Na Jenerali Ulimwengu.
NIMEKUWA nikijadili suala la watu kukimbia kutoka maeneo ya shamba na kukimbilia mijini. Tumekwisha kuona kwamba watu hawa wanakimbilia mijini kwa sababu kadhaa, moja miongoni mwao ikiwa ni kwamba miji ndiyo imekuwa na ukirtimba wa hata hayo maendeleo haba yaliyopo, na pili kwa sababu viongozi wao wamehamia mijini kwa sababu maisha ya kijijini ni adha tupu.
Kwa ye yote anayefuatilia masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ukuaji wa jamii zetu katika historia ya nchi za Kiafrika takriban zote, hali hii haiwezi kumshangaza, kwani inatokana na historia tuliyoipitia. Hatutakiwi kusahau hata siku moja kwamba katika mambo mengi yaliyotuathiri na ambayo yamesababisha tuwe kama tulivyo, uzoefu wetu chini ya utawala wa kikoloni umekuwa na nafasi kubwa mno, kiasi kwamba kila tukifurukuta tunajikuta tunalazimika kukirejea kipande hicho cha historia yetu.
Kabla ya ukoloni jamii zetu zilikuwa ni makundi ya kikabila ambayo kwa kiwango kikubwa yalijitegemea na kujitosheleza, yakifanya kazi za jamii kulingana na mahitaji ya jamii kwa wakati ule. Makundi haya yalikuwa na mahusiano na maingiliano na makundi mengine ya karibu, mara nyingi uhusiano huu ukitokana na nasaba zilizokaribiana za makundi haya au historia ya ujenzi wa makusudi wa udugu minajili ya kumaliza vita na kujenga amani baina ya makundi haya.
Katika mkundi ya kikabila uzalishaji uliamuliwa na kutekelezwa kufuatana na utashi wa jamii, na matunda ya uzalishaji huo yalikuwa ni mali ya jamii iliyoyazalisha, kuanzia chini kabisa kwenye familia mahsusi iliyotekeleza majukumu yake vyema na kupanda hadi jamii nzima ambayo kwa pamoja imetimiza malengo iliyojiwekea.
Maamuzi yalikuwa yakifanywa karibu kabisa na wanajamii na sababu za maamuzi hayo zilieleweka vyema. Watawala walikuwa watu wanaojulikana na kila mwanajamii kwa sababu waliishi ndani ya jamii yao, wakifanya kazi bega-kwa-bega na jamii na wakishiriki katika kila tukio la jamii, katika msiba na katika faraja.
Inawezekana ninachora picha isiyo sahihi sana kwa kurahisisha mambo na kuyaremba kwa waridi na yasmini. Ni kweli kwamba jamii zetu hazikufanana zote; zilipishana, tena wakati mwingine kwa viwango vikubwa, na ama kwa hakika, zipo jamii zilizoishi kwa vipindi virefu kama jamii za watumwa na vijakazi wa jamii nyingine.
Itoshe tu hapa kusema kwamba kwa jamii iliyotamanika, jamii mwanana ambayo makabila mengine yangeiona kama jamii ya kupigiwa mfano, hivyo ndivyo ilivyokuwa: Jamii inayofanya kazi kwa kupanga yenyewe, kusimamia yenyewe utekelezaji wa kazi ilizojipangia, ugawanaji wa mazao kwa haki (siyo lazima usawa), na kutathmini shughuli zote hizo kwa pamoja, kwa uhuru, kama jamii.
Ujio wa ukoloni ulifanya jambo moja ambalo limetuathiri hadi leo. Jamii zetu zilifanywa ziache kuzalisha kwa ajili ya mahitaji yao na badala yake zifanye kazi kwa lengo la kukidhi mahitaji ya wakoloni. Tunajua kwamba hayo mahitaji ya wakoloni mara nyingi hayakusadifu na mahitaji ya jamii zetu, kwani hili halikuwa lengo la ukoloni. Wao walikuwa mabwana, nasi tulikuwa watawana wa kuwatumikia, basi.
Kama mahitaji ya wakoloni wakati huo yalikuwa ni mazao ya mafuta, au mazao ya mbao au vipusa vya ndovu, watu wetu walilazimishwa kuzalisha vitu hivyo, hata kama kufanya hivyo kulikinzana moja kwa moja na mahitaji ya jamii zetu. Hii ilikuwa ni imla ya watawala wetu nasi hatukuwa na chaguo katika uzalishaji tuliotakiwa kuufanya, wala hatukuwa na uhuru wa kupanga bei za mazao yaliyotokana na jasho letu, au hata kujua huko yanakokwenda mazao hayo yanakwenda kufanya nini na kwa faida ya nani.
Wale waliopitia historia ya mapambano dhidi ya ukoloni watakumbuka kwamba wakati wote harakati zilihusiana na suala la uzalishaji, nini kinazalishwa, kwa ajili ya kukidhi haja gani, na nani anufaike kutokana na uzalishaji huo.
Ziko jamii zilizokataa kulima mazao ambayo hayakuwa na faida kwao; ziko nyingine zilizong’oa mazao zilipoona kwamba zinanyonywa kwa kulipwa bei ndogo sana; na ziko zilizogoma ili kupinga kuchukuliwa ardhi yao kwa ajili ya kilimo cha mazao yaliyotakiwa ughaibuni badala ya mazao yaliyokidhi mahitaji ya jamii hizo.
Kuondoka kwa wakoloni na kuingia kwa utawala mpya kungetarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika jinsi maamuzi yanavyofanyika kuhusu uzalishaji ili jamii zetu zizalishe kwa mpangilio niliouleza hapo juu, yaani kwa mpangilio wao na kwa manufaa yao.
Kilichotokea ni kwamba utaratibu ule ule wa ukoloni uliendelea kama vile hakuna kilichotokea, na wananchi wakaendelea kupokea maagizo kutoka Dar es Salaam na kuyatekeleza, kama walivyokuwa wakifanya chini ya mkoloni.
Ili kuhakikisha kwamba matakwa yao yanatimizwa, katika uzalishaji na masuala mengine, wakoloni walikubali aina fulani ya utawala wa wenyeji ndani ya “serikali za mitaa”, kwa utaratibu wa “indirect rule” ulioasisiswa na mkoloni Frederick Lugard nchini Nigeria na baadaye ukasambazwa katika makoloni mengi ya Uingereza.
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment