Monday, November 30, 2009

`Uagizaji mitambo mipya ni Richmond nyingine`

-Yadaiwa kuna wanaotaka kufukuzia asilimia 10

Mtego mwingine wa kuingiza Serikali katika hasara kubwa ya mabilioni ya fedha unanukia baada ya kudaiwa kuwa maofisa wake wamekataa ushauri wa watalaamu wa masuala ya umeme na kung'ang'ania kuagiza mitambo mikubwa miwili ya kufua umeme kutoka nje ya nchi.

Wataalamu hao waliishauri serikali kuongeza mkataba na iliyokuwa kampuni ya kufua umeme ya Aggreko baada ya kuonekana kufanya kazi nzuri kwa kipindi cha miaka miwili lakini ushauri huo ukapuuzwa.

Baada ya ushari huo kupuuzwa, kampuni ya Aggreko iliamua kung'oa mitambo yake na kuihamisha nchini wiki kadhaa zilizopita.

Mwaka 2006 Serikali iliingia hasara kubwa kwa kuingia mkataba na kampuni hewa ya Richmond LLC ya Marekani, baada ya nchi kukumbwa na ukame uliosababisha kukauka kwa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.

Hali hiyo ililazimu Serikali kuipa zabuni kampuni hiyo tata kufua umeme wa dharura wa megawati 100 kwa mkataba wa miaka miwili, mradi ulioigharimu takribani Sh. bilioni 200.

Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili, mpango wa kuishauri Serikali ikatae kuongeza mkataba uliandaliwa na watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Vyanzo vyetu vimesema kuwa watendaji wa Tanesco waliishauri Serikali ikatae kuongeza mkataba na kutaka iagizwe mitambo mipya bila sababu za msingi.

Habari hizo zilidai kuwa gharama ya kuagiza mitambo hiyo zinafikia dola za Marekani milioni 82 (Sh. 107,281,000,000) mara mbili ya ile ya kampuni ya Aggreko ambayo ilikuwa Dola za Marekani milioni 42 (Sh. 28,782,600,000).

Gharama hizo hazijumuishi zile za mafuta ambayo yatakuwa yanatumika kwa kila mwezi kwa ajili ya uendeshaji.

Mitambo ya Aggreko ilikuwa inatumia mafuta ya Sh. bilioni tisa ambayo ni nusu ya gharama za uendeshaji wa mitambo ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Katika mkutano wa watalaam wa umeme uliofanyika jijini Dar es Salaam mwaka 2008, waliitahadharisha serikali kuwa kutatokea tatizo la upatikanaji wa umeme nchini na kutaka mikataba ya makampuni binafsi ya kufua umeme yaliyokuwepo yaongezewe mkataba.

Inadaiwa kuwa kampuni ya Aggreko ilitaka iongezewe muda na ilikuwa tayari kufanya kazi na serikali ili kukabiliana na tatizo la umeme linalolisumbua taifa hivi sasa, lakini haikuwezekana.

Kampuni ya Aggreko iliingia mkataba na serikali ili izalishe umeme wa megawati 40 mwaka 2006 ikiwa ni miongoni mwa kampuni tatu za kuzalisha umeme.

Kampuni nyingine ni Dowans, ambayo ilirithi zabuni ya Richmond, baada ya kubainika kuwa ni bandia. Dowans ilikuwa inazalisha megawati 100 kabla mkataba wake kusitishwa rasmi mwaka jana kutokana na mapendekezo ya Bunge.

Kampuni ya tatu iliyoingia mkataba na Tanesco ni Alstom Power Rentals iliyofanyia kazi zake mkoani Mwanza.

Licha ya kuonekana kuwa mitambo ya kampuni ya Aggreko haikuwa na dosari zozote, lakini maofisa wa Tanesco walishinikiza ile yenye matatizo ya Dowans inunuliwe na serikali kwa gharama kubwa.

Imedaiwa kuwa watu waliokuwa wanashinikiza kununuliwa mitambo mipya na kuacha ile ya Aggreko walitarajia kujipatia asilimia 10 kwa njia ya rushwa.

Akizungumzia madai hayo, Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Alyoce Tesha, alithibitisha kuwepo kwa mipango ya kuagiza mitambo hiyo mipya na kwamba zabuni imeshatangazwa.

Tesha alisema Serikali inataka kununua mitambo hiyo ambayo itakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 160 ambazo zitaingizwa katika gridi ya taifa.

Tesha aliiambia Nipashe hivi karibuni kuwa watatumia Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ya mwaka 2004 katika kutangaza zabuni hiyo kati ya siku 45 hadi 60.

Alihakikishia Nipashe kuwa hakutakuwa na njia ya mkato katika kuchagua kampuni itakayopewa jukumu la kuagiza mitambo hiyo kutoka nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Tesha, baada ya kupatikana kwa kampuni itakayoshinda zabuni hiyo, itapewa muda wa kuomba kutengenezewa mitambo hiyo kutoka nchi watakayoamua wenyewe

Tesha alisema ni bora nchi kukaa gizani kuliko kujiingiza katika mtego kama ulivyotokea mwaka 2006 baada ya kuipa zabuni kampuni ya kitapeli ya Richmond, ambayo kila siku ilikuwa ikilipwa Sh. milioni 152 hata kama haikuzalisha umeme.

Kashfa ya Richmond ilimlazimisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu sambamba na mawaziri wengine wawili walioiongoza Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi..

CHANZO: NIPASHE

No comments: