Monday, November 29, 2010

Magufuli amkaanga bosi wa Tanroads

SIKU moja baada ya kuapishwa,Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli amemtaka Mkurugenzi wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Ephraim Mrema kusimamisha mara moja nafasi za kazi za mameneja wa mikoa alizozitangaza kwenye vyombo vya habari kuwa zipo wazi.

Magufuli amewataka mameneja wote ambao wamesimamishwa kazi, warudi kazini mara moja na kwamba tangazo hilo halina nguvu.

Kutokana na uamuzi huo, Dk. Magufuli amemtaka Mrema kutoa tangazo haraka kuanzia leo katika vyombo vya habari, kusitisha tangazo lake la awali la kuwasimamisha kazi mameneja wa Tanroads mikoani kwa kuwa hatua aliyoichukua inaonekana ni ya kulipizana visasi.

Dk. Magufuli alitoa maagizo hayo jana, Dar es Salaam katika mkutano wake na wakuu wa idara na vitengo mbalimbali vya wizara hiyo wakati akijitambulisha kwao.

Katika maagizo yake, Dk Magufuli alimtaka Mrema asifanye kazi kama mtu anayeondoka kesho, bali atekeleze majukumu yake kama atafanya kazi hiyo kwa miaka 100 ijayo.

“Tanroads jipangeni sawasawa, blaablaa ziishe, wewe Mkurugenzi uliona nafasi yako inatangazwa na wewe ukaamua kutangaza za mameneja wa mikoa ili kuchomeana na kila kitu kisimamishwe, kwanini ulitangaza kwamba waliopo hawachapi kazi?”

Alihoji Dk. Magufuli. Aliagiza mameneja wa mikoa waelezwe mara moja kuwa wamerudishwa kazini isipokuwa kwa nafasi ya Dodoma tu ambayo meneja wake hayupo. “

Nakuagiza Mrema, uandike katika vyombo vya habari kuwa umefuta tangazo hilo na mengine yatafuatia.”

Alimtaka Mkurugenzi huyo wa Tanroads, kufanya kazi kwa ushirikiano na kwamba kama Waziri na Naibu wake Dk. Harrison Mwakyembe watauliza jambo lolote, wajibiwe haraka, la sivyo itakuwa ni dharau.

Mkurugenzi huyo wa Tanroads inadaiwa kipindi chake cha kuongoza wakala huo kimemalizika kwa mujibu wa mkataba wake wa kazi, lakini ameendelea kukalia ofisi hiyo.

Dk. Magufuli alisema wao hawakufika katika wizara hiyo kwa ajili ya kutengua Torati, bali kuitekeleza na kwamba wanaweza kufanya kazi na yeyote na kusisitiza kuwa yaliyopita yaachwe na wafanye kazi kwa pamoja.

“Tushirikiane, tupendane, majungu yaishe, tuache rushwa kwa kuwa tutawategeshea hata fedha ya Polisi… na hivi ndio maana Rais ametuteua mimi na Naibu mwenye taaluma ya Sheria,” alisema.

Kuhusu rushwa, waziri huyo aliahidi kupanda lori lililozidisha uzito na kutoa rushwa na akasema akikamilisha kazi hiyo watakaohusika watamtambua. Aliwataka watendaji wa mizani kusimamia sheria, kukamata magari na kupiga faini na kuteremsha mizigo bila kujali mmiliki wa gari au mzigo.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Dk. Mwakyembe, alisema uteuzi wao hautakuwa na maana kama wataachia kirusi aliyeingia katika Wizara hiyo na kutia doa kuendelea.

Alisema mwanzoni wizara hiyo ilikuwa mfano wa kuigwa lakini anashangaa kuona ufanisi umepotea na sasa imekuwa sehemu ya kunyoosheana vidole bila kujua ni kirusi gani huyo aliyeingia.

Alisisitiza kuwa sasa wanahitaji kuongea lugha moja na kuimba wimbo mmoja na kuifanya wizara hiyo kuwa ya mfano na kuagiza taarifa za kukinzana zisipewe nafasi kwa kuwa hawaendeshi wizara kwa majungu na umbeya.

No comments: