HATIMAYE mtambo mmoja kati ya mitambo 10 ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), umewashwa na kuanza kuingiza mewagati za umeme 10 katika gridi ya Taifa.
Akizungumza na HabariLeo, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Dk. Magesvaran Subramanian, alikiri kuwashwa kwa mtambo huo na kuongeza kuwa uliwashwa rasmi jana saa 6.04 mchana.
“Tumeanza kufanya kazi na mtambo mmoja namba moja ndio uliowashwa na mpaka sasa kila kitu kinakwenda vizuri tunatarajia mpaka kesho (leo), utakuwa umeshaanza kuzalisha megwati zote kumi,” alisema Dk. Subramanian.
Naye Mfilisi wa kampuni hiyo, Rugonzibwa Mujunangoma, alisema mtambo huo uliwashwa jana, lakini kwa wakati ule haukuweza kuzalisha umeme wote wa megawati 10 na kwamba kadri ulivyokuwa ukiendelea kuzalisha umeme, ndipo megawati zilipokuwa zikiendelea kupanda na kufika 10.
“Tangu mtambo uwashwe na hadi ninaondoka muda wa saa saba mchana, mtambo tayari ulishaanza kuingiza megawati 1.5, lakini hadi kesho (leo)), utakuwa tayari unazalisha megawati kumi, ikumbukwe hii ni mashine,” alisema Rugonzibwa.
Kuhusu mitambo mingine tisa, alisema mafundi na watalaamu wa masuala ya umeme wanaendelea na ukaguzi ambapo nayo haitochukua muda mrefu itawashwa wakati wowote.
“Kuwaka kwa mtambo huu ni dalili nzuri kuwa mitambo mingine nayo haitochukua muda itawaka, mafundi wanaendelea vizuri na kazi yao na kwa kweli hali inatia matumaini,” alisema mfilisi huyo.
Kampuni hiyo ya IPTL ina mitambo 10 ambayo kila mmoja ukiwaka utatoa megawati 10 na hivyo mtambo mzima wa IPTL unatarajiwa kutoa megwati 100, na hivyo kupunguza tatizo la mgawo wa umeme ambalo limeikumba nchi kutokana na kuharibika kwa mitambo ya Kihansi na Songas.
Rais Jakaya Kikwete aliagiza katikati ya mwezi uliopita kwa mamlaka husika kuwa mitambo hiyo ya IPTL iwashwe ifikapo Novemba mosi, mwaka huu ili kukabiliana na tatizo la mgawo. Imechelewa kuwashwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kuchelewa kwa malipo kwa taasisi zitakazohusika kuendesha mitambo hiyo.
No comments:
Post a Comment