-Inahusu zabuni ya kumpata bosi mpya NHC
-Alipuuza mapendekezo ya Ernst & Young
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kapteni (mstaafu), John Chiligati, amejitumbukiza katika kashfa mpya ya kupuuza kazi iliyofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Ernst & Young iliyolipwa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuendesha usaili wa kumpata Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), imeelezwa.
Kutokana na utata katika kupuuza mapendekezo ya kampuni hiyo iliyojijengea heshima nchini kwa kutoa taarifa kuhusu wizi wa Sh bilioni 133 kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri Chiligati ameshindwa kuweka bayana sababu za kuipuuza kampuni hiyo.
Habari za uhakika ambazo Raia Mwema imezipata zinaonyesha kuwa, mara baada ya kustaafu kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Martin Madekwe, miezi kadhaa iliyopita, Serikali kupitia Wizara anayoongoza Chiligati, ilitangaza kuwa wazi kwa nafasi hiyo sambamba na kukaribisha watu mbalimbali kutuma maombi kuwania nafasi husika.
Watu kadhaa walijitokeza kuitikia wito huo wa Serikali na kwa wakati huo, Kampuni ya Ernst & Young iliteuliwa katika taratibu rasmi za serikali na kupewa jukumu la kuendesha usaili na kupendekeza majina ambayo mojawapo litateuliwa na Waziri.
Taratibu za upatikaaji wa Mkurugenzi wa NHC zipo mikononi mwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye kwa sasa ni Chiligati, ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi. (CCM)
Hata hivyo, taarifa hizo zinafafanua kuwa baada ya Ernst & Young kulipwa takriban Sh milioni 32 kwa ajili ya kutimiza jukumu hilo , walikabidhi mapendekezo yao kwa Chiligati.
Taarifa zinaeleza kuwa Chiligati ‘alikalia’ mapendekezo hayo ya Ernst & Young na katika hali ya utata kutafuta kampuni nyingine ya Jijini Dar es Salaam na kuikabidhi kazi hiyo ambayo tayari ilikwishafanywa na Ernst & Young na kuichotea Sh milioni 12 nyingine kama malipo ya kazi hiyo waliyopewa.
Lakini utata zaidi unatajwa kuibuka pale Chiligati alipopenyeza jina jingine ambalo halikuwamo katika majina yaliyofanyiwa mchujo wa awali na Kampuni ya Ernst & Young, ikidaiwa kuwa msingi wa hatua hiyo ni kuhakikisha mtu huyo (jina linahifadhiwa) ndiye anayeteuliwa na wengine waliopitishwa katika mchujo kihalali na kwa mujibu wa taratibu wanabwagwa.
Mtu huyo anayedaiwa kulengwa na Chiligati hivi karibuni amejiuzulu kutoka katika kampuni moja ya kitaifa inayodaiwa kukumbwa na utata katika mwenendo wake wa utunzaji wa hesabu, kampuni ambayo iliitisha mkutano wa wanahisa wake hivi karibuni.
Raia Mwema ilifanya jitihada za kumpata Waziri Chiligati kama ilivyo kwa jitihada za kupata uongozi wa kampuni ya Ernst & Young kuzungumzia kadhia hiyo ambayo dhahiri inazua utata kwenye misingi ya dhana ya utawala bora na wa sheria.
Inaelezwa kuwa katika kadhia hiyo, licha ya Ernst & Young kulipwa milioni 32 za kazi iliyopewa, takriban Sh milioni 26 nyingine zilitumika katika shughuli iliyohusiana na usaili huo wa awamu ya kwanza ikiwa ni pamoja na kugharimia matangazo ya zoezi husika.
Juhudi hizo zilizaa matunda kwa kumpata Waziri Chiligati ambaye kwa wiki ya pili sasa yupo mjini Dodoma kwa ajili ya kushiriki vikao vya Bunge katika mkutano wake wa 17, lakini juhudi za kupata uongozi wa kampuni ya Ernst & Young hazikuzaa matunda baada ya uongozi huo kushindwa kutoa majibu ya maswali yaliyotumwa kwao kwa njia ya barua pepe.
Baada ya maelezo ya utangulizi kati ya mwandishi wa gazeti hili na Waziri Chiligati, mazungumzo yalikuwa hivi:
RAIA MWEMA: “Mheshimiwa Waziri, tueleze ni sababu gani zilikushawishi kupuuza mapendekezo ya Ernst & Young kampuni inayoheshimika, na kisha kuteua kampuni nyingine kufanya kazi hiyo iliyokwishafanywa?
CHILIGATI: “Nani kakueleza mambo hayo?
RAIA MWEMA: Tumepata taarifa za uhakika kupitia njia zetu za utendaji kazi wa kawaida.
CHILIGATI: “Sasa nenda kaandike kuwa mchakato wa kumpata mkurugenzi (wa NHC) unaendelea.”
RAIA MWEMA: “Bado swali la msingi linalohusu matumizi ya fedha za wananchi pamoja na mapendekezo ya kampuni ya awali kupuuzwa na kuteuliwa kampuni mpya kwa kazi hiyo hiyo, hujajibu Mheshimiwa Waziri…naomba majibu ili wananchi waelewe kinachoendelea kwenye shirika lao la taifa.”
CHILIGATI: “Nakwambia…sikiliza bwana…watu hawana shida ya kujua hayo yote, wewe nenda kaandike kwamba mchakato unaendelea na hivi karibuni na hasa mwanzoni mwa mwezi Novemba, mkurugenzi mkuu atatangazwa…nitamtangaza mkurugenzi mkuu…sawa?”
Mazungumzo na Waziri yaliishia hapo, na hasa baada ya Waziri kuingia katika kikao kingine kilichohusu kutolewa kwa muhtasari wa shughuli za Bunge kwa wabunge wote kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, mjini Dodoma.
Shirika la Nyumba la Taifa lipo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi na kwa kawaida, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo licha ya kuteuliwa na Waziri, huwajibika kwa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo.
Jukumu kubwa la NHC nchini ni kuwezesha upatikanaji wa makazi bora pamoja na majengo ya biashara, huku lengo kuu la msingi la shirika hilo ni kuwa shirika kiongozi katika sekta ya ujenzi wa makazi.
No comments:
Post a Comment