Friday, November 20, 2009

Zaidi ya Bil 14/- zatafunwa TRA

-Wakaguzi mbioni kukamilisha ripoti
-Kigogo mtuhumiwa ajiuzulu kwa notisi ya saa 24
-Baadhi ya mabenki yahusishwa

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) sasa ipo kwenye wakati mgumu baada ya kuwapo kwa taarifa za wizi wa zaidi ya Sh. bilioni 14 uliofanyika kwa awamu ndani ya miaka tisa.

Raia Mwema linaweza kuripoti kwa uhakika kwamba kwa sasa wakaguzi wa ndani ya mamlaka hiyo wanahakiki wizi huo ili hatimaye kuchukua hatua mahususi.

Uhakiki huo mahsusi pia umethibitishwa kwa gazeti hili na Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Dk. Maceline Chijoriga ambaye, hata hivyo, alisisitiza kutoa fursa kwanza kwa kamati ya uhakiki (auditing committee) kuachwa kufanya kazi yake. Wizi huo uligundulika Julai mwaka huu.

Lakini wakati Mwenyekiti huyo akiwa na mtazamo huo, tayari mfanyakazi mmoja mwandamizi (jina linahifadhiwa) anayedaiwa kuhusishwa na wizi huyo amejiuzulu kwa notisi ya saa 24, miezi michache iliyopita lakini kukiwapo madai kutoka kwa maofisa wengine waandamizi kuwa kigogo huyo ameshirikiana na mtandao mpana wa viongozi serikalini na baadhi kwenye mamlaka hiyo na baadhi ya benki nchini, ikiwamo mojawapo maarufu iliyowahi kubinafsishwa kutoka mikono ya umma.

Taarifa za uhakika kutoka kwa maofisa watatu waandamizi kwenye menejimenti ya mamlaka hiyo zinaeleza kuwa mabilioni hayo yaliyoanza kuchotwa taratibu kuanzia mwaka 2000 yanatoka katika makato ya kodi maarufu kama Pay As You Earn (lipa kadiri unavyopata) ambayo hukatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi na kupaswa kuingizwa kwenye pato la taifa.

Inaelezwa kuwa makato hayo na hasa kutoka kwa wafanyakazi wa TRA nchi nzima yamekuwa yakichotwa taratibu na kuingia mifukoni mwa mtandao (syndicate) huo wa uhujumu na wizi na wakati mwingine TRA imekuwa ikilipa mishahara hewa kwa wafanyakazi waliokufa au kutokuwapo kazini kwa sababu nyingine za kawaida, kama kuacha au kuachizwa kazi.

Kwa mujibu wa habari hizo zilizofikishwa katika gazeti hili na jopo la maofisa watatu wa TRA, inadaiwa kuwa mbinu za kufanikisha uchotaji huo zilianza pale mamlaka kuandaa, kuidhinisha na kusaini ulipaji mishahara kutolewa kwa ofisa mmoja pekee, utaratibu unaotajwa kuwa ni kinyume kwa mujibu wa watalaamu wa masuala ya uhasibu na fedha.

“Huyu (anatajwa jina) aliandaliwa na kupewa mamlaka ya kuwa muandaaji mishahara na signatory. Ndiye aliyekuwa na sauti kwa chochote kuhusu malipo iwe mishahara au malipo mengine kwa hiyo imekuja kubainika na hasa baada ya ukaguzi wa hesabu kufanywa kwamba, kuna upotevu wa zaidi ya Sh. bilioni 14.

“Upotevu huo umetokana na wizi katika makato ya pay as you earn ya wafanyakazi wa TRA nchini na nyongeza ya mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi nyongeza ambayo hata hivyo haiendi kwa wahusika lakini pia kumekuwapo na malipo ya mishahara hewa kwa watu waliokufa au kuacha kazi,” alisema ofisa mmoja aliyekuwa akiungwa mkono na wenzake wawili ambao Raia Mwema ilithibitisha kwa utaratibu mahsusi kuwa ni wafanyakazi wa TRA makao makuu.

“Alikuwa na uwezo wa kufanya chochote katika system ya mishahara kwenye kompyuta na hata baada ya kutoa notisi ya 24 baada ya mambo kutibuka, system ilishindwa kuendeshwa kama kawaida na ililazimu aitwe kazini na alifanya kazi kwa siku mbili kuweka mambo tena sawa,” anasema ofisa mwinginen kwenye jopo hilo.

Inadaiwa kuwa kutokana na kushirikiana na baadhi ya vigogo TRA makao makuu na hata baadhi ya vigogo serikalini, mhusika huyo alijihakikishia usalama katika kuendeleza hujuma hizo hadi pale ukaguzi uliofanywa na kampuni moja ya ukaguzi wa hesabu kubaini kasoro hiyo ambayo awali, licha ya ukaguzi kufanyika taarifa zinadaiwa kutozaa matunda ikiwa ni pamoja na kuzuia tatizo kuendelea.

Katika mazungumzo yake na Raia Mwema kuhusu sakata hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya TRA Dk. Chijoriga alisema: “Ni kweli kuna auditing committee (kamati ya uhakiki) ndani ya TRA na hiyo inaripoti taarifa zake kwenye bodi kila baada ya miezi mitatu.”

Lakini kuhusu sakata hilo, alieleza: “Bado hatuwezi kutoa taarifa halisi juu ya nini kimetokea na hatua zitakazochukuliwa. Ni lazima kwanza tupishe kamati ifanye kazi yake na iwasilishe ripoti kwetu (bodi), tukianza kusema sasa nadhani si vizuri…kwa hiyo tuachie tufanye kazi yetu kikamilifu bila kuingiliwa.”

Raia Mwema pia iliwasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhani Kija ambaye hakutaka kuzungumzia kwa kina suala hilo la ujpotevu wa mabilioni ya fedha akitaja aulizwe Waziri wake, Mustafa Mkulo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo alikiri kushuka kwa kiwango cha ukusanyaji mapato TRA, lakini akishindwa kuweka bayana kuwa sababu ni kushuka kwa uaminifu miongoni mwa maofisa wa TRA na badala yake akitetea kuwa anachofahamu sababu ni mtikisiko wa uchumi duniani.

“Hilo suala la wizi aulizwe waziri ambaye ripoti hufikishwa kwake kwa hiyo kama amepewa ripoti rasmi ya ukaguzi atakueleza, lakini kuhusu kushuka kwa mapato kwenye miezi mitatu hii ni kweli yameshuka kwa asilimia 10 hivi na sababu siwezi kusema moja kwa moja ni uaminifu mdogo kwa watendaji hilo la uaminifu wanaweza kuzungumza TRA wenyewe, isipokuwa nafahamu sababu mojawapo ni mtikisiko wa uchumi duniani,” alisema Kija, ambaye aliteuliwa na Rais Kikwete kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Graye Mgonja. Awali kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

No comments: