Wednesday, December 1, 2010

Prof.Tibaijuka aanza kwa kasi: Mliopora maeneo jisalimisheni

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amewataka wananchi waliopora viwanja na maeneo ya wazi nchini na kujenga, wajisalimishe kwa mazungumzo, kwa sababu huenda wakaokoa hata matofali kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.

Profesa Tibaijuka alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati ya wizara hiyo na kueleza kuwa masuala ya ardhi yasipofanyiwa kazi, sekta nyingine zitazorota.

“Umefika wakati sasa, tunataka kubadilisha mwonekano wa miji ... na kwa wanaosema wanatumia jeuri ya pesa, tutawashughulikia, lakini baada ya kufanya utafiti wa kutosha, kwa sababu hatuwezi kukurupuka, hivyo waliopora viwanja tunawataka wajisalimishe,” alisema Profesa Tibaijuka ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Makazi (UN-Habitat).

Alisema, migogoro ya ardhi hawataimaliza bila wananchi kuwasaidia na kwa sasa, watarudisha askari wa ardhi ili kuhakikisha wanapunguza migogoro ikiwamo ya wanaojenga holela na katika maeneo ya wazi.

Tibaijuka alisema, kati ya hekta 900,000 ni asilimia mbili tu ya maeneo ndiyo yaliyopimwa, hivyo wizara yake itahakikisha inapimwa, ili miji iwe katika hali inayotakiwa kwa sababu kwa sasa hairidhishi.

Aidha, Profesa Tibaijuka alisema si maendeleo yote yanahitaji fedha, hivyo kwa muda huu waliopewa na Rais, kuna mambo ambayo watayafanyia kazi kwa haraka ikiwamo kuandika majina ya mitaa yote.

“Watu wengi hawatambui mitaa wanayoishi inaitwaje, kwa sababu wala haina majina na unakuta anashindwa kabisa kuelekeza, lakini tukiiandika tutawasaidia, hivyo tutafanya jambo hili kwa haraka maana haihitaji fedha,” alifafanua mbunge huyo wa Muleba Kusini.

Katika hatua nyingine, alisema kuna upungufu wa nyumba milioni tatu nchini, hivyo wanapaswa kujenga miji kwa kuboresha nyumba zilizopo na kuzijenga ambazo hazina viwango na kuziuza kwa wananchi.

“Wananchi wanatakiwa kutambua wanahitaji nyumba au ardhi, lakini watambue kama ni viwanja lazima waende nje ya mji, ila kama ni nyumba zipo ila zinahitaji maboresho na tutafanikiwa, kwa kuwa na benki za nyumba na mikopo ya nje, kwa sababu sekta binafsi pekee hazitaweza bila kuwa na fedha ... tuwaachie wahandisi wetu wajenge nyumba sisi tununue,” alisema.

Alisema, watafanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mazingira ili kuhakikisha miji inakuwa safi na salama; na kuboresha bonde la Mto Msimbazi, Dar es Salaam, ambalo limefanya hali ya hospitali ya Taifa Muhimbili kuwa mbaya.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Patrick Rutabanzibwa, alikiri baadhi ya wafanyakazi wake kushiriki kugawa maeneo ya wazi na kueleza kuwa tayari ameanza kuwachukulia hatua za kisheria, ikiwamo kufanya mabadiliko ya vitengo kwa nia ya kuboresha utendaji kazi.

“Uvamizi wa maeneo ni mtandao wa watu wa wizarani na manispaa nami nimejitolea kuwashughulikia na tayari kuna waliokuwa wamepora viwanja na nimewataka wavirudishe na wengine walipora na kuwauzia wafanyabiashara wakubwa,” alisema Rutabanzibwa.

Pia alisema wamesimamisha ujenzi wa eneo la wazi katika hoteli ya Palm Beach na kuahidi kufanya kazi bila kuhofia kashfa, kwani zipo tuhuma amevumishiwa na amezipeleka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kwa upande wao, mawaziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mary Nagu (Uwekezaji na Uwezeshaji) na William Lukuvi (Sera, Uratibu na Bunge), waliripoti rasmi katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuzungumza na wakuu wa idara, vitengo na taasisi chini ya Ofisi hiyo.

Mawaziri hao waliwataka watendaji kufanya kazi kwa ubunifu, ushirikiano, upendo, uwazi na bidii zaidi, ili kukidhi matarajio ya wananchi.

Nagu alisisitiza umuhimu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji bila ngojangoja ambayo ni chanzo cha kuwakatisha tamaa wawekezaji.

Alisema hakuna uchumi duniani uliofanya vizuri bila uwekezaji, iwe wa kutoka nje au ndani ya nchi husika. Alibainisha kuwa Watanzania ndio wanatakiwa kushika hatamu ya uchumi wao.

Lukuvi alisisitiza watendaji kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kuongeza ufanisi na hatimaye kufikia malengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taifa kwa jumla.

Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu aliwaambia watendaji wakuu wa wizara hiyo kuwa anawapa uhuru wa kufanya uamuzi wenye tija na ufanisi na atakayeshindwa atajiondoa mwenyewe.

Alizungumza na wakurugenzi wakuu wa idara za uchukuzi na wa taasisi mbalimbali akijitambulisha kwao rasmi na kuanza kazi.

Nundu aliwataka kufahamu dhima waliyonayo katika kuendeleza sekta ya uchukuzi ili katika kipindi cha miaka mitano ijayo, fursa zilizomo zitumike vyema pamoja na kuboresha huduma za usafiri.

Aliwataka kupeana ushauri ili wasonge mbele, kuwa wadilifu na waaminifu huku wakitoa huduma kwa dhati na kwa wakati muafaka.

“Hakikisheni mnawajibika kulingana na wakati, katika suala la uchukuzi hatupo peke yetu ulimwenguni, zingatieni matakwa ya wateja,” alisema Nundu na kuongeza:

“Fanyeni kazi kila mmoja kwa madaraka aliyonayo, toeni uamuzi wenye tija bila upendeleo na hata ubinafsi na hiyo iwe ahadi yenu kwetu,” alisema.

Alisema, anatarajia kuimarisha kampuni ya reli, kwa lengo la kuipa uwezo wa kutoa huduma bora kwa kusafirisha abiria na mizigo ya ndani na nchi jirani, na kuendelezwa kama mhimili wa mpango wa maendeleo wa eneo la ukanda wa kati.

No comments: