Wednesday, November 30, 2011

Kikwete Asaini Muswada Waliougomea CHADEMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete hatimaye leo, Novemba 29, 2011, ametia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, muswada ambao Chama cha Demokrasia na Maendeleo kiliugomea bungeni.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema hatua hiyo ya kutia saini Muswada huo inakamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limepitisha Muswada huo uliowasilishwa na Serikali katika kikao kilichopita cha Bunge.

Aidha, kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua kubwa na muhimu katika safari ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka jana, 2010.

Hata hivyo Rais Kikwete amesema pamoja na kutiwa saini hiyo bado Serikali itaendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo.

Pia Rais Kikwete ametoa wito kwa mwananchi yoyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko huru kutoa maoni yake na Serikali itasilikiza na kuchukua hatua zipasazo.

Hata hivyo tayari Rais Kikwete alifanya mazungumzoa na viongozi waandamizi wa CHADEMA, ambapo waliwasilisha mapendekezo yao kuhusu muswada huo na Rais kukubali kuendelea kuboresha zaidi sheria hiyo.

Pamoja na makubaliano hayo ya CHADEMA na Serikali kupita haijajulikana kama yataingizwa sasa katika kipindi hiki cha kuelekea kuundwa kwa tume au hapo baadaye.

Tuesday, November 29, 2011

Kikwete, Chadema Mwafaka

Rais Jakaya Kikwete (katikati) akiagana na Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kumalizika kikao cha siku 2 Ikulu Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar, Said Arfi. (Picha na Robert Okanda).

MUSWADAwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge hivi karibuni utasainiwa na Rais Jakaya Kikwete kama ilivyopangwa.

Hali hiyo inatokana na makubaliano yaliyofikiwa jana kati ya Rais na Kamati ndogo ya Chadema iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe.

Juzi na jana, pande hizo mbili zilikuwa na mazungumzo kuhusu Muswada huo ambao ulipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ushiriki wa wabunge wa Chadema na wa NCCR-Mageuzi ambao walisusia.

Kususia mjadala wa Muswada huo kwa wabunge hao wa vyama hivyo, ulitokana na madai yao ya kutaka Muswada huo usomwe mara ya kwanza bungeni wakidai haukuwa umesomwa na wananchi na kuuelewa, hivyo kukosa kuuchangia, lakini walikataliwa na Spika Anne Makinda.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa jana Ikulu Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi na Kaimu Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika, kutakuwa na haja ya sheria hiyo baada ya kusainiwa kuendelea kuboreshwa, ili ikidhi mahitaji ya kujenga na kuaminiana na mwafaka wa kitaifa.

Pia kutakuwa na mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba mpya.

Awali ilielezwa kuwa mazungumzo hayo yalifanyika katika mazingira ya uelewano ambapo Rais Kikwete aliwahakikishia Chadema kuwa yeye na Serikali yake wana dhamira ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba mpya.

Kulingana na hatua iliyofikiwa jana, Rais atasaini Muswada huo kuwa sheria ambayo inatarajia kuanza kutumika Desemba mosi, lakini wakati ikiendelea kutumika, kutakuwa na fursa ya kuifanyia marekebisho endapo haja itajitokeza.

Hili si jambo jipya kwa masuala ya uandishi wa Katiba mpya, kwani hata ya Kenya ilipitishwa na mpaka sasa zipo taarifa kuwa imeshafanyiwa marekebisho mara 11 kutokana na mahitaji yanayoibuka kwa kuzingatia mazingira na muktadha.

Makubaliano ya jana, yanamaliza sintofahamu iliyokuwa imeanza kuibuka kwa Chadema na makundi mengine kutaka kufanya maandamano nchi nzima, kupinga Muswada huo kusainiwa na kushinikiza urejeshwe bungeni kusomwa kwa mara ya kwanza.

Lakini pia kunatoa fursa pana kwa wawakilishi na wabunge kurudi kwa wananchi kuwahimiza kujitokeza kutoa maoni na mawazo yao kuhusu aina ya Katiba inayotakiwa na Watanzania wote.

Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilikubaliana kuwa ni jambo muhimu kwa mchakato huo kuendeshwa kwa namna ya kulinda na kudumisha tunu za taifa za amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Mkutano huo uliombwa na viongozi wa Chadema na Jumatatu iliyopita, ikaunda Kamati ndogo ya kumwona Rais, ikiongozwa na Mbowe huku wajumbe wengine wakiwa ni Mnyika, Makamu Mwenyekiti Bara, Said Arfi na Makamu Mwenyekiti Visiwani, Said Issa Mohamed.

