RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume ameeleza kwa undani yaliyojiri katika mkutano kati yake na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na kumtaja kiongozi huyo wa CUF kuwa ni jasiri kutokana na uamuzi wake wa kwenda kuwatangazia wafuasi wake kwamba anamtambua kuwa ni Rais.
Rais Karume alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kuelezea mazungumzo hayo ya kisiasa yaliyofikiwa. Mkutano huo uliofanyika Unguja, ulihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.
Alisema Maalim Seif alimtumia salamu za kumuomba wakutane. “Nikamkaribisha nikasema njoo bwana tena tukazungumza sana.Kuna baadhi wakasema sijui nilimpa chai ya maziwa. Maneno yale siyo ya kweli,” alisema Karume na kufafanua kwamba kila mmoja alikunywa glasi moja ya maji, hali iliyosababisha kelele za kushangilia kutoka kwa mamia ya watu waliojitokeza katika mkutano huo.
Kwa mujibu wa Karume, Katibu Mkuu huyo wa CUF alimwambia kwamba chama chake kimeyaona maendeleo na akasema kama wakishirikiana, wataleta maendeleo zaidi.
Aliueleza umati huo kuwa Maalim Seif alisema, “sisi CUF tumewakosa, nanyi mmetukosa. Imefika wakati tusameheane. Tusahau yaliyopita, tugange yajayo. Hayo ndiyo maneno tuliyozungumza,” alisema Rais Karume.
Alisema kutokana na kauli ya kiongozi huyo wa CUF, alizingatia ubinadamu kwamba hata kama mtu amekosana na mwingine kwa miaka 100, mmoja akienda na kuomba kusamehewa, lazima anayeambiwa aseme yameisha.
Alisema baada ya mazungumzo hayo, Hamad alimwambia Rais Karume amuombee dua wakati akienda kuwaeleza wanachama juu ya tamko la Baraza Kuu la CUF la kumtambua rasmi.
“Akasema niombee dua, nami nikasema nakuombea kila siku,” alisema Karume na kuendelea kushangiliwa.
Karume ambaye kila mara hotuba yake ilikatishwa na vigelegele na sauti za kushangilia, alisema, “kwa niaba yenu wote na wapenzi wa CCM, nataka nimpongeze saana, mheshimiwa Seif kwa ujasiri wake. Maana halikuwa jambo rahisi kama hivi kuzungumza na watu wake ambao siku zote walishaelekezwa hivyo.” Aliendelea kusisitiza, “alikuwa jabali na jasiri. Si jambo jepesi. Kiongozi ye yote wa siasa lazima afike pahala aseme njia hii haifai.”
Rais Karume ambaye alisisitiza anawapenda wapinzani na kuwaona kama vile ni askari Polisi, alisema kitendo hicho kilichofanywa na CUF na CCM kisiwani humo, kitaleta mustakabali mpya katika siasa. Alisema upinzani si ugomvi na wala vita.
“Nawapenda sana hawa wapinzani. Ni kama askari Polisi. Kazi moja kubwa ya wapinzani ni kuwachunga walio madarakani wasipoteze njia. Ndo maana napenda wawepo watuongoze ongoze,” alisema na kusisitiza kwamba anaamini kwamba sasa amani ya kudumu imefika Zanzibar.
Alisema matokeo ya mazungumzo hayo, ni mafanikio ya vyama vyote na Watanzania kwa ujumla na wala hakuna mshindi katika hilo. “Huu si uchaguzi. Ushindi unapatikana kwenye uchaguzi. Amani na utulivu ni wa sisi sote,” aliongeza Rais Karume.
Wakati huohuo, Rais alisema baada ya mazungumzo hayo, wapo waliosema lipo jambo lingine lililozungumzwa. Bila kutaja jambo hilo, alihoji, “jipi lingine tuzungumze jamani? Hili la amani na utulivu ni dogo?” Ingawa hakuweka wazi, miongoni mwa mambo ambayo baadhi ya watu walikuwa wakihisi kwamba huenda yamezungumzwa ni suala zima la uundwaji wa Serikali ya Mseto (ya pamoja).
Karume alisema, “suala la amani tumehangaika nalo miaka mingapi? Wale wanaobeza ebu tuachieni. Kama kuna jambo jingine, milango iko wazi tutazungumza. Kama kuna lingine lenye mustakabali wa nchi, tutazungumza. Kila jambo lina wakati wake, waamuzi wake na mazingira yake. Wananchi wa Zanzibar msidanganyike waamuzi ni nyie wenyewe.”
Alisema Zanzibar wana utaratibu wao waliojiwekea. Alisema wakubwa wanaweza kupanga, lakini hatimaye uamuzi unatakiwa ufanywe na wananchi. “Naamini jambo lolote zuri la mustakabali hamtakataa, lakini msilazimishwe.”
No comments:
Post a Comment