Friday, November 6, 2009

Hatima ya kashfa za Richmond, Kiwira yafikia kileleni

SAFARI ndefu ya mjadala mzito wa kashfa ya Richmond iliyotikisa nchi , sasa inakaribia ukingoni baada ya taarifa ya utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge kupangwa kuwasilishwa kesho kwenye chombo hicho.


Kuwasilishwa taarifa hiyo kumekuja wakati kashfa hiyo ya utoaji zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura kwa Richmond Development (LLC), ikiwa imeshasababisha mpasuko mkubwa ndani ya CCM, hasa wabunge tangu sakata hilo lilipoibuka bungeni Februari, 2008.


Wakati Richmond ikitarajiwa kutikisa Bunge kesho, taarifa ya sakata la mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ilikabidhiwa jana kwa Kamati ya Nishati na Madini, kuashiria kuwa wakati wowote itajadiliwa na chombo hicho cha kutunga sheria.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Shellukindo, ambaye jana alikuwa jijini Dares Salaam, aliithibitishia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa taarifa hiyo ya utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge itawasilishwa kesho kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote.


Serikali inatakiwa ieleze hatua ilizochukua katika kutekeleza maazimio hayo, ambayo pia yanahusishwa na kuwajibishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, ambaye inadaiwa kuwa chombo chake kilishindwa kubaini rushwa katika utoaji wa zabuni hiyo kwa Richmond.


Wakati wabunge wakiishinikiza serikali itoe taarifa hiyo baada ya kupewa miezi sita, joto la Richmond limepandishwa zaidi na uamuzi wa Takukuru wa kuwachunguza wabunge kwa tuhuma za kuchukua posho mara mbili wakati wanapotekeleza majukumu ya Bunge, kitu kilichotafsiriwa kuwa kinawalenga wale wanaoshinikiza kutekelezwa kwa maazimio hayo.


Wabunge hao, wakiongozwa na Spika Samuel Sitta wameitaka Takukuru kuachana na mpango huo, baadhi wakidai posho hizo ni haki yao na wengine wakidai taasisi hiyo haikutakiwa ifanye uchunguzi huo katika kipindi ambacho wamekuwa wakishinikiza kuchukuliwa hatua kwa mkuu wa chombo hicho.


Lakini kilio chao kimekumbana na tamko kali kutoka kwa Dk Hoseah ambaye alidai kuwa hatajiuzulu na kuwataka wabunge ambao hawampendi, kupigia kura za kutokuwa na imani naye, kauli iliyotafsiriwa kuwa ya kibabe na iliyozidisha chuki.


Huku wabunge wakiendelea kurushiana maneno makali mbele ya kamati iliyoundwa kuchunguza kiini cha ongezeko la chuki miongoni mwa wanachama na viongozi wa CCM, ikiongozwa na rais wa serikali ya awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kiasi cha baadhi kutaka kuundwa kwa tume huru kuchunguza upya sakata la Richmond, macho ya wengi sasa yatahamia kwenye mjadala huo kesho.


Akizungumza na Mwananchi hoja hiyo ya baadhi ya wabunge kutaka uchunguzi mpya, Shellukindo alisema hakutakuwepo na kurudi nyuma katika suala la Richmond na kwenda mbali zaidi akisema: "Labda Bunge livunjwe."


Shellukindo alisema Bunge limepanga kulimaliza suala hilo kesho na kuongeza kwamba, halitakubali kuona au kusikia taarifa yoyote ya serikali ambayo itachelewesha tena jambo hilo.


"Maazimio ya Bunge hayarudi nyuma; yanakwenda mbele; hakuna uchunguzi mpya unaoweza kufanyika tena kwa suala kama la Richmond. Hivi sasa tunakwenda kulimaliza jambo hili," alisisitiza Shellukindo.


Mbunge huyo wa Bumbuli alishangaa wanaotaka kujitetea sasa na akahoji: "Siku zote walikuwa wapi... mbona hawakujitetea kamati ilipowapa nafasi iweje waibuke leo."


Aliweka bayana kwamba, suala hilo lingeweza kumalizwa muda mrefu kama serikali isingekuwa na ganzi katika kulishughulikia kama ilivyofanya tangu ilipopewa maazimio hayo na Bunge Februari, 2008.


"Ni basi tu, hata hao wanaosemasema hivi sasa ni kwa sababu serikali yenyewe ilichelewa kutekeleza maazimio ya Bunge, lakini hili lisingekuwepo na tungekuwa tumeshalisahau," alisisitiza.


Kiwira, inayohusisha familia ya rais mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na waziri wa zamani, Daniel Yona, nayo imekuwa suala tete kila Bunge linapofanya mkutano wake na katikati ya mwaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliahidi kuwa serikali itautwaa mgodi huo unaodaiwa kuwa ulinunuliwa kwa bei ndogo na baadaye wawekezaji kushindwa kuanza kuzalisha umeme kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba.


Hadi sasa mjadala mzito ni juu ya utekelezaji wa maazimio 23 dhidi ya kashfa ya Richmond, ikiwemo kumwajibisha Dk Hoseah ambaye ameshajitetea kuwa azimio namba 20 la Taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini ilishaonyesha kuwa hana kosa.


Lakini, akizungumzia kinga hiyo anayoanza kuitumia Hoseah, Shellukindo alisema hakuna sehemu ambayo kamati imemsafisha bosi huyo wa Takukuru.


Dk Hoseah alitakiwa kujieleza kuhusu sababu za kuisafisha Richmond; kupuuzwa kwa ushauri wa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) na kutobaini kasoro kwenye zabuni hiyo kama ilivyofanya kamati. Serikali ilieleza kuwa Dk Hoseaa alikwishajitetea kwa Katibu Mkuu Kiongozi na anasubiri hukumu.

source: Mwananchi

No comments: