Wednesday, November 25, 2009

Amuua kwa sumu mtoto wa 'mtalaka'

POLISI wamemkamata kijana mkazi wa Kijiji cha Ufala, Kata ya Kilago wilayani Kahama mkoani Shinyanga, akituhumiwa kumuua mtoto kwa kumnywesha dawa ya kuua wadudu wanaoshambulia zao la pamba.

Inadaiwa kuwa, kijana huyo, Juma John (19),alifanya hivyo baada mama mzazi wa mtoto huyo, Limi Midone, kukataa kufanya nae mapenzi, walikuwa na uhusiano wa kimapenzi zamani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Daudi Sias, amesema, mtoto huyo, Coletha Simoni (3) alinyeshwa sumu jana saa mbili usiku katika kijiji cha Tulole.

Kwa mujibu wa kamanda Sias, kabla ya kumnyesha sumu mtoto, John alikuwa na ugomvi na mama wa mtoto huyo, unaosadikiwa kuwa ni ulisababishwa na wivu wa mapenzi.

Sias amesema, siku ya tukio, mtuhumiwa huyo na rafiki yake, Maganga Tanganyika,walitoka katika Kijiji cha Ufala na kwenda Kijiji cha Tulole, walipofika wakakaa baa iliyopo jirani na makazi ya mpenzi wake wa zamani.

Kwa mujibu wa polisi,John alimuacha rafiki yake hapo baa,akaenda nyumbani kwa Limi, hakumkuta, alimkuta mtoto huyo, akamnywesha dawa hiyo ya kuua wadudu.

Sias amesema, baada ya kumnywesha dawa hiyo, aliondoka na kurudi baa ili yeye na rafiki yake waondoke kurudi kijijini kwao Ufala usiku ule ule ili watu wasifahamu kilichofanyika.

Polisi wamesema, baada ya mama wa mtoto huyo kurudi nyumbani, Coletha alilalamika tumbo linamuuma, aliaga dunia wakati anapelekwa katika kituo cha afya.

Baada ya mtoto kufariki dunia wanakijiji wa Tulole walipiga simu kwa wenzao wa Kijiji cha Ufala kuwaeleza kuhusu tukio hilo, msako ulifanywa usiku huo huo, mtuhumiwa alikamatwa akiwa ana harufu ya dawa ya kuulia wadudu wa pamba katika nguo zake.

John amekiri polisi kuwa ni kweli alimnywesha Coletha dawa ya kuua wadudu wanaoshambulia pamba, mchakato wa kumpandisha kizimbani unaendelea.

No comments: