mwisho na Rais Karume baada ya maridhiano (Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko).

Dk Shein pia amemteua Said Ali Mbarouk aliyekuwa Waziri Kivuli wa Fedha (Waziri wa Mifugo na Uvuvi), Haji Faki Shaali aliyekuwa Waziri kivuli Uratibu wa Shughuli za Baraza
la Wawakilishi (Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu).

Wengine kutoka CUF ambao wameteuliwa kuwa manaibu waziri ni Zahra Ali Hamad (Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali), Bihindi Hamad Khamis ( Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo) na Haji Mwadini Makame (Naibu Waziri wa Ardhi, Makazi,
Maji na Nishati).

Mawaziri kutoka CCM ni pamoja na Dk. Mwinyihaji Makame (Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Ikulu), Omar Yussuf Mzee, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Serikali ya Muungano (Waziri Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo).

Wengine ni Haji Omar Kheri ambaye alikuwa Waziri anayeshughulikia Uratibu wa Shughuli za Baraza la Wawakilishi (Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mohammed Aboud Mohammed aliyekuwa Naibu Waziri wa Afrika Mashariki katika Serikali ya Muungano (Waziri Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais).

Wengine ni Ramadhan Abdulla Shaaban ambaye alikuwa Waziri wa Katiba na Utawala Bora (Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali), Zainab Omar Mohammed aliyekuwa Waziri asiye na Wizara Maalumu anayeshughulikia Pemba (Waziri wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya
Wanawake na Watoto).

Mawaziri wengine kutoka CCM ni aliyekuwa Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna (Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati), Mansoor Yussuf Himid aliyekuwa Waziri wa
Nishati, Ujenzi na Maji (Waziri wa Kilimo na Maliasili).

Pia yupo Haroun Ali Suleiman aliyekuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali (Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika), Suleiman Othman Nyanga, aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa (Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiyekuwa na Wizara
Maalumu) na Machano Othman Said, aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano ( Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri Asiekuwa na Wizara Maalum).

Katika unaibu waziri, Dk Shein amemteua Issa Haji Ussi (Naibu Waziri ya Miundombinu na Mawasiliano), mmoja wa wawakilishi wapya walioteuliwa na Rais, Dk. Sira Ubwa Mamboya ( Waziri wa Afya) na Thuwaiba Edington Kissasi (Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko).

Mbali na Nahodha, wengine walioachwa ni Samia Suluhu Hassan (Utalii, Biashara na Uwekezaji), Burhan Saadat Haji (Kilimo na Mifugo) na Asha Abdallah Juma (Kazi na
Maendeleo ya Wanawake na Watoto).

Wengine walioachwa ni Sultan Mohamed Mugheiry (Afya na Ustawi wa Jamii Taffana Kassim Mzee (Naibu Waziri wa Nishati, Aridhi na Maji) Shawana Buheit Hassan (Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii ).

Pia yumo Khamis Jabir Makame (Naibu Waziri Elimu na Vyuo vya Ufundi), Khatib Suleiman
(Naibu Waziri wa Kilimo na Mifugo) na Mahmoud Thabit Kombo (Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo).

Mawaziri wapya wataapishwa rasmi leo jioni katika viwanja vya Ikulu, Zanzibar.

No comments: