Rais Jakaya Kikwete amempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ)Amani Abeid Karume, na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Seif Sharif Hamad kwa kukaa kuzungumza kuondoa tofauti zao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwandishi wa habari wa rais, Msaidizi, Premi Kibanga, mbali na kufurahishwa kwa hatua hiyo, Rais Kikwete amewahakikishia viongozi hao ushirikiano wake na wa Serikali.
Rais Kikwete ameeleza kufurahishwa na hatua ya CUF kuitambua rasmi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kumtambua Rais Karume kama Rais wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mazungumzo ya viongozi hao ni muhimu ili kujenga msingi wa kuaminiana. Amesema, anaamini kuwa, uamuzi huo utasaidia katika juhudi zilizokuwa zinaendelea za kutafuta ufumbuzi matatizo ya kisiasa visiwani Zanzibar.
“Hii ni hatua kubwa na muhimu katika juhudi za kuleta umoja, amani na utulivu katika Visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Sina budi kuwapongeza Rais Karume na Maalim Seif kwa uamuzi wao wa busara unaojali maslahi mapana ya watu wa Zanzibar na Tanzania”.alisema
Rais amewataka Wazanzibari na wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla na Jumuiya ya Kimataifa, kuwapongeza, kuwaunga mkono na kushirikiana na Rais Karume na Maalim Seif kwa uamuzi wao wa busara na moyo wao wa ujasiri.
Rais Kikwete amesema, katika kipindi hiki, viongozi hao wanahitaji kupewa moyo ili waendeleze kwa kasi zaidi jitihada zao hadi kufikia hatma njema inayotarajiwa na wananchi wote ya kuishi kwa amani, umoja, upendo, mshikamano na ushirikiano kwa maslahi ya watanzania wote.
Mbali na hilo, amewataka watanzania wote kwa kauli moja kuwapuuza watu wanaobeza au kupinga jitihada hizo za matumaini au hata kujaribu kuzihujumu.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imempongeza Maalim Seif pamoja na viongozi wa CUF kwa kumtambua Rais Karume kuwa ni Rais halali wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Tamko la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar lililotolewa na ofisi ya Rais Ikulu, Serikali imempongeza Maalim Seif pamoja na Rais Karume kwa kumpokea kiongozi huyo wa CUF na kufanya naye mazungumzo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa hatua hiyo ya kizalendo imefungua sura mpya ya amani, utulivu, umoja na mshikamano wa wananchi wa Zanzibar na inafaa kuungwa mkono na kila mmoja pamoja na vyama vingine vya siasa nchini.
“Ni dhamira ya Serikali ya Zanzibar kukuza na kuendeleza hali hiyo ili kuhakikisha inawaridhisha wananchi
wote na kuwaletea maendeleo zaidi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na ustawi wa jamii kwa njia ya kushirikiana. Serikali inatoa wito kwa wananchi kuwaunga mkono viongozi hawa wawili walioongoza katika kufungua sura hii mpya ya kupigiwa mfano”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Tamko hilo lilieleza kuwa nia ya serikali ni kuona nchi inapiga hatua za maendeleo katika amani, umoja na mshikamano wa wananchi wote na kuondoa tofauti zisizo za msingi zilizokuwa zikiwagawa wananchi.
Tangu Januari 2007, vyama vya CCM na CUF vimekuwa katika mazungumzo ya kutatua mgogoro wa kisiasa Visiwani Zanzibar kwa lengo la kuleta amani na utulivu. Hata hivyo mazungumzo hayo ya kufikia mwafaka yalivunjika yalipofikia hatua za mwisho.
Wiki iliyopita, Rais Karume na Maalim Seif walizungumza na kuafikiana kuzika tofauti zao. Maalim Seif aliwatangazia wanachama wake uamuzi huo sambamba na kumtambua Rais Karume.
No comments:
Post a Comment