WANAFUNZI katika vyuo vikuu kadhaa nchini wanadaiwa kuishi maisha ya kubahatisha kutokana na fedha wanazozitegemea kutoka Bodi ya Mikopo kutowafikia kwa wakati mwafaka.
Ingawa taarifa zimedai kwamba vyuo vingi wanafunzi wake wamekumbwa na adha hiyo, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Tumaini, mkoani Iringa, ni miongoni mwa vyuo ambavyo baadhi ya wanafunzi walitoa taarifa kulalamikia hali hiyo.
Wanadai kwamba baadhi ya wanafunzi wanaotegemea mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wamekuwa wakipata mlo mmoja na wengine wakiomba msaada kutoka kwa wanafunzi wenzao.
“Watu wanaishi kwa mlo mmoja. Wengine wanaishi kwa kusaidiwa. Tunasaidiana kwa kukopeshana. Kwa kweli hali ni mbaya. Tunashindwa kuelewa tatizo ni bodi au chuo,” alisema mwanafunzi wa Udom, ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Taarifa kutoka chuoni hapo, zinasema wiki iliyopita, wanafunzi walianza kushawishiana kufanya mgomo. Lakini baadhi ya viongozi wa wanafunzi waliwasihi kwa kuwataka wawe na subira.
Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idris Kikula, alisema chanzo cha tatizo ni wanafunzi wenyewe kutokana na baadhi kusuasua kufanya udahili huku wengine akaunti zao walizopaswa kuingiziwa fedha kuwa na utata.
Profesa Kikula alisema katika wiki ya kwanza ya Septemba, wanafunzi 4,500 ambao ilikuwa wapatiwe fedha zao, kati yao, wanafunzi 3,900 akaunti zao zilikuwa na matatizo.
Pia wiki iliyopita, wanafunzi 500 walianza kuingiziwa fedha zao lakini baadhi yao ilibainika pia akaunti zao zilikuwa na utata.
“Tulikaa na serikali ya wanafunzi na tatizo hili limetatuliwa,” alisema Profesa Kikula na kusisitiza kwamba wiki hii, kundi hilo pia litapatiwa fedha hizo.
Alithibitisha kwamba wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza, wa pili na tatu wanaostahili kupata mkopo huo wa Heslb, fedha zao zimeshatolewa na bodi.
Akizungumzia kusuasua kwa wanafunzi kufanya udahili, Profesa Kikula alisema, “wanafunzi wengi walisuasua kufanya udahili kwa sababu sisi ni chuo tunajiendesha, kwa hiyo tulisema lazima walipie vyumba. Wengi wamechelewa kufanya hivyo.”
Hata hivyo, alisema chuo kinataka kijenge utaratibu kwa kushirikiana na bodi ili fedha hizo za mkopo ziwe zinapelekwa moja kwa moja kwa wanafunzi kwa kuwa licha ya usumbufu, ni hatari pia kwa chuo kuingiziwa mabilioni ya fedha ambazo si zake.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Heslb, Cosmas Mwaisobwa, alisema hadi kufikia Novemba 6, vyuo mbalimbali kikiwemo Udom na Tumaini, vilishapelekewa fedha kwa ajili ya wanafunzi walioidhinishwa kupata mkopo.
Kufikia tarehe hiyo, Sh bilioni 12.7 zilipelekwa kwa ajili ya wanafunzi wapya 5,363 katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Sh milioni 698 kwa ajili ya wanafunzi wapya 291 wa Chuo cha Tumaini.
Wakati Tumaini ilifunguliwa Oktoba 3 na Udom ilifunguliwa Oktoba 17, gazeti hili limebaini kwamba wazazi na wanafunzi wengi ambao majina yao yaliwekwa kwenye tovuti ya Heslb kuonesha madaraja ya mkopo, walidhani kwamba wangeweza kupatiwa fedha mara baada ya kuripoti chuoni.
“Walipofungua chuo, tulidhani kwamba baada ya kuwasili vyuoni, fedha hizo zingepatikana ndani ya muda mfupi.Lakini hali imekuwa tofauti, mtoto anasema wanaishi kwa shida sana nasi imebidi tusake japo hela kidogo kumtumia,” alisema mzazi wa mtoto anayesoma Tumaini, aliyejitambulisha kwa jina la Mama Mushi.
Wakati huo huo, Mwaisobwa alisisitiza kwamba majina yaliyotolewa kuonesha madaraja ya mkopo na asilimia zinazotakiwa kutolewa kwa waliofuzu vigezo katika mwaka huu wa masomo, siyo kigezo cha mwanafunzi kuingia chuoni na kukaidi kulipa gharama zinazotakiwa kwa kuwa huo siyo uthibitisho kwamba ameshapewa mkopo.
Aliliambia gazeti hili kwamba upo uwezekano wa baadhi ya wanafunzi wakawa wanalalamika wakati hawako kwenye orodha ya waliokwishaidhinishiwa kupewa fedha hizo.
Vile vile alitahadharisha kwamba malalamiko ya wanafunzi yanaweza kuwa yanatolewa na wale ambao bodi haijaidhinisha kama watapewa au la.
Wapo baadhi ya wanafunzi ambao hadi sasa fedha zao hazijatolewa kutokana na majina yao kuendelea kufanyiwa kazi na bodi.
Kundi lingine ni la wanafunzi ambao walichagua chuo zaidi ya kimoja. Hawa wanatakiwa wadahiliwe kwanza kwenye vyuo walivyoamua na kisha namba zao za udahili zipelekwe kwenye bodi ishughulikie mchakato wa kuwapa mkopo.
No comments:
Post a Comment