Wednesday, November 10, 2010

Shibuda aitahadharisha CCM kuhusu Uspika

AKIONEKANA kuguswa na mambo yanavyokwenda ndani ya CCM kuhusu upatikanaji wa mgombea uspika wa Bunge la Muungano, Mbunge mteule wa Maswa, kupitia Chadema John Shibuda amekihadharisha chama hicho tawala.

Amewataka wana CCM kufanya uamuzi wa busara juu ya kumpitisha mgombea uspika, vinginevyo watakisambaratisha chama hicho.

Alisema hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya kufika kwenye viwanja vya Bunge kujisajili, ikiwa ni mojawapo ya ratiba za wabunge wote wateule.

Shibuda alisema kuna kila sababu ya wana CCM kuwa makini katika kumpitisha mgombea uspika vinginevyo watakuwa wanatengeneza mwanya wa kukisambaratisha chama hicho.

Alisema inasikitisha kuona kuwa nafasi hiyo inagombewa na watu wasio na misingi ya uongozi na wanaonesha wazi uchu wa kiti hicho huku wakiwa na mawazo ya kulipiza kisasi.

Hata hivyo hakuwataja. Aidha, alimtaka Rais Jakaya Kikwete, kuhakikisha analisimamia vyema jambo hilo kwa umakini mkubwa na kudai kuwa iwapo chama tawala kitashindwa kuteua jina la mgombea makini ambaye anaweza kuongoza Bunge ni wazi kiti hicho kitachukuliwa na vyama vya upinzani.

Shibuda alisema kinachosumbua zaidi katika CCM ni makundi ambayo yamekuwa yakiibuka pindi inapoonekana kuwa yanatetea masilahi ya wengi.

Alisema Rais Kikwete anajitahidi kuongoza chama chake vizuri lakini kinachosumbua ni baadhi ya watendaji wake ambao hawataki kufanya mambo katika misingi ya ukweli na uwazi.

Alisema kutokana na tatizo hilo, ni wazi kuwa chama tawala kisipokuwa makini kijue wazi ushindi wa kishindo utaelekea katika vyama vya upinzani hususani Chadema na wasijisumbue kuendesha kampeni kwa lengo la kusaka urais.

Kwa sasa katika mji wa Dodoma wabunge wanaonekana kukaa vikundi huku wakijadili ni nani atateuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo nyeti ya uspika.

Pamoja na kampeni kuwa kali zaidi kati ya vigogo wawili ambao ni spika wa aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta na Mbunge mteule wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, bado Watanzania wengi wakiwamo wabunge wa vyama mbalimbali wanasubiri kuona hatimaye
moshi mweupe utamfukia nani.

Hadi jana wabunge mbalimbali waliochaguliwa katika uchaguzi mwaka huu walikuwa wakiendelea kujisajili, huku Kamati Kuu ya CCM, leo ikitarajiwa kutangaza mgombea wake wa uspika.

No comments: