Friday, November 13, 2009

Mrejesho wa Semina za GDSS

Utetezi Kuhusu Masuala ya Madini Katika Mtizamo wa Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi

Mada ya jumatano ya tarehe 11.11.2009 iliwakilishwa na Silas O’lang kutoka taasisi ya Revenue Watch Institute (RWI) na mchungaji Magafu kutoka Chama cha wachungaji Tanzania. Taasisi ya RWI inajenga uwezo kwa asasi za kiraia na kamati za bunge.

Wawakilishi walianza mada yao kwa maswali sita ya uchokozi kwa washiriki. Rasilimali ya madini ni ya akina nani? Ni nani anayefaidika na madini hayo? Ni jukumu la nani la kuhakikisha rasilimali ya madini inawanufaisha wananchi? Je uamuzi wa uchimbaji wa madini yetu ulifanyika kwa wakati muafaka? Je, usimamizi ukoje? Na sera zetu zipoje?

Katika kujibu maswali hayo, washiriki waliweza kuweka wazi kwamba, madini na uchimbaji wa madini hapa Tanzania haunufaishi wananchi wa kawaida, bali hunufaisha makampuni ya nje na baadhi ya viongozi wachache wa serikali.

Kaka O’lang alisema, Tanzania kuna matatizo makuu matatu ambayo yanasababisha sekta ya madini isitoe mchango mkubwa katika pato la taifa. Matatizo hayo aliyaeleza ni;

1. Sekta hii ya madini ilitarajiwa kuleta mapato kwa serikali kutokana na kodi ambayo ingesaidia kuinua huduma za jamii kama shule, hospitali, afya, nk Lakini kutokana na mfumo wetu wa sheria umetowa mwanya kwa makampuni haya kukwepa kodi, hivyo kuchangia kiasi kidogo sana katika pato la taifa.

2. Taraji la serikali ni kwamba sekta hii ya madini ingeweza kuongeza ajira kwa wananchi wa hapa nchini. Lakini kampuni hizi zinatumia teknolojia ambayo haihitaji wafanyakazi wengi sana na wanaohitajika ni watu ambao wanaujuzi maalumu. Pia walitarajia kutakuwepo na uwiano kati ya sekta hii na sekta zingine, lakini sekta hii haijakuza sekta zingine. Wawekezaji wamekuwa wakitumia malighafi zote kutoka nje. Na zaidi ya hayo, wananchi wengi walihamishwa kutoka katika maeneo yao ili kupisha uanzishwaji wa migodi hiyo, bila kulipwa fidia ya kutosha, kitu kinachozua migogoro isiyoisha katika maeneo hayo ya migodi.

3. Shughuli za uchimbaji wa madini zimekuwa na athari kubwa sana kwa mazingira na raia. Kwa mfano katika mgodi wa dhahabu wa Buhemba wawekezaji wameondoka na kuacha mashimo bila kuyafukia, na katika mgodi wa North Mara ambapo sumu kali ya migodini ilititirika hadi mto Tegete na kudhuru mamia ya raia na mifugo. Mapaka sasa serikali bado hajatowa tamko la wazi kuhusiana na uchafuzi huo, huku ikiendelea kuwatetea wawekezaji. Hali hii imekuwa ikisababisha migogoro ya mara kwa mara katika maeneo ya migodi.

Ukiachilia mapungufu hayo makubwa bado kuna swali la kujiuliza, ni kiasi gani cha mapato kinachopatikana katika sekta hii kinachokwenda kugharamia sekta ambazo zinagusa maisha ya kila siku ya akina mama, kwa mfano afya ya uzazi, maji, na nishati mbadala?

Washiriki wakichangia hoja hizo walipendekeza kupata tathimini ya mali iliyopo katika ardhi yote ya Tanzania na kufahamu itawanufaisha vipi raia wa kawaida?

Pia kupendekeza sheria ya madini iangaliwe upya. Wanaharakati wamepigia kelele mara nyingi bila mafanikio yoyote, na serikali imeendelea kushikilia msimamo wake wa kuifanya mikataba hii kuwa siri, pamoja na kuendelea kutoa misamaha ya kodi kwa wawekezaji katika sekta ya madini.

Swala la kuwasemehe kodi wageni bado liliibua majadiliano makubwa. Washiriki walisisitiza kwamba hakuna umuhimu wowote wa kuwasamehe kodi wageni kwa miaka mitano katika sekta ya madini, kwani hakuna ulazima huo kwa vile sekta hii aina ushindani ukilinganisha na sekta zingine.

• Wanaharakati walipendekeza kelele kuhusu uporaji wa madini ziendelee kupigwa zaidi. Inavyooenekana kwamba wananchi hawana sauti ya kutosha juu ya madini yao na serikali imewekwa mfukoni na wawekezaji katika sekta ya madini. Wanaharakati waandike zaidi katika magazeti, kuelimishana zaidi juu ya umuhimu wa kutetea rasilimali zetu ambazo ndio urithi wetu.
• Yaandaliwe Maandamano kwa wazira ya madini na kueleza haja yetu ya kutaka kuwa na sera ya madini ambayo itawanufaisha wananchi wote kwa usawa bila upendeleo wowote, ukilinganisha na sasa.
• Tujenge nguvu ya pamoja katika kudai haki za wananchi ambazo zinavunjwa na serikali kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa.kwa sababu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko tunayoyakusudia!

Mwisho, Wanaharakati wana nafasi ya kuleta mabadiliko kama wakiunganisha nguvu kwa pamoja.

No comments: