Monday, November 23, 2009

‘Maslahi binafsi yanachochea mgogoro Loliondo’

UONGOZI wa Kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC), umesema, maslahi binafsi yakiwemo ya wanasiasa na baadhi ya watendaji serikalini, ndiyo chanzo cha mgogoro unaoendelea katika eneo tengefu la ardhi la Loliondo wilayani Ngorongoro ambako kampuni hiyo imepewa kibali cha kuwinda.

Mkurugenzi wa OBC Tanzania, Isaac Mollel, amesema, maslahi hayo binafsi yanachangia kuwepo kwa mgogoro huo, lakini kama sheria zikifuatwa, hakutakuwa na mgogoro katika eneo hilo ambalo Ortello imekuwa ikiendesha shughuli zake kwa kibali cha serikali tangu mwaka 1993.

Mollel alihoji ni kwa nini mgogoro katika kitalu hicho hutokea kila wakati serikali inapotaka kugawa vitalu na kila watanzania wakijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu, akitolea mfano wa mwaka 1993 na sasa miezi kadhaa kabla ya uchaguzi wa mwakani.

"Hili suala lina maslahi binafsi. Kwa nini linajitokeza kila tunapoelekea Uchaguzi Mkuu na ugawaji wa vitalu vipya? Mwaka 1993 ilikuwa vivyo hivyo, ingawa na mwaka huu kuna suala pia la ukame. Lakini pia msije kuidharau issue (suala) la ardhi kwa nchi za Afrika Mashariki,” alieleza Mollel.

Alisema,kwa kuwa Kenya ardhi ni tatizo, wapo baadhi ya watu kutoka nchi hiyo ambao wengi ni wa jamii ya wafugaji wa Kimasai, wameingia Loliondo na kuchukua ardhi, na kusababisha mtafaruku kwa jamii ya wenyeji.

Akifafanua zaidi suala la maslahi, alisema mgogoro huo pia ni baina ya Wazungu na Waarabu, akihoji kuwa kama kuna vitalu zaidi ya 100 nchini, kwa nini kitalu kimoja cha OBC tu kinachomilikiwa na Mfalme wa Dubai, Shehe Mohamed Rashid bin Maktoum kiwe na matatizo na siyo vingine.

“Suala ni la maslahi, kwa sababu hiki kitalu ni cha kipekee, kinapata wanyama wa aina zote, wanaenda na wanarudi. Sasa kuna watu wamevamia pale, hawana kibali chochote, sijui kama wanalipa fedha wapi, lakini wapo ndani ya eneo la OBC ambayo inalipia kila kitu serikalini na hawajachukuliwa hatua.

“Ndio maana tunahoji, inawezekanaje mtu akavamia eneo la mwenzake, akaachwa tu. Humuulizi, unachouliza wewe ni hela tu, na sijui kama hela hiyo inakwenda serikalini. Ziko kampuni zaidi ya kumi zinafanya kazi ndani ya kitalu chetu, lakini serikali imekaa kimya,” alihoji Mkurugenzi wa OBC.

Alisema kampuni hiyo inaamini kuwa kama sheria zikifuatwa, Loliondo hakuna tatizo wala mkanganyiko wa sheria kama inavyodaiwa na baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa na mashirika yasiyo ya kiserikali, hasa kwa sababu eneo hilo la OBC ni ardhi ya uhifadhi na wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

Alisema wao wako tayari kubaki na eneo la hekta za mraba 1,200 kati ya 4,600 za Loliondo, hasa baada ya kuipa Serikali ya Mkoa wa Arusha, Sh milioni 156 kwa ajili ya kupima eneo hilo kwa matumizi ya wakazi wake.

Kauli ya Mollel imekuja wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira leo inaanza kazi yake ya kufanya tathmini ya hali halisi huko Loliondo kutokana na kuwepo kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu baada ya wananchi waliovamia kitalu cha OBC kuondolewa kwa nguvu na Serikali ya Mkoa.

No comments: