Friday, November 20, 2009

Mrejesho wa GDSS: Mjadala juu ya Uchimbaji wa Madini Unaendelea.

Katika mfululizo wa semina za GDSS wiki hii ya tarehe 18.11.2009, mjadala juu ya uchimbaji wa madini uliendelea na muwasilishaji mkuu wa mada alikuwa ni mchungaji Magafu kutoka Chama cha Wachungaji Tanzania, ambaye aliwasilisha mada yake kwa kutumia video juu ya mgogoro wa mgodi wa North Mara unaomilikiwa na Barick. Katika mgogoro huo, madini ya sumu aina ya Sodium Cyanide yanayotumiwa kuchimbia dhahabu yalitiririka kutoka katika mgodi huo wa North Mara na kuingia katika mto Tegete, na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi, wanyama, na mazingira ya maeneo hayo. Wananchi wa maeneo hayo wanatumia maji ya mto huo kwa shughuli zao za kila siku, pamoja na mifugo yao. Wananchi wengi wamedhurika na mifugo kadhaa imeshakufa mpaka sasa, na mimea imikauka kabisa.

Washiriki wa semina baada ya kuangalia video hiyo, waliweza kuchangia na kutoa maazimio kadhaa ambayo walipendekeza yafanyiwe kazi na wanaharakati kutokana na madhara yaliyopatikana katika mgodi huo. Hapa chini ni baadhi ya michango na mapendekezo ya wanaharakati kutokana na mgogoro huo.

• Ipo haja kwa mawaziri wahusika –waziri wa usalama wa raia, waziri wa madini, na waziri wa mazingira– kuchukuliwa hatua kwa sababu ingawa walikuwa wanafahamu juu ya uchafuzi huu wa mazingira lakini hawakuchukua hatua yoyote na kuwaacha wananchi kupata matatizo yanayoendelea. Hata baada ya kuambiwa hawakuchukua hatua yoyote ya msingi dhidi ya wahusika wakuu, ambao ni Barick.
• Wanaharakati walihoji kwa nini mgodi huo wa North Mara bado haujafungwa mpaka sasa? Na kwa nini serikali imeendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua yoyote kwa wawekezaji hao? Ipo haja kwa wanaharakati kuweka maazimio ili rais aweze kupata taarifa juu ya uchafuzi na uonevu huu dhidi ya wananchi wake. Kwa sababu wanaharakati tayari wanao ushaidi wa kutosha juu ya uchafuzi huu ni vyema rais akaambiwa.
• Ipo haja kwa wanaharakati kutambua wale wote waliopo katika mapambano haya, ili iwe rahisi kwao kuunda mtandao wa pamoja wa kupigania madini na urithi wa nchi yetu, kwani kwa sasa ni vigumu kuunda mtandao wa pamoja wa kupambana na uvamizi wa nchi yetu.
• Wanaharakati waingie barabarni na kufanya maandamano ya kupinga uonevu huu wa watu wa Mara, kwani bila kuingia barabarani si rahisi kwa watu wengi kupata taarifa juu ya uvamizi huo. Serikali yenyewe imejaribu kuficha taarifa hizi mara nyingi lakini wameshindwa!
• Vyombo vya habari vilinyimwa kuonyesha picha kama hizi ili wananchi wengi zaidi wasiweze kupata taarifa juu ya uchafuzi huo. Hivyo serikali ilikuwa inajua juu ya hali halisi inavyoendelea kule North Mara lakini ikachagua kukaa kimya na kuendelea kuwakumbatia wawekezaji wale, hivyo kuna haja kwa wanaharakati kusambaza taarifa juu ya uchafuzi ule ili watu wengi zaidi wapate taarifa juu ya hali halisi inavyoendelea kule North Mara ili waweze kuingia katika harakati hizi za utetezi wa rasilmali zetu ili ziweze kuwanufaisha wananchi wa kawaida.
• Pawepo na maandalizi ya mjadala wa kitaifa juu ya unyonyaji na uonevu unaondelea juu ya rasilimali zetu hasa katika sekta ya madini. Semina za GDSS kama hizi ni sehemu mojawapo ya mijadala hiyo inayotakiwa endeshwe nchini nchi nzima. Mijadala hii itasaidia wananchi kufahamu juu ya uharibifu unaoendelea katika migodi, pamoja na wananchi wanavyopata tabu katika nchi yao.
• Wanaharakati walipendekeza iundwe kamati ndogo ambayo itafuatilia mambo ya madini, ikiwa na pamoja na kuandaa maandamano makubwa ya amani yenye lengo la kupeleka taarifa kwa wananchi kwa wingi zaidi, na kuibua hisia za kutetea rasilimali zetu.

Wanaharakati tuungane kupinga uonevu huu dhidi ya raia wanyonge.

No comments: