ZANZIBAR imeshauriwa kuunda Serikali ya Mseto ikilazimika kufanya hivyo, kwa sababu si jambo la aibu, bali ni sehemu ya demokrasia.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu, alisema jana kuwa watu hawatajisikia vibaya kuhusu uundaji wa Serikali ya Mseto kutokana na kuwa sehemu ya kuundwa kwa demokrasia ya kweli.
“Nafikiri rafiki zetu wa Zanzibar wakifikiria kuwa na Serikali ya Umoja si mbaya,” alisema Balozi Mwapachu na kuongeza: “Ingawa wanasiasa wengi katika nchi za Afrika Mashariki hupendelea serikali inayoendeshwa na chama kimoja.”
Alizungumza hayo baada ya kufungua mkutano wa demokrasia katika nchi za Afrika Mashariki ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea miaka 10 tangu kuundwa kwa EAC Novemba 1999.
Alisema Serikali ya Mseto imefanikiwa katika nchi nyingine kama za Ujerumani na Italia, huku akiunga mkono makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), akisema ni mwanzo mzuri wa upatikanaji wa amani Zanzibar.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala, alisema sababu ya watu wachache kujitokeza katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita inatokana na wananchi kuamini kuwa viongozi wanaochaguliwa hawaleti tofauti yoyote.
Alisema ni jambo la kawaida duniani uchaguzi unapofanyika kama wa mitaa, unakuwa na matokeo duni mpaka Uchaguzi Mkuu ambao wananchi wanaamini kuwa kura zao zinaweza kuleta mabadiliko.
Profesa Mukandala alishauri katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ufanyike kwa wakati mmoja ili kuhamasisha wananchi wengi kujitokeza kupiga kura katika kuchagua viongozi wa mitaa.
No comments:
Post a Comment