Wengine ni Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Mwanasheria wa Chama hicho, Tundu Lissu, wajumbe wa Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari na Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halmashauri ya Chama hicho, John Mrema.

Upande wa Serikali katika mazungumzo hayo, uliwakilishwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
–Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani.

Monday, November 28, 2011

Msichana ajinyonga akibisha kupika chakula

MWANAFUNZI wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mbezi Juu, Kinondoni mkoani Dar es Salaam, amejinyonga kwa kutumia kitenge baada ya kubishana na kaka yake kuhusu nani apike chakula cha mchana.

Mwanafunzi huyo wa kike mwenye amri wa miaka 11 (jina limehifadhiwa), alikutwa amejinyonga chumbani kwake juzi akiwa amejitundika kwa kutumia kitenge kilichofungwa katika nondo ya dirisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema jana kuwa msichana huyo kabla ya kuchukua uamuzi huo, alibishana na kaka yake mwenye umri wa miaka 12 (jina limehifadhiwa) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo.

Alisema inavyoonekana, msichana huyo alichukua uamuzi huo baada ya kugombana kuhusu nani apike chakula cha mchana kwa kuwa baada ya ugomvi, aliingia ndani ya chumba chake
na ndipo baadaye mwili wake ukakutwa ukining’inia.

Katika tukio lingine, mfanyabiashara Ahmed Mguni (27), mkazi wa Mbagala Charambe amekutwa juzi amekufa na mwili wake umelala kitandani bila jeraha lolote.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alisema sababu ya kifo chake haijafahamika na kwamba Polisi wanaendelea na uchunguzi huku mwili wake ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alisema Polisi inamtafuta dereva
na gari lililomgonga fundi ujenzi aliyetambuliwa kwa jina moja la James (35) na kufa papo hapo.

Shilogile alisema fundi huyo aliyekuwa akitembea kwa miguu aligongwa na gari juzi asubuhi
katika eneo la Mvuti kwenye barabara ya kwenda Msongola.

JK akutana na CHADEMA, wawasilisha mapendekezo yao

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na ujumbe wa Serikali yake Novemba 27, 2011, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, yamefanyika katika mazingira ya urafiki na ujumbe wa CHADEMA umewasilisha mapendekezo yake kuhusu mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Tanzania. Serikali imepokea mapendekezo hayo.

Hata hivyo, pande zote mbili zimekubaliana kukutana tena leo asubuhi, Novemba 28, 2011, ili kuipa nafasi Serikali iweze kutafakari mapendekezo hayo.

Lakini pande hizo mbili zimekubaliana kuwa Katiba ya sasa ni Katiba nzuri iliyolilea Taifa kwa miaka 50 iliyopita kwa sababu ni Katiba ya sasa iliyoliwezesha Taifa la Tanzania kuwa na amani, utulivu na kupata maendeleo makubwa ambayo nchi yetu imepata mpaka sasa.

Pia pande zote mbili zimekubaliana kuhusu umuhimu wa kutunga Katiba Mpya kama Mheshimiwa Rais Kikwete alivyoliahidi taifa wakati wa salamu zake za mwaka mpya Desemba 31, mwaka jana, 2010, Katiba ambayo italiongoza Taifa la Tanzania kwa miaka mingine 50 ijayo.

Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Rais aliwahakikishia wajumbe hao wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuwa ni dhamira yake na ya Serikali kuhakikisha Tanzania inapata Katiba mpya.

Katika mkutano huo, pande zote mbili zimekubaliana kuwa ni jambo muhimu sana kwa mchakato mzima wa kutungwa Katiba Mpya kuendeshwa kwa namna ya kulinda na kudumisha tunu za taifa za amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Aidha, pande zote mbili zimekubaliana kuwa mchakato huo uendeshwe kwa kuzingatia misingi ya mambo mengine muhimu kwa taifa la Tanzania kama vile kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, kuligawa Taifa kwa misingi ya udini na ukabila ama kutugawa kwa misingi ya maeneo.

Zitto Na Demokrasia - Msimamo wangu: Kupandisha posho za wabunge ni ukichaa na kutojali Hali ya Nchi

Nimeshtushwa sana na taarifa za kupandishwa kwa posho za vikao kwa Wabunge. Nimeshtushwa zaidi kwamba Posho hizi zimeanza kulipwa katika mkutano wa Bunge uliopita kabla hata Rais hajaamua maana maslahi yote ya Wabunge huamuliwa na Rais Baada ya kupokea mapendekezo ya Bunge kupitia Tume ya Bunge.

