Monday, November 29, 2010

Sitta: Tanzania haiuzwi

MAWAZIRI wateule jana waliapishwa kuanza kutekeleza majukumu waliyopewa serikalini.

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta akisema wamekabidhiwa madaraka hayo kwa umakini ili asijetokea mtu akauza nchi.

Akizungumza muda mfupi baada ya kumaliza kupiga picha ya pamoja na Rais Jakaya Kikwete mara baada ya mawaziri hao na naibu mawaziri kula kiapo chao, Sitta alisema kazi waliyopewa inahitaji ujuzi wa kila namna.

“Kubwa la kuzingatia ni uzalendo, hii kazi (ya Uwaziri wa Ushirikiano Afrika Mashariki), humpi mtu tu, anaweza kutuuza,” alisema Sitta wakati akifafanua changamoto zinazomkabili katika wadhifa huo ambapo awali alianza kwa kumshukuru Rais Kikwete kwa kumteua kushika nafasi hiyo.

Alitamba kuwa utendaji wa kasi na viwango, sasa umehamia serikalini na kushangaa watu wanaoona kuwa atashindwa kupiga vita ubadhirifu kutokana na nafasi yake kama Waziri.

“Wakati ule nilikuwa nje, sasa nimeingia ndani ndio nitajua hali halisi ilivyo na kusaidia. Kwanza tutahakikisha sheria mpya ya maadili ya viongozi inapitishwa haraka.

“Unajua wananchi wanapata shida katika imani yao kwa Serikali hasa wanapomuona mtu aliyepata madaraka, ghafla ana pauni huko Uingereza na nyumba Ufaransa, tutapigia kelele hilo,” alisema Sitta ambaye alikuwa Waziri wa kwanza kuapa.

Alisisitiza nia ya kutetea kuwasilishwa bungeni haraka kwa muswada wa sheria mpya ya maadili ya viongozi ambayo inalenga kutenganisha biashara na siasa, ni ili kuepuka viongozi ambao wanatumia nafasi zao kujitajirisha wenyewe.

“Huwezi kutajirika katika siasa, kwa mfano mimi natakiwa Arusha Jumatatu na nitakuwa ofisini kuanzia asubuhi mpaka usiku, hiyo biashara utafanya saa ngapi halafu tunaambiwa wenzetu ni wachakarikaji, hakuna kuchakarika hapo.

“Ushahidi wa kwanza wa mwanasiasa mla rushwa ni kutajirika ghafla, labda kama aliingia madarakani akiwa na utajiri wake,” alisema Sitta na kujitolea mfano kuwa aliingia serikalini mwaka 1974 akitokea Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kama ofisa na katika hali hiyo asingeweza kujenga nyumba nje ya nchi.

Kuhusu umuhimu wa wizara hiyo kwa sasa, Sitta alisema Tanzania inakwenda kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na katika hilo maslahi ya Watanzania yanatakiwa kulindwa.

Alisema pia kuna changamoto ya kuwaondolea Watanzania hofu ya kuwa baada ya Shirikisho, watapata shida ikiwemo ya kukosa nguvu za kiuchumi na kuhusu mamlaka ya viongozi wao kama Rais.

“Tutaangalia mikataba na kuhakikisha tunaingia katika Shirikisho kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania hasa katika ardhi na ajira yanalindwa,” alisema Sitta na kutamba uwezo wake katika sheria na uzoefu serikalini wa karibu miaka 36 umemfanya kuwa mtu mwenye kuweza kazi hiyo.

Alisema, alipoachia aliyekuwa Waziri katika Wizara hiyo, Dk. Diodorus Kamala ndipo atakapoanzia yeye na kusifu uteuzi wa Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Abdallah Juma Abdallah kuwa ni mtu mzuri atakayesaidiana naye kazi.

Alikiri kuwa Tanzania iko nyuma ikilinganishwa na baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo na kuongeza kuwa atajitahidi kuomba muda katika mambo kama ardhi na ajira ili nchi isigeuke kama “shamba la bibi”. Alisema pia ataomba kuongezewa bajeti katika jukumu la kutoa elimu kwa Watanzania ili EAC ifahamike na kuondoa hofu.

No comments: