-Lowassa ahusishwa kuibua mgawanyiko
MZIMU wa mradi tata wa umeme wa dharura uliotolewa kwa kampuni ya Richmond Development LLC ya Marekani, umeliyumbisha Bunge, serikali na wanasiasa wazito na sasa upepo wa suala hilo unaonekana kutotabirika, Raia Mwema limebaini.
Suala hilo ambalo lilitarajiwa kujadiliwa katika Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge ulioanza jana, halimo katika ratiba mpya ya mkutano huo hali ambayo imewatisha wabunge na watendaji serikalini pamoja na wahusika wengine nje ya mfumo.
Tayari hali ya mgawanyiko wa wazi umejitokeza ndani na nje ya Bunge kwa kuwapo makundi yanayopingana, moja likiwa na katika mkakati wa kumsafisha na kumzamisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya mradi huo na lingine likiendelea kutaka mwanasiasa huyo awajibike zaidi kisiasa.
Makundi hayo ambayo yameelezwa kuwa ndiyo msingi wa mpasuko mkubwa ndani ya Bunge unaowahusisha wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kuwa “makamanda” wa vita dhidi ya ufisadi na wenzao ambao wamekuwa wakionekana kupingana nao dhahiri na kwa siri huku makundi hayo yakiwa na wafuasi hata ndani ya vyama vya upinzani.
Katika hali isiyo ya kawaida na ambayo ni kinyume cha matarajio ya wabunge wengi na wananchi kwa ujumla, Bunge limetoa ratiba ya mkutano wa 17 kwa wabunge isiyoonyesha kuwapo kwa siku ya kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge kuhusu wahusika wa kampuni ya Richmond Development.
Mkutano wa 17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulianza Jumanne wiki hii kwa wabunge kupewa ratiba hiyo isiyotaja uwasilishaji wa taarifa ya Serikali kuhusu Richmond, hatua ambayo ni nadra kutokea na ikizua mjadala wa chini kwa chini na baadhi wakiamini kuna mambo yanafanywa kwa faragha zaidi ya matarajio yao.
Hatima ya taarifa hiyo inatarajiwa kufahamika leo baada ya kikao cha wabunge wa CCM jana jioni na baadaye kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge itakayofanya maamuzi kuhusiana na ratiba ya mkutano huo wa ulioanza jana huku kukiwa na hadhari kubwa na wasiwasi miongoni mwa wabunge.
Imeelezwa kwamba makundi kuhusiana na tuhuma za ufisadi ndiyo yanayozidisha ugumu wa kamati ya CCM inayoongozwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ambayo imepanga kukutana na wabunge wa chama hicho mjini Dodoma.
Usiri uliopo na mazungumzo ya hapa na pale ni sawa na yale ambayo yaliibuka wakati iliyokuwa Kamati Teule ya Bunge, ikiongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ilipokuwa ikikaribia kulipua taarifa yake bungeni, ambayo iliangusha vigogo kadhaa, Februari 2008.
Kwa mujibu wa utaratibu na uzoefu wa mikutano ya Bunge, wabunge hupewa ratiba rasmi inayoonyesha mpangilio wa shughuli za vikao kwa kila siku na pia ratiba hiyo huwekwa wazi kwa waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa mkutano ingawa pia huweza kujitokeza marekebisho ya hapa na pale ambayo ni madogo kama nyongeza ya siku za vikao.
Safari hii hali inaonekana ni tofauti hapa bungeni mjini Dodoma ambapo waandishi habari waliitwa kwenye mkutano na Ofisa Habari Mkuu wa Bunge, Ernest Zulu, ambaye hakuwa katika nafasi ya kutoa ratiba rasmi ya mkutano huu wa 17 unaoendelea.
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari Zulu alieleza kuwa ratiba haijawa tayari kwa kuwa bado Kamati ya Bunge ya Uongozi haikuwa imekutana kwa wakati huo ambao alikuwa na mkutano na waandishi.
Kwa upande wa wabunge ambao wengi walitarajia ratiba waliyopewa jana Jumanne ionyeshe siku ya uwasilishaji wa utekelezaji wa ripoti ya Richmond, walionyesha kushangazwa zaidi na kwa kuwa walikuwa na mkutano wa kupewa muhtasari jana mchana waliahidi kuuliza swali hilo.
Suala la utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Richmond limepangwa kufikia tamati katika mkutano wa sasa wa Bunge baada ya kukataliwa katika mkutano uliopita.
Lakini pamoja na hayo, licha ya taratibu kuelekeza kuwa kamati za kudumu za Bunge na hasa Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge kuwa na fursa ya kutaka na kupewa ripoti za serikali kama hiyo ya Richmond, hali haikuwa hivyo wakati kamati hiyo ilipokutana jijini Dar es Salaam wiki moja iliyopita.
Katika vikao vyake vya Dar es Salaam kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli, William Shellukindo, iliahidiwa kuwa ripoti hiyo itawasilishwa mjini Dodoma wakati mkutano wa Bunge wa 17 ukiwa umeanza.
Jambo jingine tofauti ambalo limeanza kujitokeza ni kwamba tofauti na ilivyokuwa katika mkutano wa 16 wa Bunge ambapo taarifa ya serikali kuhusu Richmond iliwasilisha na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, safari hii katika mkutano huu wa 17 ripoti hiyo inatajwa kuwasilishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Taarifa zaidi ambazo zinadai kuwa taarifa kuhusu utekelezaji wa lala salama wa maazimio ya Bunge kuhusu Richmond baada ya kukamilishwa mchakato wake iliwasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye naye aliikabidhi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni.
Katika hali ya kawaida wakati wote ilikuwa ikitarajiwa kuwa muwasilishaji wa taarifa hiyo ni Waziri Mkuu na si Waziri Ngeleja kama ilivyojitokeza kwenye mkutano wa 16 wa Bunge.
Mara kwa mara katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo, Waziri Mkuu Pinda amewahi kuulizwa maswali kuhusu utekelezaji huo ambao Bunge linaamini kuwa unasuasua.
Kwa ujumla suala ya mjadala wa lala salama kuhusu Richmond umekuwa ukisubiriwa kwa hamu na wabunge wa kambi za utetezi wa waliotajwa kuhusika na kashfa hiyo pamoja na wenye msimamo mkali wakitaka yeyote aliyehusika achukuliwe hatua bila aibu.
Kambi hizo mbili zimetajwa kujizatiti katika malumbano ya hoja pindi mjadala huo utakapoingizwa bungeni huku kukiwa na taarifa za kambi mojawapo kujisafisha na hasa vinara wa kambi hiyo na kambi nyingine yenye msimamo wa wazi wa kutaka hatua zichukuliwa bila aibu ikijizatiti kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua.
Mmoja wa wabunge walioshtushwa na ratiba isiyoonyesha ni lini Richmond itaguswa bungeni katika mkutano huu ni Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii ambaye alikuwamo kwenye iliyokuwa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond ambayo ndiyo chanzo cha kung’oka madarakani kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.
Lakini wakati hali ikiwa hivyo, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule iliyofichua uozo wa Richmond na kupendekeza kati ya wanaopaswa kuchukuliwa hatua ni pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuiya na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, jana Jumanne alikutana na waandishi wa habari waliofika mjini Dodoma kuripoti habari za Bunge.
Katika mazungumzo yake hayo, Dk. Mwakyembe alizungumzia kile kinachoelezwa kuwa kukataa kuhojiwa na TAKUKURU kuhusu madai ya kupokea posho mara mbili kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la kila siku nchini.
Akizungumzia suala hilo Dk. Mwakyembe aliweka bayana kuwa hayuko tayari kuhojiwa na TAKUKURU ambayo inatiliwa shaka na hasa Mkurugenzi wake mtendaji kwa kuwa tayari kamati teule ya Bunge aliyoiongoza imependekeza achukuliwe hatua na kwamba yuko tayari kupelekwa mahakamani na wakutane huko.
Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliyewahi kusoma na kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliweka bayana kuwa alikataa wito wa taasisi hiyo yenye dhamana ya kupambana na rushwa ili ahojiwe kwa kuwa haina hadhi ya kufanya hivyo.
Kutokana na Mwakyembe kukataa kuhojiwa na taasisi hiyo ni wazi kwamba haijulikani kama anakiri kosa alilotakiwa kuhojiwa kuhusika au la na badala yake anataka wakutane mahakamani.
Mbali ya TAKUKURU ‘kutunishana misuli’ na wabunge, hali ni tete kwa Mkurugenzi wake, Dk. Hosea, ambaye pamoja na Kamati ya Nishati na Madini, kuelezea kuridhishwa na taarifa ya awali ya serikali kuhusiana na utekelezaji wa azimio namba 20, bado hatima yake iko mashakani.
Katika maelezo ya kamati yaliyosomwa na Mwenyekiti wake, William Shellukindo, Agosti mosi, 2009, kamati iliridhishwa na utekelezaji wa azimio namba 20 la Bunge ulioonekana kumpa afueni Dk. Hosea kwa kuwa hakukuwapo ushahidi wa kwamba alighushi nyaraka za Richmond na wala hakubadili taarifa ya watendaji wake.
Hata hivyo, hatima ya Dk. Hosea bado iko mashakani kutokana na wabunge wengi kuona kwamba mkuu wa chombo kizito kama hicho hapaswa kuwa na tuhuma zozote na kitendo cha kubainika kuzembea katika suala la Richmond kinampunguzia nguvu ya kuweza kupambana na rushwa na ufisadi mkubwa.
Kwa upande wa wanasiasa walioathirika na kashfa hiyo akiwamo Lowassa, hali bado si shwari kwa upande wao kutokana na uzito wa tuhuma dhidi yao na wepesi wa utetezi unaotolewa na wafuasi wao.
Kumekuwapo na maelezo kwamba Lowassa amekuwa akijiandaa kutaka kujitetea upya ndani ya Bunge huku kundi linalojitambulisha kupambana na ufisadi likiwa makini kujiandaa kujibu mapigo na kutoa siri nyingi zaidi kuhusiana na kashfa hiyo.
Kwa mujibu wa habari hizo baadhi ya wabunge wametishia hata kuihusisha serikali nzima katika sakata la Richmond, ikiwa ni moja ya njia ya kutaka kumkwamua Lowassa katika sakata hilo ambalo lineonekana kuwa kikwazo kwa mwanasiasa huyo machachari kupanda zaidi kisiasa.
No comments:
Post a Comment