Monday, November 15, 2010

UWT wamtabiria Pinda

WAKATI kesho Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kumteua Waziri Mkuu, Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), umeanza kumtabiria Waziri Mkuu aliyemaliza
wake, Mizengo Pinda, kuwa atateuliwa tena kushika wadhifa huo.

Hata hivyo, Pinda amewaambia kuwa anaogopa, kwani Rais Kikwete anaweza kusema wanampangia, hivyo akafuta uteuzi wake, lakini kama atarejeshwa, ameahidi kushirikiana naye.

Wanawake hao walieleza hisia zao wakati wa sherehe za kumpongeza Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo, zilizofanyika jana mjini hapa.

Sherehe hizo ziliandaliwa na UWT Mkoa wa Dodoma pamoja na wabunge wanawake.
Mwanamke wa kwanza kutoa utabiri huo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dodoma, Fatma Tofiq wakati akitoa risala yawanawake hao, kwa kumtaja Pinda kama Waziri Mkuu mtarajiwa.

Alipompa nafasi ya mke wa Pinda, Tunu Pinda kuwasalimia na kuzungumza na wanawake waliofika katika sherehe hizo, wakati akitoa utangulizi alisema, “Waziri Mkuu mstaafu si ndiyo (akacheka)… Waziri Mkuu mtarajiwa…hapo sawaaaaa (watu wakacheka) na Mbunge wa
Katavi… tumeanza vizuri kuwa na Spika mwanamke na natarajia miaka ijayo, Waziri Mkuu pia atakuwa mwanamke.”

Naye Mwenyekiti wa UWT Taifa, Sophia Simba wakati akitoa utambulisho, alimtaja Pinda kama Waziri Mkuu mtarajiwa akiamini rais atamteua tena.

Hata hivyo, Pinda alipopewa nafasi kusalimia hadhara hiyo, alisema “nimeogopa mlivyosema mimi Waziri Mkuu Mtarajiwa kwa sababu Mzee Kikwete anaweza kusikia akasema mnanipangia, sitaki sasa…kama nitakuwa bounceback (kurejea tena) nitashirikiana
naye”.

Naye Makinda alipopewa nafasi kama mgeni rasmi kutoa hotuba yake, alianza kwa kusema
“Mheshimiwa bounceback” na ndipo watu wakacheka.

Rais Kikwete kesho anatarajiwa kupeleka bungeni jina la mteule wake wa nafasi ya Waziri Mkuu ambalo litapigiwa kura na wabunge ili kuidhinishwa kushika wadhifa huo, kama Katiba inavyoelekeza.

Pinda aliyeingia madarakani Februari 2008, baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa kwanza
aliyeanza na Rais Kikwete katika Awamu ya Nne, Edward Lowassa, anatajwa kupewa nafasi ya kuendelea na wadhifa huo katika kipindi hiki cha pili na cha mwisho kikatiba kwa Rais Kikwete.

Uadilifu wake na uwezo mkubwa wa kusimamia shughuli za serikali zikiwamo za Bunge; kubana na kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za serikali na kutojihusisha na makundi ndani ya chama chake, ni mojawapo ya sifa zinazompa nafasi kubwa Pinda kuendelea na
kiti hicho katika kipindi chake cha mwisho cha miaka mitano kama mbunge baada ya kutangaza kutowania tena nafasi hiyo mwaka 2015.

No comments: