WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Celina Kombani amekiri kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi ulitawaliwa na vituko, uzembe, vurugu za makusudi na mtu mmoja kujeruhiwa kwa risasi kwa bahati mbaya pamoja na uchaguzi huo kwenda vizuri.
Aidha, katika hatua nyingine matokeo ya awali yanaonesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kwa asilimia kubwa katika mikoa mingi nchini.
Kombani ambaye alizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, alisema vurugu na vituko vilivyotokea katika maeneo mengi ni pamoja na baadhi ya watu kwa makusudi kukimbia na masanduku ya kura.
Alisema pamoja na vurugu hizo, uchaguzi huo katika wilaya 131 ulimalizika salama isipokuwa Kilwa ambayo kutokana na uzembe wa Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya hiyo, vifaa vilichelewa kusambazwa kwenye vituo na hivyo wananchi wa wilaya hiyo kulazimika kupiga kura jana na leo.
“Yaani mpaka saa saba mchana jana (juzi), masanduku yalikuwa hayajafika katika vituo, hii yote ni kutokana na uzembe wa huyu Mtendaji kwani tulishampa masanduku hayo tangu Oktoba mosi mwaka huu, pamoja na fedha za uchaguzi ambazo zilipelekwa Septemba 11,” alisema Kombani.
Akizungumzia vituko na vurugu alisema katika Mkoa wa Mwanza, mtu mmoja alipigwa risasi kwa bahati mbaya na polisi, baada ya kutokea vurugu na askari huyo wakati akituliza ghasia hizo, akafyatua risasi hiyo ambayo ilimpata na kumjeruhi.
Pamoja na hayo, pia Kombani alisema katika wilaya za Rufiji, Kahama, Kilindi na Geita, baadhi ya watu walikamatwa na polisi baada ya kupora masanduku ya kura na kukimbia nayo, muda mfupi kabla ya matokeo kutangazwa.
“Yaani ilikuwa ni vituko, kwa mfano Kilindi, wakati masanduku ya kura yapo tayari kusomwa, walitoka watu na kupora masanduku hayo na kukimbia nayo, lakini kwa bahati nzuri walikimbizwa na polisi na kukamatwa, hii ni dalili kuwa kuna kundi la watu lilidhamiria kufanya fujo,” alisema.
Alisema pamoja na vurugu hizo, katika Wilaya ya Geita, mgombea wa CUF alinusurika kifo baada ya kuokolewa na polisi baada ya kutaka kujinyonga kutokana na kushindwa katika uchaguzi huo hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Simon Sirro, alisema bado hajapata taarifa za tukio hilo.
Alisema hata hivyo kuna baadhi ya vyama kikiwamo CUF katika baadhi ya maeneo vilikataa matokeo.
“Ila sisi tunawaambia kuwa ni ruksa kwao kwenda mahakamani ndani ya siku 30 baada ya uchaguzi.”
Kwa upande wa vyama vya upinzani vimeendelea kulalamika na kudai kuwa CCM ilishirikiana na watendaji wa ofisi za wakurugenzi na wilaya kuwahujumu wakati chama hicho cha CCM chenyewe kilisema kushinda katika maeneo mengi kunaonesha vyama vya upinzani vimedorora zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Kinondoni, John Mnyika, alisema wagombea walioonekana kuwa tishio walienguliwa kwa madai wamedhaminiwa na kata.
Baadhi ya maeneo ambayo walienguliwa ni Sinza B, Sinza C na mitaa ya wilaya yote ya Handeni na Nkasi.
"Sisi tunaamini serikali imevuruga uchaguzi huu na watu waelewe kuwa matokeo ya uchaguzi huu si kipimo cha uchaguzi mkuu, huu ni uchaguzi wa ovyo ovyo tu, kwa sababu umesimamiwa na halmashauri lakini uchaguzi mkuu utasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Hata hivyo tumeona asilimia 30 ya kura hadi sasa tumepata Chadema hivyo tumepanda, mfano Wilaya ya Kinondoni tumeshinda mitaa ya Bunju A na B, Makoka na Ali Maua A”, alisema.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alilaumu ofisi za wakuu wa wilaya kuwa zilitumika kuharibu uchaguzi huo na kuahidi kwenda mahakamani kushtaki maeneo ambayo walionewa.
