WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema, mahari ni jambo zuri lakini zinasababisha wanawake wanyanyaswe kijinsia.
Waziri Mkuu amesema, watanzania wanapaswa kutafuta namna ya kuacha utaratibu wa kulipa mahari ili wanawake wasinyanyaswe.
Pinda amesema, zinahitajika juhudi za kulitazama suala hilo taratibu na kwa makini sanjari na kuanzisha vilabu katika shule za msingi na sekondari ili kutoa elimu kuhusu vitendo hivyo kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Waziri Mkuu ametoa changamoto hiyo, Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia, kwa kutumia Kauli mbiu isemayo ‘Siko peke yangu mwenye nia binafsi , uthubutu, na utayari wa kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia’
Amewataka Maofisa Maendeleo wa jamii kuwasaidia wanafunzi kuanzisha vilabu hivyo kwa kuwa ni kuna umuhimu wa kulielimisha kundi hilo ili jamii inufaike.
Pinda amesema, Serikali itaendelea kupambana na mila , desturi na imani zozote zenye madhara kwa jamii ikiwemo mila ya kukeketa, na mauaji ya Abino.
Amesema, Serikali itahakikisha kuwa utaratibu uliowekwa kisheria ,Kiutawala,kimila na kijadi vinalenga kulinda haki , utu na heshima ya wananchi.
“Kuwepo kwa vipengele vya kisheria na kiutawala vinavyokataza ukatili wa kijinsia hakutakidhi haja endapo jamii hatutakuwa tayari kupiga vita imani, mila, desturi, tabia na mienendo inayosababisha kuwapo kwa vitendo hivyo” amesema Pinda.
No comments:
Post a Comment