Wabunge wote watambue kwamba kuamua kujipandishia posho zao bila kuzingatia Hali ya maisha ya mwananchi wa kawaida ni usaliti usio na mfano. Mbunge yeyote ambaye anabariki Jambo hili au anaishi hewani haoni tabunza wananchi au ni mwizi tu na anaona Ubunge ni Kama nafasi ya kujitajirisha binafsi.

Kwa Wabunge wa Chadema, wajue uamuzi kuhusu posho ni uamuzi wa chama na ni uamuzi wa kisera. Mbunge yeyote wa Chadema anayepokea posho za vikao anakwenda kinyume na maamuzi ya sera za chama tulizoahidi wananchi wakati wa uchaguzi. Nimemwomba Katibu Mkuu wa chama kuitisha kikao maalumu cha Kamati Kuu ya chama kujadili suala hili.

Toka tarehe 8 juni mwaka 2011 nilikataa kupokea posho za vikao. Popote ninapohudhuria vikao huomba Risiti ya fedha ninazokataa. Baadhi ya Wabunge Kama Januari Makamba wamekataa posho na hata kwenye semina ya kamati ya nishati alikataa na tumeona kwenye vyombo vya habari jina lake likiwa limekatwa ilhali viongozi wakubwa kabisa wamechukua posho. Nampongeza kijana mwenzangu kwa uzalendo huu. Nawataka wabunge wengine wenye Moyo wa dhati kukataa sio tu ongezeko hili la posho Bali posho yote ya vikao. Kwa nini mbunge akubali kulipwa kwa kukaa?

Tazama nchi hii, juzi serikali ilipokea Msaada wa tshs 20bn kwa ajili ya Sensa ya mwakani wakati wabunge wanalipwa 28bn Kama posho za kukaa tu.

Tanzania inaagiza gesi ya matumizi ya nyumbani kutoka nje kwa kutumia mamilioni ya dola za kimarekani. Kuwanda cha kutengeneza LPG kinagharimu tshs 35bn tu, Wabunge peek Yao kwa mwaka wanatumia 28bn kwa posho za kukaa tu achilia mbali mishahara na marupurupu mengine.

Ipo siku Watanzania watatupiga mawe kwa usaliti huu dhidi yao.

Friday, November 25, 2011

MAADHIMISHO YA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA


SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII TGNP WATAWASILISHA:

MADA: MAADHIMISHO YA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

Lini: Jumatano Tarehe 30 Novemba, 2011

Muda: Saa 03:00 Asubuhi – 08:00 Alasiri

MAHALI: Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni


WOTE MNAKARIBISHWA

TAMWA Yawakutanisha Wahariri Kujadili Ukatili Wa Kijinsia

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya (kulia) akizungumza katika warsha ya wahariri wa habari kutoka vyombo mbalimbali walipokutana kujadili vitendo vya Unyanyasaji wa Kijinsia jijini Dar es Salaam Novemba 23, 2011.


Baadhi ya wahariri wa habari kutoka vyombo anuai nchini Tanzania walipokutana Novema 23, 2011 kwenye semina kujadili masuala ya Ukatili wa Kijinsia, semina hiyo iliandaliwa na TAMWA kwa kushirikiana na UNFPA.

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) jana kimewakutanisha wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kujadili ukatili wa kijinsia kwa jamii. Hatua hii ni moja ya programu ya Kihistoria ya Siku 16 za wanaharakati kupinga ukatili wa kijinsia kwa jamii ambayo ilianzishwa tangu mwaka 1991 na Kituo cha Kimataifa cha Wanawake katika Uongozi (Centre for Women’s Global Leadership). Akizungumza katika semina hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya amesema lengo la semina kwa wahariri hao ni kuhakikisha wanafahamu mchango wa wanaume katika kupambana na ukatili wa kijinsia nchini Tanzania. Akifafanua zaidi Mkurugenzi huyo alisema lengo lingine ni kuhakikisha wahariri wanakuwa mstari wa mbele kuanzia Novemba 23 hadi Desemba 10 kuwaamsha kiutendaji pande husika kuchukua hatua juu ya vitendo hivyo vya kikatili. Aidha mada anuai zimetolewa kwa washiriki ili kujenga uelewa juu ya namna ya kutumia nafasi zao kwa vyombo vya habari na kuleta mabadiliko katika suala zima la ukatili wa kijinsia ambalo limekuwa likiwaathiri zaidi wanawake na wanafunzi hasa wa kike.Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ni “Miaka 50 ya Uhuru: Pinga Ukatili Kuimarisha Tanzania Huru”.