“Tukishafanya tathmini na kuona maeneo tuliyoonewa, tutakwenda mahakamani kufungua kesi kwa hujuma za maeneo hayo pekee, kwa sasa Kasulu kati ya mitaa 48 tumeshashinda 12 na Nguruka kati ya mitaa 14 tumeshinda minane”, alisema.
Naibu Mkuu wa Propaganda wa CCM, Tambwe Hiza, alisema chama chake kilitarajia kusikia malalamiko kutoka Upinzani kutokana na tabia ya kulaumu pindi wanaposhindwa.
Hiza alisema matokeo ya uchaguzi huo ambapo CCM imeshinda katika maeneo mengi yamethibitisha kuwa upinzani umerudi nyuma zaidi ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita na kuongeza: “Mfano Chadema kwa Dar es Salaam wameshindwa kusimamisha wagombea kwa asilimia 85”.
Alisema “ushindi huu unaonesha uchaguzi mkuu mwakani CCM haitapata ushindani mkubwa”.
Naye Martha Mtangoo, kutoka Dodoma anaripoti kuwa CCM mkoani humo imeshinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa asilimia 82 katika vijiji, mitaa na vitongoji mbalimbali. Taarifa za matokeo ya awali iliyotolewa jana mjini hapa na Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Kapteni mstaafu John Barongo, zilieleza kuwa katika Wilaya ya Bahi chama hicho kilishinda kwa asilimia 100 ambapo kati ya vijiji 56 imeshinda vijiji vyote na vitongoji 514 imeshinda vitongoji 508 ambapo bado taarifa za vitongoji vingine bado hazijapatikana.
Naye John Nditi, kutoka Morogoro anaripoti kuwa wanachama CUF Morogoro Mjini juzi usiku walikesha wakishangilia ushindi wa wenyeviti na wajumbe wa mitaa ya kata chache walizoshinda mjini humo ambapo chama hicho kilipata ushindi katika mitaa ya Unguu A na Manzese.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Raphael Ndunguru, alisema CUF katika uchaguzi huo ilitwaa mitaa 10, TLP minne na Chadema mmoja na kufanya idadi ya mitaa 15 wakati CCM ikishinda mitaa 259 kati ya 274.
Mugini Jacob kutoka Tarime anaripoti kuwa matokeo ya awali ya uchaguzi huo yanaonesha kuwa CCM iliibuka mshindi wilayani humo baada ya kutwaa viti 57 vya serikali za vijiji sawa na asilimia 78 huku Chadema ikiambulia viti 16 wakati katika mamlaka ya Mji wa Tarime CCM ilishinda viti 10 Chadema vinne.
Naye Anna Makange kutoka Tanga anaripoti kuwa matokeo ya uchaguzi huo yanaonesha CCM iliongoza kwa kupata mitaa 65 sawa na asilimia 74.7, CUF 22 sawa na asilimia 25.3 katika mitaa 87 iliyomo kwenye kata hizo na upande wa wenyeviti wa vijiji CCM ilipata viti saba sawa na asilimia 87.5, CUF kimoja sawa na asilimia 12.5 katika vijiji vyote vinane vilivyomo kwenye kata hizo 12.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Majuto Mbuguyu, kwenye ngazi ya vitongoji CCM pia iliongoza kwa kunyakua viti 18, CUF kitongoji kimoja na TLP kimoja cha uenyekiti katika vitongoji 20 vilivyomo kwenye kata hizo 12.
Naye Juma Nyumayo kutoka Songea anaripoti kuwa CCM mkoani humo pia iliongoza ambapo wagombea wake katika viti vya mitaa katika Manispaa ya Songea walishinda viti 63 kati ya 71 sawa na asilimia 89 ambapo Chadema na CUF vilijipatia viti vinane ikiwa ni ongezeko la viti sita ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.
No comments:
Post a Comment