Friday, November 27, 2009

Vuguvugu hili jipya la wanawake liungwe mkono!

Na Padri Privatus Karugendo

HARAKATI za ukombozi wa mwanamke zimepiga hatua mpya baada ya wanaharakati wa kupigania haki za wanawake kuamua kuanzisha vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi.

Hatua hii imefikiwa baada ya jitihada za miaka mingi. Tunafahamu mengi yaliyofanyika kwenye Mpango wa Mwanamke katika Maendeleo na ule wa Jinsia na Maendeleo. Pamoja na mambo mengi na mazuri yaliyofanyika kupitia mipango hiyo niliyoitaja hapo juu, wanaharakati wa kupigania haki za wanawake walihisi mapungufu katika mchakato mzima wa kutetea haki za wanawake.

Bado mwanamke anakandamizwa, bado anawekwa pembeni katika uongozi, mfano chama tawala cha CCM uongozi wa juu umeshikiliwa na wanaume; mwenyekiti, makamu wenyeviti na katibu mkuu ni wanaume; uongozi wa kitaifa; rais, makamu wa rais, waziri mkuu, spika n.k. ni wanaume.

Kule vijijini mwanamke analima, anachanja kuni, anapika, anachota maji, analea watoto n.k. Upande mwingine mwanaume anafanya kazi kidogo lakini ndiye anayenufaika zaidi. Baada ya mavumo mwanaume ndiye anayepokea fedha, hasa zile za mazao ya biashara kama vile kahawa, korosho, chai na pamba.

Kuna habari kwamba kule Mbozi wanawake walifikia hatua ya kujinyonga baada ya kuona wanafanyishwa kazi kubwa ya kulima, kuvuna na kutunza kahawa na chai, lakini fedha zinaingia kwenye mifuko ya wanaume.

Mashirika ya kutetea haki za wanawake kama vile TGNP, TAMWA na mengine mengi, yameona kuna haja kubwa ya kuanzisha vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi ili kwenda sambamba na mipango mingine inayoendelea ya kumkomboa mwanamke kama vile Mwanamke katika Maendeleo na Jinsia na Maendeleo.

Inafahamika kwamba kumwelimisha mama ni kuielimisha familia nzima, ni kuielimisha jamii na ni kulielimisha taifa zima. Hivyo ukombozi wa mwanamke kimapinduzi ni kulenga katika kulikomboa taifa letu la Tanzania.

Changamoto iliyo mbele ya wanaharakati wa vuguvugu la Ukombozi wa Mwanamke Kimapinduzi, ni kuliangalia jambo hili kwa upana zaidi. Badala ya kuendesha vuguvugu la Ukombozi wa Mwanamke Kimapinduzi, waendeshe vuguvugu la Ukombozi wa Mwanadamu Kimapinduzi.

Hoja kubwa hapa ikiwa kwamba hata wale wote wanaoendeleza mfumo dume, wale wanaowanyanyasa na kuwatesa wanawake, wale wanaowaweka pembeni wanawake katika mfumo wa uongozi wa taifa letu, wanakuwa hawajakombolewa. Hawa nao wanahitaji ukombozi wa kimapinduzi.

Mwanadamu akikombolewa kimapinduzi ni wazi kutajitokeza usawa katika jamii zetu. Kuweka nguvu kubwa katika kuwakomboa wanawake na kuwaacha wanaume pembeni, ni kulishughulikia tatizo nusunusu na kesho na keshokutwa tutajikuta tukihitaji kubuni mbinu mpya za kuwakomboa wanaume kimapinduzi.

Kama inawezekana sasa hivi (kuendesha ukombozi wa mwanamke na mwanaume) kwa nini yote yaya yasifanyike kwa pamoja? Ingawa kuna ukweli kwamba akikombolewa mwanamke, taifa zima linakombolewa, bado kuna wanaume waliobobea katika mfumo dume; kuna haja ya kuubomoa mfumo huu kwanza ndipo tufuate ule wa kumkomboa mwanamke kwa lengo la kulikomboa taifa lote.

Changamoto nyingine ambayo ni ya hatari zaidi ni kule kuyaangalia mapambano ya ukombozi wa mwanamke kama uhasi ndani ya jamii: Kwamba wale wote wanaopigania haki za wanawake hawako kwenye ndoa; kwamba wanaharakati hawa wanaunga mkono ndoa za jinsia moja, kwamba wanaharakati wanaunga mkono maisha ya dada poa na kaka poa.

Mawazo haya hasi yanalenga kuvuruga jitihada zote zinazofanywa na wanaharakati wa ukombozi wa mwanamke kimapinduzi.

Ni wazi jamii yoyote ile inahitaji familia nzuri na zenye maadili bora. Hili wala halina mjadala. Lakini swali ni je; ni familia gani nzuri na yenye maadili bora?

Familia inayoongozwa na unafiki na kuonekana bora mbele ya macho ya watu wakati ndani ya familia kuna moto - mama anateswa, ananyanyaswa, hana furaha na wala hana hata dakika moja ya kuyafurahi maisha yaliyoumbwa na Mwenyezi Mungu, ndiyo familia bora?

Au ni ile ambayo mwanaume ana haki zote hata na ile haki ya kutafuta virusi vya ukimwi na kuvipandikiza kwa mke wake? Familia bora ni ukimya wa mwanamke? Familia bora ni kubeba msalaba?

Wateja wa kaka poa na dada poa wanatoka wapi? Wateja wa “vibustani” wanatoka wapi? Kama familia zetu zingekuwa bora na zenye maadili mazuri; kaka poa na dada poa wangepata wateja?

Mbona hatuwanyoshei vidole wale wote wanaovuruga maadili na kuyaharibu maisha ya watoto wetu? Mtu asiyekuwa katika ndoa hawezi kuweka misingi ya maadili bora? Kama masista na watawa wanakuwa msitari wa mbele kuweka misingi ya maadili bora, kwa nini akina mama wanaharakati wanyoshewe vidole pamoja na ukweli kwamba ndoa zao zilivurugwa na mfumo dume?

Uamuzi wa kuanzisha vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi, unawapatia nguvu wanaharakati kujitambulisha kama wanaharakati wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

Utetezi wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi ni dhana ya kisiasa, hivyo dhana hii inawaweka wanaharakati kwenye msimamo ulio wazi kiitikadi; kwa maneno mengine vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi kunaliweka suala la ukombozi wa wanawake katika nafasi ya wazi kiitikadi na kisiasa.

Kwa njia hii wanaharakati wanaweza kuhoji uhalali wa mifumo mbalimbali iliyopo ambayo inamkandamiza mwanamke na kuibua nyenzo kwa ajili ya uchambuzi na utendaji ambao ni wa kimageuzi.

Uchambuzi wa kina unaelekezwa kwenye miundo na mfumo dume wa mahusiano ya kijamii ambayo imejengeka kwenye miundo mingine mipana kandamizi na ya kinyonyaji.

Mfumo dume ni mfumo wa mamlaka ya kiume ambao unahalalisha ukandamizaji wa wanawake kupitia taasisi na mifumo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kisheria, kitamaduni, kidini na hata kijeshi. Mamlaka ya umiliki na udhibiti wa rasilimali na marupurupu na dhawabu nyingine kwa wanaume katika ngazi binafsi na kijamii unatokana na itikadi na mfumo dume uliotawala.

Mfumo dume unatofautiana kulingana na majira na wakati na unabadilika kutokana na tabaka, rangi, jamii/kabila, asili ya mtu, imani/dini na mahusiano yaliyopo katika miundo ya kimataifa ya ubeberu. Pia, kwa hali halisi ya wakati tuliomo, mfumo dume haubadiliki tu kulingana na sababu hizi bali una mahusiano na unachangia katika mahusiano ya kitabaka, rangi, kabila dini na ubeberu wa kimataifa.

Hivyo basi, ili kutoa changamoto stahiki kwa mfumo dume ni budi pia kuichambua mifumo mingine iliyo kandamizi na ya kinyonyaji ambayo mara nyingi hutegemeana.

Hivyo basi jukumu la kiitikadi la wanaharakati wa vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi ni kuielewa mifumo yote kandamizi, na jukumu lao la kisiasa ni kuibomolea mbali mifumo yote kandamizi ukiwemo mfumo dume. Mwelekeo ni kupambana dhidi ya mfumo dume kama mfumo kandamizi na sio dhidi ya wanawake na wanaume kama watu binafsi.

Kwa upande wa Afrika, mapambano ya ukombozi wa wanawake yana uhusiano wa karibu na hali iliyopita ya bara letu, kama vile muktadha wa kabla ya ukoloni, utumwa, ukoloni, mapambano ya ukombozi, ukoloni mambo leo, utandawazi n.k.

Mataifa ya kisasa ya Kiafrika yamejengwa ka kupitia migongo ya wanaharakati wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi ambao walikuwa wanapambana bega kwa bega na wanaume katika ukombozi wa bara hili. Baada ya uhuru mfumo dume ulisimika mizizi na kuwarudisha wanawake jikoni.

Ipo mifano mingi hapa Tanzania, inayoonyesha jinsi wanawake walivyosalitiwa na mfumo dume ulipofika wakati wa kushika madaraka ya kuliongoza taifa letu. Akina Bibi Titi Mohamed na wenzake ni mifano michache.

Hivyo wanaharakati wanaona kwamba wakati huu tunapojaribu kujenga Mataifa mapya ya Kiafrika katika milenia mpya, kuna haja ya kujenga pia utambulisho mpya wa wanawake wa Kiafrika, utambulisho wa kuwa raia huru wasioathiriwa na ukandamizaji wa mifumo ya uonevu na kandamizi.

Wanataka wanawake wawe na haki ya kupata, kumiliki na kudhibiti rasilimali, miili yao na kutumia vema sehemu chanya za utamaduni wao kwa malezi bora nakatika kuleta ukombozi wa kimaendeleo.

Ili vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi lifanikiwe, panahitajika maadili binafsi na maadili ya kitaasisi. Maadili binafsi ni pamoja na wanaharakati wa ukombozi wa mwanamke kimapinduzi wa kiafrika, mmoja mmoja, kudhamiria na kuamini katika msimamo wa usawa wa kijinsia wenye misingi ya ukombozi wa wanawake.

Pia kutambua kwamba haki za binadamu za wanawake hazigawanyiki, hazitenganishwi na zinafungamana na haki za binadamu duniani kote.

Aidha, kujenga mazoea yasiyoruhusu ukatili wa aina yoyote ile na kufikia jamii isiyokuwa na ghasia na kutokomezwa kabisa kwa ukatili wa kijinsia; haki ya wanawake wote kuishi bila kukandamizwa, kubaguliwa wala kunyanyaswa na mfuno dume; Haki ya wanawake wote kuwa na maisha endelevu na ya usawa, na kupata huduma bora za ustawi zikiwemo Afya, Elimu, Maji salama na usafi wa mazingira.

Kingine ni uhuru wa kufanya uchaguzi na mamlaka juu ya masuala ya miili ya wanawake ikiwemo haki ya uzazi, kutoa mimba, utambulisho na utashi wa utambulisho wa aina jinsia na mahusiano kijinsi; kujihusisha katika majadiliano ya masuala ya imani/dini, utamaduni, mila na hasa yale yanayolenga katika kuhalalisha kutawaliwa kwa wanawake kwa kutetea msimamo na mtizamo wa msingi wa haki za wanawake.

Maadili ya kitaasisi ni pamoja na kila taasisi ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi kudhamiria kutetea uadilifu, usawa na uwajibikaji kwa taasisi na mashirika yanayoongozwa na misingi ya ukombozi wa wanawake, kusisitiza na kutambua kuwa taasisi ya ukombozi wa wanawake haimaanishi isiwe ya kitaalamu, yenye ufanisi, nidhamu na yenye misingi ya uwajibikaji.

Mashirika ya wanaharakati wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi wa Kiafrika yawe mfano wa kuigwa miongoni mwa jamii na mashirika ya kiraia, yakihakikisha kuwa raslimali fedha na vitu zilizopatikana kwa kusudi la kuwaendeleza wanawake wa Kiafrika zinatumika kwa kusudi hilo, na sio kwa maslahi binafsi.

Vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi ni chachu mpya katika jamii yetu. Tunawajibika kuliunga mkono vuguvugu hili ili tuweze kujenga jamii yenye usawa na kuheshimu haki za binadamu.


Simu:
0754 633122

No comments: