-Apitia mikataba ya Chenge
-Adaiwa kunusa hadi kwa DPP
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, amemzungumzia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, ambaye miaka yake 10 kwenye nafasi hiyo wakati wa Rais Benjamin Mkapa, nchi iliingia mikataba mingi mibovu, akisema 'atapekua' mikataba aliyosimamia Chenge na hatimaye serikali kuiridhia ili kubaini alipoteleza.
Hata hivyo, wakati akitoa ahadi hiyo muda mfupi baada ya kuapishwa jan Jumanne mjini Dodoma, Werema aliweka bayana ya kuwa bado Chenge anastahili sifa kwenye baadhi ya maeneo ya kazi alizosimamia.
Aidha, mbali na Chenge, Jaji Werema aliwasifu wanasheria wengine wakuu waliomtangulia akiwamo Jaji Joseph Warioba pamoja na Damian Lubuva, akisema ni wanasheria makini wa kujivunia.
Katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu ambapo Chenge alikuwa AG, taifa liliingia mikataba kwenye uwekezaji wa madini pamoja na mchakato mzima wa ubinafsishaji, mali za umma yakiwamo mashirika yakiuzwa kwa mikataba tata na ya bei nafuu.
Baadhi ya mikataba hiyo inafanyiwa marekebisho kwa sasa na hasa sheria husika mfano sheria inayohusu uwekezaji kwenye sekta ya madini, marekebisho ambayo msingi wake ni mapendekezo ya iliyokuwa Kamati ya Jaji Mark Bomani iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete.
Akijibu maswali kadhaa ya Raia Mwema kwenye viwanja vya Bunge, Werema alionyesha kumkumbuka Chenge kama mwanasheria makini kwenye sakata la kashfa ya mfanyabiashara Chavda, huku akisita kuzungumzia mikataba tata aliyoingia Chenge kama AG kwa hoja ya kuwa bado hajaipitia mikataba hiyo kuona maeneo tata aliyohusika nayo Chenge.
“Tunaweza kumlaumu Chenge katika baadhi ya maeneo lakini bado anayo haki yake ya kutambuliwa kama mwanasheria mahiri ingawa pia hicho kinachosemwa kwamba amekosoa bado sijapitia kuona wapi kulikuwa na tatizo.
“Mimi ni mtaalamu wa masuala ya mikataba kwa hiyo nitapitia kila kitu kuona wapi alikosea, lakini Chenge pia aliwahi kufanya kazi nyingine nzuri za kitaifa kama kesi ya Chavda,” alisema Jaji Werema.
Lakini wakati Werema akiingia ofisini na mtazamo huo, wapo baadhi ya watendaji waandamizi serikalini wanaomtazama kama mtu ambaye kwa sehemu kubwa anaweza kufanya kazi yake kwa mafanikio makubwa lakini wakati huo huo pia akajiharibia.
Wanaoamini kuwa anaweza kujiharibia wanaeleza kuwa wakati fulani amekuwa na hulka ya ubabe kiasi cha kuingilia mamlaka ya ofisi au idara nyingine baadhi wakinukuu kauli yake siku alipozungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam mara baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete.
Siku hiyo Jaji Werema aliwaambia waandishi wa habari kuwa atahakikisha kuwa kesi zote za serikali kabla ya kwenda mahakamani zimepitia ‘mikononi’ mwake ili kujihakikishia matunda yenye manufaa kwa taifa.
Kauli hiyo inatamzwa na baadhi ya wafanyakazi waandamizi wa Wizara ya Katiba na Sheria kuwa inaweza kuingilia mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Elieza Feleshi, ambaye kimsingi ndiye anayeamua kesi gani ipelekwe mahakamani na ipi isiende na ipi iliyopo mahakamani ifutwe.
Lakini pia Raia Mwema imepata habari kuwa tayari kiongozi huyo ameonyesha makucha yake ndani ya ofisi yake mpya akianza kuhoji ni kwa nini baadhi ya vigogo wanapewa ulinzi wa saa 24, akionyesha kutaka kufahamu kila chembe ya dondoo ofisini. Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kati ya vigogo wanaopata ulinzi wa saa 24 ni pamoja na DPP.
Hata hivyo, kuhusu madai hayo Werema ameieleza Raia Mwema kuwa jambo la muhimu zaidi ni kusimamia mfumo wa kiutawala na si kumfuatilia mtu na kusisitiza kuwa atakuwa mtu wa kusimamia na kufuata matakwa ya sheria, taratibu na mwongozo husika.
“Niseme tu kwamba nitafanya kazi zangu zote kwa mujibu wa sheria hii ikiwa ni pamoja na kuingilia maeneo mengine ambayo nitaamini mambo hayaendi vizuri lakini nasisitiza kwa mujibu wa sheria,” aliweka bayana msimamo wake.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe katika mazungumzo yake na Raia Mwema alisema katika muundo na mfumo wa Wizara hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali yupo juu ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ingawa pia kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania kila mmoja ana uhuru na mipaka yake.
“DPP yupo chini ya AG ndani ya Wizara na anawajibika kwake japokuwa ndani ya Katiba DPP anao uhuru wake ambao hata mimi Waziri siwezi kumuingilia,” alisema Waziri Chikawe ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma.
No comments:
Post a Comment