Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein amewaahidi Wazanzibari hatawaangusha na atafanya kila linalowezekana kufikia matarajio yao chini ya serikali ya umoja wa kitaifa atakayoiongoza.
Dk. alitoa ahadi hiyo jana muda mfupi baada ya kula kiapo cha kuwa Rais wa awamu ya saba ya Zanzibar, baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31.
Rais Dk. Shein aliapishwa katika uwanja wa Amaan Zanzibar majira ya saa 4:00 asubuhi na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud.
“Nitafanya kila uwezo wangu kuhakikisha natimiza matarajio ya wananchi, wakati wote wa uongozi wangu,” alisema Dk. Shein.
Alisema kwamba ataendeleza ari ya amani na utulivu iliyopatikna Zanzibar kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Rais mstaafu, Amani Abeid Karume, na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.
Alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa juhudi kubwa alizochukua kuhakikisha mpasuko wa kisiasa Zanzibar unamalizika.
Alieleza kuwa Rais Kikwete baada ya kuingia madarakani, aliwaahidi Watanzania kuwa atachukua juhudi za kumaliza mpasuko wa kisiasa ili kuona wananchi wa Zanzibar wanaishi kwa maelewano.
Dk. Shein aliwashukuru wafanyakazi wa vyombo vya habari vya Zanzibar na Tanzania Bara kuwa wamefanyakazi kubwa ya kufanikisha uchaguzi wa mwaka 2010 bila ya kupendelea upande wowote.
“Ni vizuri amani na utulivu uliopo hivi sasa isidharauriwe au kubezwa ushindi uliopatikana ni wetu sote,” alieleza Dk. Shein.
Aidha, aliwashukuru viongozi wa CCM Zanzibar na Tanzania Bara kutokana na mashirikiano makubwa waliyompa na kuweza kufikia malengo ya kuwa Rais wa Zanzibar.
Nao viongozi wa dini wakitoa nasaha zao waliomuombea kiongozi kwa Mwanyezi Mungu ampe uwezo na busara ya kuongoza wananchi wa Zanzibar na kumuwezesha kuchagua wasaidizi wazuri watakaofanikisha lengo la kuleta maendeleo.
Viongozi hao ni Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji Khamis; Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Augostine Shao na Mchungaji, Mathew Muhagama wa Kanisa Anglikana Zanzibar.
Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni Rais Kikwete; Waziri Mkuu Mizengo Pinda; Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi; Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour.
Wengine ni aliyekuwa Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha; Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye; Spika wa Baraza la Mawakilishi aliyemaliza muda wake, Pandu Ameir Kificho na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika hatua nyingine, Wazanzibari bila ya kujali itikadi zao za kisiasa jana walifurika uwanja wa Amaani Zanzibar kushuhudia tukio la kuapishwa kwa Dk. Shein.
Shughuli zilianza baada ya kuwasili uwanjani hapo, na baadaye aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, kupokea heshima kutoka kwa vikosi vya ulinzi na usalama na kupokea gwaride la kumuaga.
Karume alipewa heshima ya kupigiwa mizinga 21, huku wimbo wa Taifa wa Zanzibar ukiimbwa na bendera ya Rais wa Zanzibar ikishushwa taratibu kuashiria kumalizika muda wake wa uongozi kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Baadaye Rais Karume aliingia katika jukwaa dogo ndani ya uwanja huo jirani na Dk. Shein na ndipo aliposogea Jaji Mkuu wa Zanzibar Hamid Mahmoud na kufanya kazi muhimu iliyokuwa ikisubiriwa na wananchi.
Baada ya Rais Dk. Shein kula kiapo, mlinzi aliyekuwa akimlinda Rais Karume ghafla alihamia kwa Dk. Shein kuashiria kuwa sasa Rais Karume anaungana na marais wastaafu wa Zanzibar.
Baadaye Dk. Shein alipokea heshima kutoka kwa vikosi vya ulinzi na usalama na kupigiwa wimbo wa Taifa wa Zanzibar huku bendera ya Rais wa Zanzibar ikipandishwa. Dk. Shein alikagua gwaride kabla ya kutoa hotuba ya shukurani.
Hata hivyo, wananchi wengi wakiwemo wafuasi wa vyama vikuu vya CCM na CUF walilazimika kufuatilia matukio hayo wakiwa nje ya uwanja kutokana na uwanja kufurika.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment