-Kikwete yaanza kumshinda
-Sasa hata Dk. Shein azoza
SIKU chache tu baada ya kutuma ujumbe kwamba akipita mwakani hatabeba mawaziri wazee, Rais Jakaya Kikwete ameanza kutekeleza azma hiyo kwa kuwatangazia mawaziri wake kwamba amechoshwa nao kwa kuwa hawamsaidii, imefahamika.
Habari ambazo Raia Mwema imepata zinasema kwamba Rais Kikwete na hata wasaidizi wake, Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wamekuwa wakali isivyo kawaida yao katika vikao vyao vya kazi.
Kwa mujibu wa habari hizo, katika kipindi kiasi cha wiki mbili zilizopita, Rais Kikwete amekutana na mawaziri wake mara mbili na katika vikao hivyo amesema waziwazi kwamba mawaziri wake hawamsaidii kama alivyotarajia wakati akiwateua.
"Hakikua kikao cha baraza, lakini alizungumza kwa ukali akiwaambia kwamba alipowateua alikuwa na matumaini makubwa nao kwamba atakuwa amepunguza kwa kiasi kikubwa uzito wa kazi.
"Akawaambia amekuwa akilazimika kufanya mambo mengi ambayo yangeweza kufanywa na mawaziri wake aliowaamini na akawapa dhamana," anaeleza ofisa mmoja wa serikali aliyezungumza na Raia Mwema wiki kwa masharti ya kutotajwa gazetini.
Mtoa habari huyo amesema wiki iliyopita Rais Kikwete alikuwa mkali kwa wasaidizi wake kuliko ilivyopata kutokea tangu aingie madarakani mwishoni mwa mwaka 2005.
Imefahamika kwamba kabla ya kikao cha wiki iliyopita, kilichofanyika nje ya Dar es Salaam, Rais Kikwete aliwaita mawaziri wake ghafla katika hatua ambayo ilizua hofu miongoni mwao wakiamini kwamba huenda alitaka kuvunja Baraza lake.
Habari zaidi zinasema katika kikao cha awali waziri mmoja mwanamke alikwepa kuhudhuria baada ya kupata fununu kwamba Rais Kikwete alikuwa amekerwa na baadhi ya kauli zake za hivi karibuni.
Habari zinaeleza kwamba, hata Dk. Shein ambaye anafahamika ya kuwa mara nyingi hana hulka ya ukali amebadilika, na sasa naye ameanza kuwa mkali waziwazi katika vikao vya utendaji.
"Kuna kikao kimoja ambacho baada ya Rais kumbana waziri mmoja kutokana na kuwasilisha waraka uliokuwa umejaa mapungufu, Makamu naye alizungumza kwa ukali akimtaka waziri huyo kuacha kufanya mambo bila kufuata taratibu," anasema mtoa habari huyo.
Anaongeza: " Katika kikao hicho Rais alimkatiza waziri huyo mara kwa mara akitaka ufafanuzi na wakati mwingine kumlazimisha waziri huyo kubadili baadhi ya mambo ambayo aliona yana makosa mengi katika waraka wake.”
Ukali wa ghafla wa Rais Kikwete, Dk. Shein na Pinda unatajwa kuwa umechochewa na utendaji usioridhisha wa mawaziri wengi unaosababisha viongozi hao wa juu kabisa kulazimika kufanya kazi ya ziada.
Katikati ya habari hizo ni hali kwamba mawaziri wengi wanashindwa kuitetea na kuisimamia Serikali ndani na nje ya Bunge, mbele ya umma na katika shutuma nyingi zinazotajwa kwenye vyombo vya habari.
Anasema mtoa habari huyo: "Rais alieleza wazi kwamba anakerwa na taarifa za mara kwa mara katika vyombo vya habari zikionyesha udhaifu mkubwa wa Serikali yake huku wasaidizi wake wakiwamo mawaziri wakishindwa kutoa hoja zenye nguvu au mkakati mahususi wa kukabiliana na taarifa hizo.”
Japo tathmini inaonyesha kwamba si rahisi katika muda mfupi uliobaki kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu kuwa na mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, Raia Mwema imearifiwa ya kuwa tayari mchakato umeanza ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa wa kuchunguza mienendo ya watu wakiwemo wajumbe wa sasa wa Baraza la Mawaziri na wajumbe watarajiwa ikibidi kufanyika kwa mabadiliko.
Habari zaidi zinaeleza kwamba yamekuwapo mapendekezo kwa Rais Kikwete ya kutaka abadili baadhi ya mawaziri waliopo kwa baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakitajwa kuwa wako msitari wa mbele katika inayotajwa kuwa ni vita ya ufisadi katika hatua ya kukisafisha Chama cha Mapinduzi (CCM) katika tuhuma za ufisadi na migawanyiko ya dhahiri ili kuvutia kura katika uchaguzi wa mwakani.
Mbali ya kuingiza sura mpya na kupunguza baadhi ya mawaziri, kuna taarifa kuwa yapo mapendekezo kwa Rais ya uwezekano wa kupandisha ngazi naibu mawaziri walioonyesha uwezo mkubwa.
Haya yakiendelea zimekuwapo taarifa za wizara mbalimbali ambako wafanyakazi wanawalalalimikia mawaziri wao kwa utendaji kazi usioridhisha.
Kati ya waliotajwa na wafanyakazi hao ni pamoja na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati; Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya na Naibu wake, Dk. Makongoro Mahanga; Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsha Mwangunga na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora, Sophia Simba.
Lakini akizungumza na Raia Mwema wiki iliyopita Chiligati alisema “hawezi kufanya mtihani na kujisahihishia mwenyewe.”
“Hayo maoni ya watu siwezi kuyaingilia, mimi siwezi kufanya mtihani na kujisahihisha mwenyewe lakini naamini watendaji ofisi wanajua naingia ofisini saa ngapi na natoka saa ngapi,” alisema Chiligati na alipoulizwa kuhusu shughuli za chama kuingilia majukumu ya serikali, alisisitiza kutotaka kujisahihishia mtihani.
Katikati ya mwezi huu akizungumza na vijana wa kutoka nchi mbalimbali za Afrika mjini Dar es Salaam, Rais Kikwete alituma salamu za mwanzo kwa wateule wake kwa kuwaambia vijana hao ya kuwa endapo atajaliwa kuongoza tena Tanzania mwakani, atafanya jitihada kubwa kuondokana na sura za wazee ambao atawabadilisha na vijana.
Akizungumza katika mkutano wa vijana hao wa kulea viongozi wa Afrika, Rais Kikwete alisema atafanya mabadiliko makubwa kwenye Serikali yake akshinda uchaguzi ujao.
Alisema Kikwete: “Wale viongozi wa rika langu, lazima waanze kuwaachia nafasi vijana. Tunahitaji wakuu wa wilaya vijana zaidi, wakuu wa mikoa vijana zaidi na hata mawaziri vijana zaidi. Ndivyo ilivyotokea kwetu sisi wakati tukiwa vijana.”
No comments:
Post a Comment