MAPATO katika Kituo cha Mabasi yaendayo Mikoani cha Ubungo (UBT), yameongezeka kutoka sh milioni moja kwa siku hadi sh milioni nne.
Wakati Kampuni ya Smart Holdings ilipokuwa ikikusanya mapato kituoni hapo ilidaiwa kuwa ilikuwa inakusanya sh milioni moja kwa siku, lakini baada ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuchukua jukumu hilo sasa zinapatikana sh milioni nne kwa siku.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji, Ahmed Mwilima, alitoa taarifa hiyo jana katika Baraza la Madiwani la Jiji na kusema kutokana na ongezeko hilo, inaonesha kulikuwa na mizengwe katika taarifa zilizokuwa zikitolewa awali kuhusu mradi huo.
Mwilima ambaye alikuwa akizungumzia juu ya mapato yatokanayo na mradi huo wa ukusanyaji mapato UBT, alisema halmashauri imegundua kuwa mapato yaliyokuwa yakidaiwa kukusanywa awali yalikuwa ni kidogo.
Alisema halmashauri haijaamua imkabidhi nani mradi huo kwa kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi wa utendaji wake na vielelezo vyote muhimu kwa ujumla ili kuepuka utata kama uliotokea awali.
“Suala hili ni nyeti, linahitaji umakini wa hali ya juu katika kulitekeleza na kabla ya kukabidhi mradi huu kwa yeyote. Ni vizuri halmashauri iendelee kuuendesha kwa sasa ili kujua uhalisia wa makusanyo yake na utendaji wake ili kabla ya kukabidhi au kutafuta mkusanyaji mwingine, halmashauri iwe tayari na maelezo yote muhimu yanayotakiwa kuhusu mradi huo ili kuepuka mtafaruku mwingine kama wa awali,” alisema Mwilima.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilianza kazi ya kukusanya mapato katika kituo hicho Novemba mosi mwaka huu kutokana na kumalizika kwa mkataba wa Kampuni ya Smart Holdings inayomilikwa na familia ya mwanasiasa mkongwe na Mbunge wa Kuteuliwa, Kingunge Ngombale-Mwiru.
Wakati wa usimamizi wa kampuni hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kutembelea kituoni hapo na kubaini kuwepo kasoro katika ukusanyaji wa mapato.
Alimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua mapato na matumizi ya makusanyo katika kituo hicho pamoja na Soko Kuu la Kariakoo.
Tayari CAG ametoa ripoti zake na kumkabidhi Waziri Mkuu ambaye wataalamu wake wanaendelea kuzifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment